Bunge: Zitto kulipwa mafao yake yote
>
Kaimu Kiongozi wa serikali shughuli za bunge pia ambaye ni Waziri wa Uchukuzi ,Samuel Sitta, akiagana na aliyekuwa mbunge wa Kioma Kaskazini ,Zitto Kabwe.
Kaimu Kiongozi wa serikali shughuli za bunge pia ambaye ni Waziri wa Uchukuzi ,Samuel Sitta, akiagana na aliyekuwa mbunge wa Kioma Kaskazini ,Zitto Kabwe.
Ikiwa ni siku moja tangu Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe kutangaza kung’atuka katika nafasi yake ya ubunge, Bunge limeeleza
kuwa mbunge huyo atapata mafao yake yote kama wabunge wengine.
Zitto
ambaye alitangaza juzi bungeni kuwa anaondoka baada ya kuvuliwa
unanachama wa Chadema aliahidi kuwa ‘Mungu akipenda’ atakuwa tena ndani
ya chombo hicho cha kutunga sheria Novemba mwaka huu baada ya uchaguzi
mkuu.
Kuondoka kwa mbunge huyo pia kunaifanya nafasi ya
uenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali(PAC) kuwa wazi kwa kuwa ndiye
aliyekuwa akiishikilia hadi alipotangaza rasmi juzi kuachia ubunge.
Akizungumzia
uamuzi wa Zitto na juu ya mafao yake baada ya kuamua kuondoka mwenyewe,
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema kuwa mbunge huyo
atalipwa mafao yake yote.
“Unajua Chadema wametangaza
kumvua uanachama Zitto lakini hawajampa barua, sasa yeye ameona kuwa
kuliko kuendelea na ubunge wake ni vyema akakaa kando. Kutokana na suala
hilo atalipwa tu mafao yake yote,”alisema Joel.
Katika
hatua nyingine, baadhi ya wajumbe wa PAC wamesikitishwa na kuondoka kwa
Zitto kabla ya muda wa Bunge la 10 kumalizika huku wakimwelezea ni
kiongozi aliyeweza kuwaunganisha katika kamati bila kujali itikadi za
vyama.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wajumbe
hao walisema aliwafanya wajumbe wa kamati hiyo kuwa familia na
aliwaamini na kuwaheshimu wote.
“Ni mtu aliyekuwa na ushirikiano na aliweza kutuunganisha bila kujali itikadi.
Alitufanya
kama familia na alituamini na kutuheshimu. Tunamtakia kila la kheri
katika mipango yake ijayo,”alisema Ismail Aden Rage (Tabora Mjini).
Mbunge
wa Mkwamtipura, Kheir Ali Khamis alisema kujiuzulu kwa Zitto ni suala
la Kikatiba asingeweza kuendelea kushika nafasi hiyo.
“Hili ni suala la Kikatiba haki ya kuwa mbunge inaondolewa ukishakuwa si mwanachama wa chama cha siasa,”alisema.
Alisema kutojiondoa mwenyewe kungeleta mgogoro kati yake na chama chake kwa kuwa tayari walishamvua uanachama.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy alisema kuondoka
kwa Zitto kunalenga katika kujipanga upya katika chama chake kipya cha
siasa.
“Yeye ni mwanasiasa atakaa hivi hivi? Na kwenye
chama chake ameshafukuzwa anaenda kukijenga chama chake cha ACT ili
katika uchaguzi ujao apate madiwani na wabunge,”alisema Keissy.
Mbunge
wa Ludewa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Deo
Filikunjombe alisema, “Zitto alikuwa kama baba ndani ya kamati na
kuondoka kwake kutaifanya kamati kuyumba.”
Filikunjombe
ambaye ni rafiki wa karibu wa Zitto alisema kamati hiyo itayaenzi
mazuri yake na kwamba kazi alizozifanya ndani ya Bunge zitaendelea
kukumbukwa.
Hata hivyo, Filikunjombe alisema, “Zitto
bado hajafukuzwa kwa sababu hajapewa barua rasmi ila yeye mwenyewe
ameamua kukaa pembeni kutokana na maneno yanayoendelea kusemwa pamoja na
ukimya wa chama chake.”