Bagonza: Maaskofu hatujagawanyika kuhusu Katiba
Dar es Salaam. Mjadala kuhusu tamko la Jukwaa la Wakristo
Tanzania umezidi kupamba moto baada ya Askofu Benson Bagonza wa Kanisa
la Kiinjili la Kilutheri Tanzani (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, kupinga
kuwapo kwa mgawanyiko miongoni mwao kama unavyosemwa na Serikali.
Kauli
ya Askofu Bagonza imekuja siku moja baada ya Serikali kupitia Waziri wa
Uchukuzi anayekaimu nafasi ya Kiongozi wa Serikali bungeni, Samuel
Sitta kueleza kuwa maaskofu wamegawanyika na mgawanyiko huo hauwezi
kubadili msimamo wa Serikali.
Sitta, ambaye pia alikuwa
mwenyekiti wa Bunge Maalumu, alisema maaskofu hao wawaache wananchi
waamue wenyewe aina ya kura wanayotaka kuipigia Katiba Inayopendekezwa.
Akizungumza
na gazeti hili jana, Askofu Bagonza alisema hakuna mgawanyiko na
Serikali imeandaa maaskofu wake mfukoni ambao huwatumia kujibu hoja
mbalimbali za maaskofu.
Alitoa mfano wa askofu mmoja ambaye alisema hafahamiki kwa Kanisa la Pentekoste, Walutheri wala Wakatoliki.
Kauli ya Pengo
Akizungumzia
kauli aliyotoa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam,
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo inayopingana na maoni ya Jukwaa la
Wakristo Tanzania, Askofu Bagonza alisema hayo ni maoni yake binafsi na
haiwezi kuwa sauti ya Wakatoliki wa Tanzania.
Askofu
Bagonza alisema sauti ya Wakatoliki hutolewa na Baraza la Maaskofu
Tanzania (TEC) ambalo ndilo mwanachama wa Jukwaa la Wakristo Tanzania.
“Mwadhama yeye ni mjumbe wa TEC, alitoa tu maoni yake na
aliagiza tamko letu la jukwaa lisomwe kwenye makanisa ya jimbo lake la
Dar es Salaam,” alisema Askofu Bagonza na kufafanua kuwa tamko
lililotolewa na jukwaa ndiyo kauli rasmi ya Wakristo.
Askofu
huyo alisema kabla ya msimamo wa jukwaa hilo kutolewa, siku tatu kabla
TEC ambayo Kardinali Pengo ni mjumbe, lilitoa tamko lenye ujumbe
unaofanana na wa jukwaa, ukiitaka Serikali kuahirisha kura ya maoni la
sivyo waumini wahamasishwe kuipigia kura ya hapana Katiba
Inayopendekezwa.
Msimamo wa makundi
Askofu
Bagonza alisema suala la Katiba ni la Watanzania wote, hivyo makundi
katika jamii yana haki ya kutoa maoni yake yanayoweza kutofautiana na ya
wengine.
“Kama CCM na Serikali yake wanashawishi watu
wapige kura ya Ndiyo, Ukawa wamewaeleza watu wao wasusie, iweje iwe
tatizo kwa Jukwaa la Wakristo kuwaeleza wafuasi wao wapige kura ya
Hapana?” alihoji.
Hata hivyo, Askofu Bagonza alisema
jukwaa katika mjadala wake halikujikita katika mambo yaliyomo katika
Katiba Inayopendekezwa, bali yale yaliyoachwa na jinsi mchakato
ulivyokwenda.
Mahakama ya Kadhi
Kuhusu
Mahakama ya Kadhi, Askofu huyo alisema jukwaa hilo halina tatizo na
uzuri au ubaya wa mahakama hiyo, bali Serikali kujihusisha na suala hilo
na kuifanya kama ahadi ya kuwavutia Waislamu kuipitisha Katiba
Inayopendekezwa katika Bunge la Katiba.