Aina tano za kuachana katika uhusiano
1. Kuchemka hadi kumwagika “The Boil Over”
Katika
hali hii unaanza kuziona dalili za kuachana kwenu kwa mbali. Labda
mwenzako amekuwa akifanya au kusema vitu fulani kwa muda mrefu na
vimekuwa havikufurahishi, kila unapotaka kumpasukia kuna kitu
kinakwambia “subiri, mpe nafasi nyingine”, ndani yako unajiona kabisa
kuwa wakati umewadia sasa wa kumpasha habari yake kwa mara ya kwanza na
ya mwisho. Pia ndani yako unakuwa na utayari wa kubeba majukumu kwa
chochote utakachomwambia. Ghafla siku moja kinatokea kitu kidogo tu,
labda ni neno lililosemwa au kitu kilichofanywa na wewe au mpenzi wako,
mnagombana na kutofautiana sana na kutokana na machungu na maumivu ya
muda mrefu moyoni mmoja anaamua kuutumia upenyo huo kulitamka neno “it’s
over” (naomba tuachane) na huo unakuwa mwisho wa penzi lenu.
2. Kuachana kimlipuko
Yako
baadhi ya uhusiano ambayo huwa yana vipindi vya amani kwa kitambo
kidogo na milipuko ya ugomvi kwa kipindi kingine. Milipuko hii
simaanishi kule kutoelewana kwa kawaida bali uhusiano unaokumbwa na
milipuko ya kutoelewana kwa kitu fulani kizito au ugomvi, unakuwa mzito
na wenye kuyumbisha pande zote mbili. Kwa mfano baada ya kitambo cha
amani na mapenzi kunagundulika kuwapo kwa uhusiano wa pembeni kwa mmoja
wa wapenzi (cheating) na hili linazua mlipuko wa ugomvi ambao ghafla
unalizima penzi na ule ukaribu wenu unafifia ghafla na kutokomea jumla.
Yamkini ni mlipuko mmoja tu umetokea, lakini mpenzi mmoja aliyeumizwa
hatamani hata kumwona mwenzake kwa macho, wapendanao hawa wanajeuka
maadui ghafla (one blow away).
3. Leo nje kesho ndani, kesho baridi keshokutwa moto
Hii
ni staili ya kuachana ambayo wengi wetu huitumia mara kwa mara na mara
nyingine pasipo mhusika mmoja katika penzi kufahamu kwamba safari ya
kuachana ndo inawadia. Katika uhusiano wa watu wa namna hii, kunakuwa na
mazingira yanayowafanya leo wanakorofishana kesho wanapatana, kesho
wanakuwa pamoja keshokutwa unaskia hawapo tena pamoja, mara unasikia
wamerudiana, tena wanakuja kufarakana na tabia hii inakuwa ndo maisha
yao ya kila siku na mfumo wa uhusiano yao. Tabia hii huendelea kudumu
hadi inafika nyakati mmoja akitoka basi anatoka jumla, kila mwenzake
akiwaza kwamba yamkini atarudi kama mazoea yao yalivyo lakini haiwi
hivyo tena na penzi lao linakatikia hapo.
4. Mkate ulioungua
Mara nyingi tunapopika mkate huuweka kwenye joto kali
ili uive na mara kwa mara muokaji huuangalia kama umeiva kwa
kuutumbukizia kitu kikali kama vile uma ili kuangalia hali yake ya ndani
ilivyo na kufahamu maendeleo ya uivaji wake. Mkate uliosahaulika
kuangaliwa mara kwa mara huungua na muokaji anapokuja kuutoboa ndipo
anapofahamu kuwa mambo yameshaharibika kuanzia ndani na mkate haufai
kuliwa tena.
Katika uhusiano wetu hususani kwa baadhi
ya wale walioweza kukaa muda mrefu au hata waliooana, bahati mbaya kwa
sababu ya masumbufu ya maisha ya kila siku na mapenzi ya kimazoea
wakasahau kuchochea na kuziamsha hamasa za penzi lao kila mara, penzi
hilo taratibu hushuka na kupoa ladha na taratibu pasipo wapendanao hawa
kugundua kila kitu kinakuwa chabaridi, kilichoganda, kisicho na ladha na
kilammoja akitamani penzi la ladha ya tofauti kutoka kwa mtu wa
tofauti. Hii inasasababisha wawili hawa kuchagua kuachana.
5. Ghafla moto ghafla baridi
Kama
umewahi kutumia mashine ya kupashia joto chakula “microwave” utaelewa
kitu ninachojaribu kuzungumza hapa, tabia ya mashine hii ni kupasha joto
chakula kwa haraka sana na mara kikitoka huweza kupoa kwa haraka zaidi
pia. Yako mapenzi ambayo yameanzishwa ghafla sana (kwa muda mfupi sana)
na yakapaa juu sana, kila mmoja akimhisi mwenzake kiukaribu sana, na
hisia za wawili hawa zinakuwa za moto kama zilizo wekwa kwenye
‘microwave’ lakini ghafla mmoja kati ya wapendanao hawa anazimika na
kutoendeleza tena moto uliokuwepo. Kwa mfano mlianza ghafla kuhusiana na
mapenzi yakawa moto kuliko mlivyofikiri, kila siku mko wote na lazima
muonane au muwasiliane kwa simu, ghafla mwenzako hapokei simu na wala
akiiona simu yako hawajibiki kukupigia au kukwambia nini kinaendelea na
tabia hiyo inaendelea hivyo hivyo hadi unakata tama na unaamua kukubali
yaishe.
Mapenzi haya yaliwaka na kuzima kwa mtindo wa
microwave. Wakati unahisi penzi lenu linafikia mwisho ni vyema mkafikiri
njia bora za kuachana na maranyingine ikibidi kuliongea hili kwa
pamoja. Baadhi ya zinazoweza kuwa na madhara makubwa na ya muda mrefu
kwa wahusika au muhusika mmoja na nyingine madhara yake ni madogo na
yasiyo ya muda mrefu.
Wakati wote tunashauri kuachana
isiwe ndiyo njia mbadala ya kwanza bali jitihada za kusuluhisha na
kubadilika tabia ziangaliwe kwanza na kupewa kipaumbele na kila
anayehusika katika penzi.
Kumbuka kuwa katika jitihada
za kubadili tabia ni zoezi linalotakiwa kusaidiana baina ya wawili
wapendanao na siyo kazi ya mtu mmoja. Nakutakia kufanikiwa zaidi katika
uhusiano yako na sio kukimbilia kuachana.