JK, Nkurunziza wazindua treni za mizigo kwenda Burundi, Uganda na DR Congo


> Rais wa Burundi, Pierre Nkurunzinza akipeperusha bendera kuzindua safari za kusafirisha mizigo zijulikanazo kama Block Trains katika shesheni ya Dar es Salaam jana. Kulia ni Rais Jakaya Kikwete Picha na Venance Nestory
Rais Jakaya Kikwete na mwenzake Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi wamezindua safari za treni tatu za mizigo ‘block train’ kutoka Dar es Salaam kwenda Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Uzinduzi wa treni hizo zenye mabehewa 15 hadi 20 ulifanyika jana jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya Rais Kikwete kuzindua mkutano wa marais wanachama wa nchi zinazounda ukanda wa kati.
Marais waliohudhuria mkutano huo wa siku mbili ni Rais Yoweri Museven wa Uganda, Rais wa Kenya aliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Amina Mohamed, Rais wa DRC aliwakilishwa na Waziri wa Usafirishaji, Justine Kanumba huku Rais wa Rwanda, akiwakilishwa na Waziri wa Miundombinu wa nchi hiyo, James Musoni.
Akizindua treni hizo, Rais Kikwete alisema, “kuanzia sasa zitakuwa zikibeba mizigo ya nchi moja pekee yake kwa wakati mmoja, kama ni mizigo ya Burundi itakuwa Burundi tu vivyo hivyo kwa DRC na Uganda, kinyume na ilivyokuwa awali.
“Awali safari za treni za mizigo zilikuwa zikichukua wiki mbili kufikisha mizigo kwenye nchi husika, lakini sasa itakuwa inachukua siku mbili pekee,” alisema Rais Kikwete.
Kwa upande wake Rais Nkurunziza alisema Tanzania imefanya jambo la maana kuisaidia nchi yake ambayo ipo mbali na bahari. “Safari hizo zitasaidia kusafirisha mizigo mingi na kwa njia ya kwa haraka.”
Vikwazo vya usafirishaji
Awali akifungua mkutano wa Ukanda wa Kati wa Kibiashara jijini hapa, Rais Kikwete alisema Tanzania imeshapiga hatua kubwa katika kuhakikisha inaondoa vikwazo vyote vya usafirishaji mizigo kwenda nchi jirani, ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya vizuizi barabarani.
“Tumeamua kupunguza vizuizi vya polisi barabarani kutoka 15 hadi vitatu na vituo vya mizani kutoka 10 hadi vitatu vitakavyojengwa vigwaza mkoani Pwani, Manyoni (Singida) na Nyakahura (Kagera),” alisema Rais Kikwete.
Alisema ni jukumu la nchi kuonyesha kuwajibika katika mradi huo kwa kuwa sehemu kubwa ya mradi ipo nchini, hivyo ni vyema kuhakikisha nchi jirani zinasafirisha mizigo yao kutoka bandari ya Dar es Salaam bila tatizo.
“Kama ambavyo nimesema inatuwezesha kukuza biashara za ndani na kimataifa na kukuza uchumi.”
Katika mradi huo, kilomita 2,707 za reli hiyo zipo Tanzania, barabara ni kilomita 2,406, pia bandari kubwa tatu za Dar es Salaam, Kigoma na Mwanza zipo Tanzania.
Kuhusu ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam, Rais Kikwete alisema kuwa idadi ya mizigo inayosafirishwa imeongeka kutoka tani milioni 9.2 mwaka 2010 hadi tani milioni 14 mwaka 2014 na kufikia mwishoni mwa mwaka huu inatarajiwa kufikisha tani milioni 18.
“Idadi ya siku za kutoa mzigo bandarini zimepungua kutoka siku 21 hadi 9 na bado tunataka zipungue zaidi. Kuhusu wizi hakuna taarifa ya tukio lolote kwa miaka miwili sasa…pia Serikali ina mpango wa kujenga bandari mpya Bagamoyo itakayoweza kuhifadhi tani milioni 240 kwa mwaka,” alisema Rais Kikwete.
Kuhusu reli, alisema kuwa vichwa 13 vya treni vimeshanunuliwa na kati yake viwili viliwasili nchini wiki iliyopita. Vichwa vitano vinatarajiwa kuwasili mwezi ujao na vilivyobaki vitaletwa Mei mwaka huu. Pia mabehewa 274 yamenunuliwa kati yake 150 yaliwasili nchini Februari mwaka huu.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema pamoja na Tanzania kuingiza nchini mkongo wa mawasiliano ya intaneti, bado haijanufaika kiasi cha kutosha kwa kuwa baadhi ya wananchi wanautumia kwa ajili ya kutuma ujumbe na picha kwa njia ya mtandao wa kijami wa WhatsApp.
Rais Museveni aliyekuwa kivutio kwa watu wengi mkutanoni kutokana na muda mwingi kutoa matamshi ya utani, alisema sababu mbalimbali zinazokwamisha biashara kufanikiwa kuwa ni pamoja na ukosefu wa usalama, kutokuwapo kwa watendaji wenye ujuzi, kukosekana kwa soko na kukosekana kwa faida kuwa ndiyo sababu zinazoweza kukwamisha biashara kustawi.
Alisema ili mipango ya kibiashara inayopangwa na nchi hizo ifanikiwe lazima vikwazo vijulikane na kutafutiwa ufumbuzi mapema.
“Wataalamu wa uchumi wanasema gharama ya usafiri katika biashara inapaswa kuwa asilimia 40, mtaji asilimia 20, kazi asilimia 10, ukilitimba asilimia tano, lazima tujiulize kikwazo kipi kinatukwaza,” alisema Museven.
Alisema hakuna namna ujenzi wa reli unaweza kuepukika kwa kuwa barabara zinapitika mara kwa mara huku zikigharimu fedha nyingi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed alisema miradi iliyoanzishwa chini ya mradi huo itachangia sehemu kubwa kuimarisha hali ya kiuchumi iliyokuwa imekwama katika baadhi ya miradi.
Powered by Blogger.