Lowassa: Nimeshawishika kuwania urais
>Mbunge
wa Monduli ,Edward Lowassa akiagana na Masheikh wa wailayani Bagamoyo
mkoani Pwani baada ya kumkabidhi mchango wa kuchukua fomu ya kuwania
urais nyumbani kwake,Dodoma jana.
Hatimaye mbunge wa Monduli, Edward Lowassa amesema
“ameshawishika” na kuweka bayana kuwa atachukua fomu ya kugombea urais
kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Lowassa,
ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne, amekuwa akitajwa
kuwa ni mmoja wa makada wa CCM wanaowania urais, lakini hakuwahi
kutangaza nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini.
Lakini
jana, alilazimika kufunguka kuhusu suala la urais ambalo lilimfanya
yeye na wenzake watano wafungiwe kwa kipindi cha miezi 12 kujihusisha na
harakati hizo baada ya Kamati Kuu ya CCM kuwatia hatiani kuwa walianza
kampeni mapema kabla ya muda kufika.
“Nimepata barua za
ushawishi kutoka kwa watu wengi, lakini nyinyi nimeshawishika,” alisema
Lowassa nyumbani kwake mjini Dodoma wakati alipokuwa anazungumza na
masheikh wa misikiti ya Wilaya ya Bagamoyo wanaokadiriwa kuwa kama 50
hivi ambao pia walikuja mjini hapa kwa ajili ya kumshawishi aingie
kwenye kinyang’anyiro cha urais na kumkabidhi mchango wa Sh700,000 za
kuchukulia fomu.
“Lakini bado kuna taratibu za chama za kuheshimu. Nangojea pale watakaposema sasa tuwe, basi itakuwa.”
Lowassa
alifungiwa na CCM Februari 18, 2014 pamoja na Bernard Membe, ambaye ni
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Steven Wasira
(Kilimo, Chakula na Ushirika), na January Makamba (Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia).
Wengine
waliofungiwa ni Frederick Sumaye, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali
ya Awamu ya Tatu na William Ngeleja (Mbunge wa Sengerema).
Pamoja
na adhabu hiyo kumalizika Februari 18, CCM imesema Kamati ya Maadili
inaendelea na uchunguzi kwa ajili ya kujiridhisha kama miongoni mwao
kuna waliokiuka adhabu hiyo kabla ya kuwasilisha mapendekezo kwenye
Kamati Kuu ambayo itafanya uamuzi.
Masheikh waliofika
jana nyumbani kwake wanatoka maeneo ya Mlingotini, Kondo, Kaole, mjini
Bagamoyo, Lugoba na Chalinze wilayani Bagamoyo.
Mbali na kumuomba atangaze nia, masheikh hao pia walimsomea dua ya kumtakia heri katika harakati hizo.
“Nyie
ni special (maalum), mnatoka Bagamoyo na inajulikana kwa historia na ni
nyumbani kwa Rais (Jakaya Kikwete). Namimi nimepata baraka zake na nyie
mmemuwakilisha,” alisema Lowassa.
“Tumetoka naye mbali
sana, lakini Mwenyezi Mungu akinijalia nitaanzia pale alikomalizia.
Amefanya kazi kubwa na ya heshima kwa kweli. Kwa hiyo kitendo cha kutoka
nyumbani kwenu kuja kuniona kwa kweli kimenipa nguvu kwamba wenzangu wa
Bagamoyo wako pamoja na mimi.”
Alisema anaheshimu sana maneno waliyomwambia masheikh hao na anayakubali.
“Kwamba
siku ikifika muda kwa mujibu wa taratibu za chama, nitachukua hiyo
fomu. Lakini haitoshi tu kunishawishi, naomba mniombee dua… kuliko yote
hili ni jambo la msingi sana. Kura zitapatikana kwa dua zenu,” alisema.
Lowassa pia alimsifia Rais Kikwete kwa kufanya mambo makubwa nchini na kwamba kati ya maeneo aliyoshughulika nayo sana ni elimu.
“Lakini
elimu ni mtandao mkubwa, kuna matatizo mengi kunahitaji bado
kushughulikiwa. Nikifanikiwa, inshallah nitaanza na suala la elimu kwa
kufanya elimu iwe kipaumbele chetu katika Taifa letu,” alisema Lowassa
ambaye alikuwa mstari wa mbele kuanzisha shule za kata na ndiye
aliyeongoza ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma.
“Nikianza
na elimu nitashughulikia mambo mengine mengi; kilimo kwanza, afya, ajira
kwa vijana msingi wa hayo ukiwa ni elimu bora unaweza kuyashughulikia
vizuri sana.”
Alisema pia akifanikiwa ataangalia jinsi
ya kushirikisha dini katika muundo wa Serikali ili mambo ya Serikali na
ya dini yaende vizuri bila mijadala nje ambayo inatishia amani na
utulivu.
“Kuna nchi nyingine, mahali kama Pakistan
mambo ya dini yana wizara yake ndani ya serikali. Kwa sababu mambo haya
ni magumu sana, ukiyaendea vibaya yanaleta tabu katika nchi, yanaleta
mauaji, vifo na vitu vingine,” alisema Lowasa.
Alisisitiza kuwa hata kama alikuwa na mawazo nusu nusu ujio wao umemuimarisha sana.
“Niseme
kwamba ujumbe umefika, mkikutana naye msikitini pelekeni salamu kwa
mheshimiwa Rais (Kikwete), mwambieni mlikuja Dodoma. Mie nimesema
nitaendeleza pale alipomalizia kama Mwenyezi Mungu atanijalia,” alisema.
Mmoja wa viongozi wa msafara huo, Sheikh, Hassan Kilemba
alimsifu Lowassa kuwa alipokuwa Waziri Mkuu alilibeba tatizo la
wanafunzi kukosa elimu ya sekondari kwa uchungu na kutekeleza kwa
vitendo.
“Kama ungeendelea kubaki madarakani, shule zote za sekondari zingekuwa na mfano wa ajabu,” alisema.
Alisema pia matatizo ya maji katika Kanda ya Magharibi yaliweza kupungua na kuisha kwa jitihada zake na wananchi.
“Mheshimiwa
Lowasa ulikubali kuachia ngazi lakini bado ukawa mtiifu kwa chama chako
na bado ukawa mwadilifu kwa kuwapenda wananchi,” alisema.
Alisema
mkoani Mwanza, Waislamu walitaka kuanzisha redio yao lakini bila kujali
tofauti ya dini alikwenda kwenye harambee ya kuchangia redio hiyo.
Pia
alisema msikiti wa Mtambani walipopata tatizo la moto, alikwenda
kuwafariji, jambo ambalo ni kubwa sana kwa waumini wa dini ya Kiislamu.
“Sisi
pasipo kushawishiwa na mtu yeyote tumeamua kuja kukushawishi uwanie
urais. Tafadhali tafadhali wala usipate kigugumizi chukua fomu. Bagamoyo
hauko pekee yao. Sisi masheikh wa Bagamoyo tumeamua kujichangisha ili
fedha zikusaidie katika harakati zako,“ alisema.
Naye Sheikh Yusuph Suruhu alisema Lowasa alikuwa kiongozi wa vitendo na hakuwa mtu wa kulalamika.
Lowassa
alijiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu mwaka 2008 baada ya kutajwa kwenye
kashfa ya mkataba wa kampuni ya uzalishaji umeme ya Richmond Development
Company ya Houston Marekani, ambayo ilionekana haikuwa na uwezo wa
kutekeleza utashi wa mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura wakati nchi
ikiwa kwenye tatizo kubwa la nishati hiyo. Kamati ya Bunge iliyoundwa
kuchunguza kashfa hiyo ilimtaka Lowassa apime ushiriki wake katika
kuingia mkataba huo na afanye uamuzi.
Katika hotuba
yake ya kutangaza kuachia ngazi, Lowassa alisema ameamua kujiuzulu ili
kulinda heshima ya Serikali katika kashfa hiyo kubwa iliyotikisa nchi na
kusababisha mawaziri wengine wawili kuwajibika pia.
Kikundi
hicho cha masheikh wa wilayani Bagamoyo ni hitimisho la mlolongo wa
vikundi ambavyo vimekuwa vikipishana mjini Dodoma na jimboni kwake
Monduli mkoani Arusha kumshawishi achukue fomu ya kuwania urais, lakini
amekuwa akieleza kuwa muda ukifika atafanya uamuzi huo.
Waziri
huyo wa zamani wa Maji na Maendeleo ya Mifugo alipata shahada yake ya
sanaa kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na shahada ya umahiri wa
masomo ya maendeleo kwenye Chuo Kikuu cha Bath nchini Uingereza.
Lowassa
alikuwa waziri wa Nchi, Ofisi ya waziri Mkuu wakati wa kipindi cha pili
cha Serikali ya Awamu ya Pili. Wakati Rais Ali Hassan Mwinyi
alipomaliza muda wake, Lowassa alijitokeza kuwania urais kwa tiketi ya
CCM mwaka 1995, lakini alishindwa katika hatua za mwanzo na Benjamin
Mkapa alishinda na kuongoza kwa vipindi viwili.
Alirejea
bungeni na hakuteuliwa kuwa waziri hadi mwaka 1997 alipoteuliwa kuwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Kupambana na
Umaskini).
Baada ya uchaguzi wa mwaka 2000, aliteuliwa
kuwa Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo, wizara ambayo
alijitengenezea jina kama mchapakazi.
Uchaguzi
uliofuata, Lowassa hakujitosa kwenye mbio za urais, na badala yake akawa
kitovu cha kampeni cha mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete ambaye
alikuwa rafiki yake wa muda mrefu na haikuwa ajabu kwa Kikwete kumteua
kuwa waziri wake mkuu wa kwanza baada ya kushinda uchaguzi.
Lowassa
ameingia kwenye historia kama Waziri Mkuu wa kwanza kujiuzulu wadhifa
wake kutokana na kashfa dhidi ya Serikali iliyosababisha rais avunje
Baraza la Mawaziri.
Lowassa ni nani?
Jina
lake kamili ni Edward Ngoyai Lowassa. Alizaliwa Agosti 26 mwaka 1953 na
kusoma katika Shule ya Msingi Monduli kati ya mwaka 1961 na 1967. Mwaka
1968 hadi mwaka 1971, alisoma katika Shule ya Sekondari Arusha, kabla
ya kujiunga na Elimu ya Juu ya Sekondari katika Shule ya Milambo Tabora
kati ya mwaka 1972 na 1973.
Baada ya kuhitimu, Milambo,
alijiunga na Masomo ya Shahada ya Ualimu katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam kati ya mwaka 1974 na 1977, kabla hajaingia katika Chuo kikuu cha
Bath kilichoko nchini Uingereza kwa ajili ya Masomo ya Shahada ya Pili
ya Sayansi mwaka 1983 hadi 1984, na baadaye kuendelea chuoni hapo kwa
Shahada nyingine ya Pili ya Elimu ya Maendeleo.
Baada
ya kuhitimu kozi hiyo, Lowassa alirudi nchini na kuanza ajira yake ya
kwanza katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha jijini Arusha (AICC)
akiwa Mkurugenzi Mtendaji na baadaye kuwa Waziri wa Katiba na Mambo ya
Bunge kati ya mwaka 1990 na 1993. Mwaka 1993 hadi 1995 Lowassa alikuwa
Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi na kati ya mwaka 1997 na 2000,
alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mazingira na Umaskini) kabla
hajateuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Waziri Mkuu mwaka 2005 hadi
2008. Amekuwa Mbunge wa Monduli kwa kipindi cha miaka 20 sasa.