Staili ya Chegeni yatumika tena kumshawishi Edward Lowassa
Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa akiwakaribisha wananchi kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Manyara waliofika nyumbani kwake wilayani Monduli jana kumwomba atangaze nia na kugombea urais mwaka 2015. Picha na Daniel Mjema.
Monduli. Staili aliyotumia Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya
Taifa ya CCM, Dk Raphael Chegeni kumshawishi Waziri Mkuu mstaafu, Edward
Lowassa agombee urais imetumika tena jana baada ya makundi mbalimbali
ya jamii kwenda nyumbani kwake Monduli na kumtaka achukue uamuzi huo
haraka.
Wakiwa nyumbani kwa Lowassa, wananchi hao
kutoka Kanda ya Kaskazini walimkabidhi Sh2,567,600 walizosema
zimechangwa na marafiki wa Lowassa kwa ajili ya kuchukulia fomu.
Miongoni
mwa watu hao walikuwamo vijana, wazee, wanawake, viongozi wa dini na
watu wenye ulemavu wanatoka mikoa ya kanda ya kaskazini ya Kilimanjaro,
Arusha,Tanga na Manyara pamoja na wajumbe watatu wa Mkutano Mkuu wa
Taifa wa CCM na wenyeviti wawili wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Wananchi
hao walifika nyumbani kwa Lowassa wakitembea kwa miguu kutoka umbali wa
kilometa moja huku wakiimba wimbo wa “Tuna imani na Lowassa”.
Akisoma
risala kwa niaba ya wananchi hao, Protas Soka alisema kwa sasa
Watanzania wanamhitaji Lowassa aweze kuwaongoza kama Rais wa awamu ya
tano.
“Tunakuomba usimame mbele ya Watanzania na utoe japo neno roho zao zitulie,” alisema Soka ambaye ni mlemavu wa ngozi.
“Kwa
lugha nyingine mheshimiwa Lowassa sasa tunakuomba utangaze nia ya
kuingia kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Tanzania 2015. Wewe ni
tumaini la walio wengi Tanzania,” alisema.
Kwa upande
wake, mratibu wa marafiki wa Lowassa Kanda ya Kaskazini, Noel Nko
alisema Sh2.5 milioni walizomkabidhi, zimechangwa na wananchi wa kawaida
kabisa kutoka moyoni mwao.
Akizungumza na wananchi
hao, Lowassa alisema yuko tayari kutangaza nia wakati wowote lakini
anasubiri tamko kutoka CCM na huenda akatangaza nia hiyo mwanzoni mwa
Aprili.
Lowassa alisema iwapo CCM itatoa tamko hilo,
atatangaza nia hiyo katika uwanja wa mpira wa Sheikh Amri Abeid Jijini
Arusha, akisema anaamini kundi hilo pia litamuunga mkono siku hiyo.
“Nimebubujikwa
na machozi ya furaha kwa ujio wenu huu. Ninawashukuru kwa tendo hili.
Tukishafanikiwa katika safari yetu ya matumaini tukutane tena hapa
hapa,” alisema.