‘Asilimia 80 ya wabunge hawafai’
>
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa akifafanua jambo
alipokuwa akifanyiwa mahojiano maalumu na waandishi na wahariri wa
magazeti ya Mwananchi Communications Limited, alipotembelea ofisi za
magazeti hayo Tabata Relini, Dar es Salaam jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa
amesema zaidi ya asilimia 80 ya wabunge waliopo bungeni sasa
hawakustahili kuwa wabunge kwa sababu baadhi yao wana uwezo mdogo
kiakili alioulinganisha na GB moja ya kompyuta.
Msigwa
alisema kwa maoni yake, ni asilimia 20 pekee ya wabunge ndiyo wenye
uwezo na vigezo vinavyostahili kupata nafasi hiyo ya uwakilishi wa
wananchi katika chombo hicho cha kutunga sheria.
Mchungaji
Msigwa alikuwa akizungumza na wahariri alipotembelea ofisi za Kampuni
ya Mwananchi Communications Ltd inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The
Citizen na Mwanaspoti, Tabata Relini, Dar es Salaam jana.
Alisema wakati umefika kwa Taifa kuweka viwango maalumu vya kuwapata viongozi wa kisiasa wakiwamo wabunge na Rais.
“Tatizo
kubwa Watanzania hatuna ‘standards’ (viwango) na vigezo tunavyoviweka
kwa mtu anayetaka kuwa kiongozi, yaani tujue kuwa mtu anayekuja kuomba
uongozi anapaswa awe mtu wa aina gani.
“Tutakuwa
tunafanya makosa makubwa kama Taifa, ikiwa hatutakuwa na ‘standards’.
Vinginevyo tutapata hata wasio na sifa ndiyo hawa wanaojitengenezea
maandamano kwa kujifanya kuwa ni maarufu.”
Alisema
kigezo kinachozingatiwa katika siasa ili kuwa mbunge cha kujua kusoma na
kuandika hakitoshi na siyo sahihi, hivyo kinapaswa kitazamwe upya ili
kupata wawakilishi watakaoweza kutimiza wajibu wao ipasavyo wakiwa
watungaji wa sheria na watetezi wa rasilimali za Taifa.
“Tunaambiwa
kigezo muhimu cha kuwa kiongozi akiwamo mbunge ni kujua kusoma na
kuandika, hii siyo sahihi kwani kujua kusoma na kuandika pekee hakutoshi
kuwa kigezo cha mtu kuwa mbunge au kiongozi,” alisema.
“Kujua
kusoma na kuandika siyo kigezo cha kupitia vifungu vya sheria. Unajua
kuna baadhi ya wabunge kutokana na upeo mdogo, mtu kama Tundu Lissu
akiongea kule ndani (bungeni) hawaelewi, ndiyo maana unakuta wanaishia
kumwona kama kichaa.
“Wabunge wengi hawamuelewi Tundu
Lissu, kwa sababu vichwa vyao vina ‘GB’ moja za ubongo. Sasa ‘kucontain’
(kukusanya) mambo yote yale ya Bunge, kichwa kinapata moto na ili
kupata majibu rahisi, wanasema ni (Lissu) kichaa, maana hawawezi
kufikiri kiwango kile kutokana na akili yao kuwa ni ndogo sana,” alisema
Msigwa bila kutaja majina ya wabunge hao.
Alisema
mbunge anapaswa kuwa na uwezo wa kujieleza, kuelewa mambo, kusoma mambo
mengi, akisisitiza kuwa kwa ilivyo sasa ni kama asilimia 20 ya wabunge
wote, ndiyo wenye sifa na uwezo wa kujadili mambo.
“Wengi
wao wamekaa kaa tu, hawawezi kusema lolote, wabunge wengine
tunaposafiri nao, tunashuhudia mambo ya aibu tupu. Wengi wanakuwa kama
mabubu, wamekaa kaa tu, hawasemi chochote, hawana michango yoyote,
wanasubiri kufanya ‘shopping’ tu kana kwamba wamekwenda kwa ajili hiyo,”
alisema Msigwa.
Alisema wapo wabunge ambao tangu walipochaguliwa hawaonekani kuwa na thamani kwani hawachangii lolote bungeni.
Suti za wabunge
Alipoulizwa
jambo analojutia katika maisha ya siasa, Mchungaji Msigwa alisema kabla
ya kuwa mbunge hakufahamu haiba ya wabunge waliopo, akivutiwa na suti
zao, hadi alipopata fursa ya kuingia bungeni na kushuhudia udhaifu wa
wabunge walio wengi.
“Nilipokuwa naona wabunge wanavaa
suti kule ndani, nilikuwa navutiwa nao na kutamani niwe mbunge… baada ya
kuwa mbunge na kuingia ndani kule, nimegundua wabunge wengi hawana sifa
zinazofanana na suti wanazovaa. Hawapo makini na wanawadanganya
Watanzania na suti zao, zile suti zao ni kuficha uhalisia wao, lakini
hawana nia na dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko,” alisema.
Aliongeza:
“Wengi wao hawajui wanachokitaka, ndiyo maana unaona mbunge anasema
akitoka chama hiki, anakwenda kile, maana lengo lake ni kuendelea kuwa
mbunge tu.”
Kuhusu jambo analojivunia alisema:
“Nimefanya kazi kubwa ya ‘kuchange mind set’ (kubadilisha fikra za
watu). Hiyo ndiyo ilikuwa hoja yangu jimboni, naamini hata bungeni
nimelifanya hilo.”
Vigezo vya Chadema kushinda
Akizungumza
kwa kujiamini, mchungaji huyo aliyeingia bungeni mwaka 2010 alisema
katika Uchaguzi Mkuu ujao Chadema kina uhakika wa kushinda kutokana na
vigezo walivyonavyo huku akiviainisha.
“CCM imeendelea kushuka, kwa mfano, jimbo langu pale,
CCM imekuwa ‘unpopular’ (siyo maarufu tena). Wanashindwa hata kufanya
mikutano kwenye jimbo, lakini kibaya zaidi Serikali imeshindwa kabisa
kutimiza malengo na matumaini ambayo wananchi walikuwa nayo.
“Kwa
kipindi cha miaka mitatu iliyopita, chama chetu kimekua sana. Kwa muda
mrefu chama chetu kilikuwa kinasubiri Zitto Kabwe, Dk Willibrod Slaa au
Freeman Mbowe wafanye mikutano, lakini baada ya kuunda kanda 10, chama
chetu kimepanuka sana.
“Kimepanuka kwa sehemu kwa sana
kama vile matofali yakichomwa likianza moja mengine yanaanza kujiunguza
yenyewe. Mikutano ya Chadema haimsubiri mtu. Hiyo siyo kwa Iringa pekee,
ukienda Mufindi, Kilolo, Ludewa ndiyo hivyohivyo… ni kila mahala hata
maeneo ambayo hatuna mbunge, moto umesambaa… wananchi wameendelea
kuiamini Chadema.
“Jingine, katika uchaguzi wa mwisho
wa mwaka 2010, Rais Jakaya Kikwete ameingia madarakani baada ya kupata
asilimia 62 ya kura wakati alikuwa anatoka Ikulu. Alikuwa na ‘control’
(udhibiti) wa ‘machinery’ (mifumo) yote. Sasa anakuja mwingine kukutana
na adui yuleyule ambaye ameimarika zaidi na pale Ikulu inakwenda kuwa
Ikulu ambayo haina mwenyewe,” alisema. “Tunakwenda kwenye majimbo ambayo
kila mtu anakwenda kufa peke yake. Hautakuwa kama uchaguzi wa Kalenga
ambao walikuja wote kushambulia, sasa hivi kila mtu anakwenda kupambana
mwenyewe. Ndiyo maana tunasema, tuna kila sababu ya kusema uchaguzi huu
kama utakuwa wa huru na haki hawa jamaa hawachomoki.”
Akitaja
kigezo kingine cha ushindi wa Chadema Mchungaji Msigwa alisema: “Kwa
msuguano uliopo ndani ya CCM… haitatoka salama. Kama wakati ule makundi
ya Kikwete yalidumu kwa miaka 10 hata sasa, makundi ndani ya chama hicho
hayatakosekana. Kwa hiyo kugawanyika kwao ni faida kwetu.”
Ukomo wa ubunge
Akizungumzia
majaliwa yake kisiasa, Mchungaji Msigwa aliyesema ana uhakika wa
kushinda ubunge kwa kipindi cha pili, endapo chama hicho hakitashinda
urais Oktoba mwaka huu, kitakuwa kipindi chake cha mwisho kwa ubunge.
“Labda tukishinda nchi (urais) nitagombea tena,” alisema Mchungaji Msigwa.
Alipoulizwa
iwapo kauli yake kuwa ataendelea kuwania ubunge iwapo watatwaa urais
inaonyesha wasiwasi wake wa kutoshinda nafasi hiyo, Msigwa alisema:
“Siwezi
kusema nina wasiwasi, lakini katika chaguzi za kiafrika ‘anything can
happen’ yaani unaweza ukashinda ukanyang’anywa, hata katika uchaguzi
uliopita nilikuwa katika hatari ya kunyang’anywa.
“Nilishinda
tangu saa mbili usiku, lakini matokeo yakatangazwa siku ya pili saa 10
jioni na hapo niliambiwa na vijana wa Usalama wa Taifa, unajua kuna
Usalama wa Taifa ni wazuri. Waliniambia umeshinda lakini wanataka
kukunyang’anya ushindi. Sikulala siku hiyo vijana waliniletea ‘Red Bull’
10,” alisema Msigwa.
Manispaa ya Iringa
Alisema katika uchaguzi ujao, mbali na ilani ya chama, atafanya kampeni ya kuchukua Manispaa ya Iringa Mjini.
“Nataka
tuongeze pato la Iringa Mjini. Wakati ninaingia, manispaa ilikuwa
inaingiza Sh900 milioni na sasa tunaingiza Sh3.2 bilioni, tunataka
mapato yaongezeke na kufikia Sh7 bilioni ili Iringa mjini tuweze
kujijengea miundombinu. Tujue ‘pedestrian’ (waenda kwa miguu)
wanatembeaje hata waendesha baiskeli, badala ya kutegemea Serikali Kuu,”
alisema.
Alipoulizwa kuhusu hatima ya Ukawa katika
uchaguzi na anavyompima mpinzani wake kisiasa kutoka CCM, David
Mwakalebela, ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe kama ni
tishio kwake, alisema:
“Nianze na jimbo. Kwa
Mwakalebela siyo ‘threat’ (tishio) kwangu hata kidogo. Sasa hivi CCM
wanagombana kuhusu ubunge. Wakati ule walisema nilishinda kwa sababu eti
Mwakalebela hakugombea.
Sasa Kikwete (Rais) angefanya
vizuri sana asingempeleka Wanging’ombe, angemleta Mwakalebela pale
Iringa Mjini kuwa mkuu wa wilaya, tuwe wote pale yeye anakuwa na cheo
cha DC, mimi mbunge. Angefanya vizuri sana kampeni zake za ubunge.
Nasema hivi kwa sababu ‘he is not a threat at all’ (yeye siyo tishio
kwangu kabisa).”
Aliongeza: “…Kinana alivyokuwa Iringa
Mjini aliwaambia watu wa Iringa mjini huyu Msigwa alishindaje?
Mmemchaguaje wakati ninyi ni watu wa CCM, mmefanya makosa…
Walimdanganya, lakini majibu ya hoja aliyoijenga mwenyewe wameyapata
katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopita. Mimi nilishinda ubunge
nikiwa na mwenyekiti mmoja wa Serikali za Mtaa, sasa nina wenyeviti wa
mitaa 67 kati ya 130.
“Hiyo ni ishara tosha kuwa
wananiamini. Hiyo ni ishara tosha ya kwamba nakubalika. Hayo yametokea
baada ya Kinana kusema mimi nina mwenyekiti mmoja. Nimewapa maneno
ambayo hayatoki kichwani. Hata vijiweni wanani-quote (wananinukuu).
Utawasikia, hata Mchungaji Msigwa alisema... niliwaambia mimi sitawapa
samaki, nitawafundisha kuvua samaki na ndiyo maana niliwaambia mimi siyo
ATM, miezi sita ya mwanzo nilikuwa ‘unpopular. Kiongozi ni yule
anayefanya mambo sahihi, siyo mambo mazuri.”
Imeandikwa na Joyce Mmasi, Suzan Mwillo na Exuperius Kachenje