Marsh aagwa Dar kuzikwa Mwanza
Dar es Salaam. Aliyekuwa kocha msaidizi wa Taifa Stars, Silvester Marsh ameelezwa kujitabiria kifo chake saa chache kabla ya kutokea juzi asubuhi kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Akizungumza katika ibada ya mazishi
iliyofanyika jana, Katekista wa Kanisa Katoliki Muhimbili, Rogatus Fussi
alisema Ijumaa asubuhi alipokea barua ya Marsh akiomba kufanyiwa sala
ya toba.
“Barua hiyo ilikuwa na majina matatu likiwamo
la Marsh ambaye aliomba padri akamuombee sala ya toba, kwa kuwa Padri
hakuwepo, saa tisa alasiri nilikwenda mimi.
“Nilimkuta
Marsh akiwa katika hali mbaya, nilifanya nae sala hadi saa 11 jioni na
kupitia yeye pia kuna baadhi ya watu kwenye wodi aliyolazwa walipata
huduma hiyo.
“Asubuhi jana (juzi Jumamosi) nilikwenda
kumtembelea kama nilivyoahidi na nesi kuniambia tayari Marsh amefariki,
hii ni ishara tosha kuwa mpendwa wetu alijiandaa kabla ya kifo chake
hivyo na sisi tuliobaki tunatakiwa kujiandaa,” alisema katekista huyo.
Mwili
wa Marsh uliwasili kanisani majira ya saa 5:30 asubuhi tayari kwa ibada
ya mazishi ambayo ilianza saa 6:30 kanisani hapo na kuhudhuriwa na
wadau mbalimbali wa soka akiwamo Kocha wa Yanga, Charles Mkwassa, Kocha
wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage, mwakilishi kutoka Idara ya Maendeleo
ya Michezo, Juliana Yasoda, wanafamilia na wadau wengine.
Katika
hali ya kushangaza, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilikosa
mwakilishi wa kutoa salamu za rambirambi katika ibaada hiyo baada ya
katekista kumtaka mwakilishi wa familia na yule wa TFF kutoa salamu hizo
na kwa upande wa familia, kaka wa Marehemu, Zablon Marsh alisema
taratibu za mazishi zitajulikana baada ya mwili wa marehemu kuwasili
jijini Mwanza huku upande wa TFF wakikosa mtu na katekista kuamua
kuendelea na taratibu za kuuga.
Hata hivyo, gari la TFF
(Hiace) ambalo lilitarajiwa kuusafirisha mwili wa Marsh halikuwepo eneo
la Hospitali, hivyo kulazimika mwili wa Marsh kusubiri kwa saa kadhaa
baada ya kuagwa kwa kile ambacho kilielezwa dereva alikuwa njia kutoka
Morogoro.