Kinana: Ujenzi barabara ‘ya Ngorongoro’ umeiva
Ngorongoro. Katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amesema
mpango wa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Monduli kupitia Hifadhi ya
Taifa ya Ngorongoro hadi Mugumu umekamilika baada ya Rais Jakaya Kikwete
kumaliza mazungumzo na nchi zilizokuwa zimegoma.
Kinana
alito kauli hiyo jana alipozungumza katika mkutano wa hadhara
uliofanyika Wasso wilayani Ngorongoro, akisema kuwa mkutano wa Rais
Kikwete na wadau uliwezesha kukubalika kwa ushawishi wake na kuondolewa
na vitisho vilivyokuwa vimewekwa.
Kauli ya Kinana
imekuja wakati kuna kesi imefunguliwa Mahakama ya Afrika Mashariki
(EACJ) na asasi isiyo ya kiserikali ya Africa Network For Animal Welfare
(ANAW) ya Nairobi, Kenya ikipinga ujenzi wa barabara hiyo.
Katika
hukumu ya jopo la majaji wa EACJ walioongozwa na Jaji Kiongozi Jean
Bosco Butasi, Juni 20, 2014 Tanzania ilitakiwa kusitisha mradi wowote wa
ujenzi kutokana na athari ambazo zinaweza kujitokeza kutokana na
utekelezaji wake.
Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ya Tanzania amekata rufaa kupinga hukumu hiyo na shauri hilo
bado liko kwenye mchakato wa usikilizaji.
Kinana
alisema katika mazungumzo hayo, Rais alieleza adhima yake katika ujenzi
huo kuwa si kujenga barabara ya lami kwenye eneo lote, bali kilomita 50
tu ambazo ni sehemu ya mapito ya wanyama hao zitaachwa.
“Kwa
sasa upo umuhimu mkubwa wa barabara hiyo ya kiwango cha lami kwa kuwa
idadi ya watu wanaotumia barabara hiyo imeongezeka tofauti na ilivyokuwa
miaka ya nyuma,” alisema Kinana.
Alisema haiwezekani
msimamo huo ukaendelea kushikiliwa kwa kuwa itakuwa ni sawa na
kumthamini mnyama kuliko binadamu, jambo ambalo si sahihi.