Zitto: Iko siku nitashika nafasi kubwa Tanzania
Wananchi wa Kijiji cha Nyalubanda wakiwa wamembeba Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alipowasili katika kijiji hicho jana katika hafla ya kukabidhi gari la wagonjwa alilotoa ahadi katika kampeni za Uchaguzi wa mwaka 2010. Picha na Edwin Mjwahuzi
Kigoma. Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amesema
kutimuliwa uanachama na Chadema ni dhoruba inayomkumba mwanasiasa yeyote
anayefanikiwa na kwamba iko siku atashika “nafasi kubwa ya uongozi ya
kuwatumikia Watanzania”.
Zitto aliwasili mjini hapa
juzi, ikiwa ni siku chache baada ya Chadema kutangaza kumtimua uanachama
kwa kosa la kupeleka mgogoro wa ndani ya chama kwenye mahakama.
Alifungua
kesi Mahakama Kuu akitaka imuamuru katibu mkuu wa Chadema kumpa nyaraka
za mwenendo wa vikao vya Kamati Kuu vilivyomvua madaraka yote na
baadaye kukizuia chama hicho kumjadili. Hata hivyo mahakama ilitupilia
mbali shauri lake na Chadema ikatangaza mara moja kumtimua.
Akihutubia
mamia ya watu kwenye Kijiji cha Nyarubanda ambako alikabidhi gari la
wagonjwa, Zitto aliwatoa hofu wananchi hao walioonyesha shauku ya kujua
hatma yake na kuwaeleza kuwa hajawatupa, ataendelea kuwahudumia.
“Hakuna
kiongozi aliyefanikiwa kisiasa bila kupitia misukosuko ya kupingwa,”
alisema Zitto ambaye anamalizia kipindi cha pili cha ubunge wake kwenye
jimbo hilo.
“Waziri Mkuu za zamani ya India, Indira
Gandhi alifukuzwa na chama chake na aliamua kuunda chama kipya na
baadaye kuwashinda waliomfukuza katika uchaguzi. Kwa hiyo nawatoa hofu
kwa maana ninajengwa zaidi kisiasa.
“Nipo kwenye dhoruba ambayo inanijenga kisiasa na ipo
siku nitawatumikia Watanzania katika nyadhifa kubwa za uongozi.” Katika
mkutano huo ambao wananchi walimpokea wakiwa na mabango yenye ujumbe
mbalimbali kama “Mheshimiwa Zitto tulikuchagua wewe na siyo chama,” huku
mengine yakiandikwa “chama siyo bora, ubora ni utendaji kazi”.
Viongozi
mbalimbali wa CCM na vyama vingine vya siasa walijumuika kwenye uwanja
huo kumpokea Zitto na kushiriki naye kucheza ngoma za asili.
Baadhi
ya viongozi hao ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma,
Hamisi Betese, mkurugenzi wa halmashari hiyo, Michael Mwandezi na
viongozi wengine wa serikali za mitaa.
Akiongea katika
hadhara hiyo, Betese alisema kuwa kitendo cha Zitto kutoa gari ambayo
aliwaahidi wananchi kipindi cha uchaguzi ni utekelezaji wa ilani ya CCM
ambayo ndiyo chama tawala.
Aliongeza kuwa yeye kama
mwenyekiti wa halmashauri bado anamtambua Zitto kama mbunge wa Kigoma
Kaskazini mpaka hapo taarifa rasmi zitakapotolewa.
Wanakijiji
hao walishukuru Zitto kwa kutoa gari hilo wakisema litawasaidia kuokoa
fedha nyingi walizokuwa wakitumia kutafuta magari binafsi wanapokuwa na
wagonjwa wanaohitaji matibabu ya haraka.