Askari wawili mbaroni kwa fedha bandia
>
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo akionyesha sare za jeshi la wananchi zilizokamatwa kutoka kwa askari polisi baada ya kupekuliwa nyumbani kwake. Picha na Faustine Fabian
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo akionyesha sare za jeshi la wananchi zilizokamatwa kutoka kwa askari polisi baada ya kupekuliwa nyumbani kwake. Picha na Faustine Fabian
Jeshi la Polisi mkoani Simiyu linawashikilia askari wawili
wa magereza na polisi kwa kukutwa na noti bandia ikiwa pamoja na sare za
Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Kamanda wa Polisi
mkoani hapa, Charles Mkumbo alisema askari hao walikamatwa juzi saa tisa
mchana katika Mtaa wa Old Maswa, Kata ya Nyakabindi, wilayani Bariadi.
Alisema
askari hao walifika kwenye kibanda cha Mpesa kinachomilikiwa na Mwalimu
wa Shule ya Sekondari Old Maswa, Kassian Luhende (29) wakiwa na
pikipiki aina ya Sunlg kwa lengo la kuweka fedha hizo katika simu.
Alisema
baada ya mwalimu huyo kupokea noti 10 zenye thamani ya Sh100,000
alizitilia shaka na kuamua kuzikagua zaidi ndipo alipogundua kuwa siyo
fedha halali.
Mkumbo alisema mwalimu huyo baada ya
kugundua hilo aliomba msaada wa kukamatwa kwa askari hao. Alisema
majirani walipofika walihoji, ndipo mmoja wao alipotoa kitambulisho kuwa
yeye ni askari na mwingine kujitambulisha kuwa ni dereva bodaboda.
Alibainisha kuwa baada ya wananchi kuambiwa hivyo
waliwatilia shaka zaidi na kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Bariadi
na kisha kukamatwa.
Mkumbo aliwataja watuhumiwa hao
kuwa ni askari mwenye namba H 2420 PC Seleman Juma (25) ambaye ni wa
Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Simiyu, na mwenye namba B.6499
WDR Edmund Masaga (28) wa Magereza wilayani Bariadi.
Kamanda
Mkumbo alieleza kuwa, baada ya askari hao kukamatwa mmoja wao PC
Selemani alipopekuliwa katika mfuko wa suruali yake, alikutwa na noti
nyingine za bandia za Sh100,000.
Mbali na hilo Mkumbo
alisema askari huyo alipopekuliwa nyumbani kwake alikutwa na sare za
JWTZ ambazo ni kaptula nne, fulana mbili, kombati moja pamoja na
kitambaa.
Alisema uchunguzi zaidi unaendelea ili
kubaini mtandao mzima wa usambazaji wa noti bandia ndani ya mkoa na
kwamba baada ya uchunguzi kukamilika askari hao watachuliwa hatua za
kinidhamu pamoja na kisheria
.