Lipumba akubali tamko la maaskofu
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba
ameunga mkono tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania kupinga Katiba
Inayopendekezwa, akisema hoja zao ni za msingi kwa kuwa kuna mambo mengi
yanayopingwa na wananchi.
Kauli ya Profesa Lipumba ni
mwendelezo wa kauli tofauti zilizotolewa na watu mbalimbali kuhusu tamko
la jukwaa hilo, wakiwamo wasomi, viongozi wa dini, wanaharakati na
wanasiasa kuhusu hatima ya Kura ya Maoni na muswada wa Makahama ya
Kadhi.
Alhamisi iliyopita, jukwaa hilo linaloundwa na
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
(TEC) na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) liliwataka
waumini wake kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, kushiriki kikamilifu
katika elimu ya Kura ya Maoni, na kisha kuipigia kura ya “hapana” Katiba
Inayopendekezwa.
Pia, tamko hilo lililotiwa saini na
maaskofu Dk Alex Malasusa wa (CCT), Tracisius Ngalalekumtwa (TEC) na
Daniel Awet wa CPCT, lilishauri mjadala unaoendelea kati ya Serikali na
vikundi vya kidini kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kikatiba na
kisheria ufungwe na badala yake ziachiwe taasisi husika za kidini kuamua
juu ya masuala hayo bila kuihusisha serikali wala waumini wa dini
nyingine.
Jana gazeti hili lilimnukuu makamu mwenyekiti
wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi akisema tayari tamko hilo
limeshasambazwa katika majimbo yote ya kanisa katoliki nchini.
Kauli ya Lipumba
Akizungumzia
tamko hilo, Profesa Lipumba alisema ni sahihi kuipinga Katiba hiyo kwa
sababu wananchi walilalamikia mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya
baada ya kubaini kuwa mambo mengi waliyoyapendekeza yaliondolewa wakati
wa Bunge Maalumu la Katiba.
“Wananchi walitaka kuwepo
na ukomo wa wabunge wao, viongozi wasifungue akaunti nje ya nchi na
mambo mengine yote hayamo kwenye Katiba Inayopendekezwa. Hoja yao
(maaskofu) ni ya msingi,” alisema Profesa Lipumba aliyeongoza wajumbe wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka nje ya Bunge la Katiba na
kususia mchakato huo moja kwa moja.
Alisema Serikali
imeonyesha kutokuwa na uaminifu kwa wananchi ndio maana haikujali hisia
zao, badala yake iliamua kuendelea na mchakato huo licha ya baadhi ya
wajumbe kuususia.
Profesa Lipumba, ambaye ni mtaalamu
wa uchumi, aliongeza kuwa wananchi walitaka kuwepo na utaratibu maalumu
kuhusu viongozi wao kupewa zawadi wawapo madarakani, lakini Katiba
Inayopendekezwa ililitupa nje suala hilo.
Mahakama ya Kadhi
Kuhusu
suala la Mahakama ya Kadhi, Profesa Lipumba alisema pia Serikali
isitishe uamuzi wake wa kupeleka Muswada ya Mahakama ya Kadhi katika
Bunge lijalo kwa kuwa bado yapo mambo mengi yanayotakiwa kuwekwa sawa.
Profesa
Lipumba alisema pamoja na mahakama hiyo kutokuwa ngeni hapa nchini kwa
kuwa ilikuwapo Tanzania Bara wakati wa ukoloni na Zanzibar, bado
inaendelea kufanya kazi bila tatizo, mfumo unaotaka kutumiwa na Serikali
kuianzisha hivi sasa unapingwa na baadhi ya Waislamu na Wakristo hivyo
kusababisha mgawanyiko.
Alisema hali hiyo imefikia hapo
kutokana na CCM kuliingiza suala hilo kwenye ilani yake ya uchaguzi ya
mwaka 2005, hivyo njia bora ya kuondoa sintofahamu iliyopo ni kwa
kutumia muda mrefu zaidi katika kutafuta muafaka.
“Ni bora tungetumia muda mrefu zaidi kutafuta muafaka, Serikali isiendelee na muswada huo,” alisema Profesa Lipumba.
Wiki
iliyopita, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema Muswada wa Marekebisho ya
Sheria mbalimbali, likiwamo suala la Mahakama ya Kadhi, utawasilishwa
katika bunge lijalo ukiwa na maudhui ya kuangalia namna ya kuendesha
masuala ya imani ya dini ya Kiislamu.
Nyambabe aunga mkono
Katibu
mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema anaunga mkono uamuzi
uliofikiwa na maaskofu hao kwa kuwa haiwezekani nchi ikapiga Kura ya
Maoni ya Katiba Inayopendekezwa wakati wananchi wamegawanyika.
“Msimamo wa maaskofu ni kama wa Ukawa. Bila kuchukua hatua mmomonyoko wa maadili hautaisha,” alisema Nyambabe.
Kuhusu
Mahakama ya Kadhi, Nyambabe alisema: “Hakuna mtu anayepinga kuwepo kwa
mahakama hiyo, lakini isiwe chini ya serikali moja kwa moja, iwe huru.”
Kauli za wachungaji
Baadhi
ya wachungaji waliunga mkono uamuzi wa Jukwaa la Kikristo kwa maelezo
kwamba jambo hilo limeamuliwa na viongozi wao wa juu, lazima
litekelezwe.
“Kwa kuwa wameshaamua, naamini tutapata
hiyo barua haraka tu, lakini mpaka sasa hatujasikia jambo lolote,”
alisema Mchungaji Emmanuel Owoya wa Usharika wa Nkwatira, Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Wilaya ya Hai.
Naye,
Mchungaji Jackson Mwaisabile wa Kanisa la Pentecostal Assemblies of God
(PAG) mkoani Iringa, alisema bado hajauona waraka unaosambazwa na
Jukwaa la Maaskofu na kwamba utakapowafikia watajua nini cha kufanya.
Mzee
wa Kanisa la Nguvu ya Uponyaji wa Ukombozi (LHPM) la Dar es Salaam,
Ayubu Luchenje alisema masuala la Katiba Inayopendekezwa na Mahakama ya
Kadhi yanahitaji kuyafahamu vyema kabla mtu hajatoa uamuzi wake.
Luchenje
alisema suala la Mahakama ya Kadhi linakiuka misingi ya Taifa kwa kuwa
Katiba iliyopo inaitambua nchi isiyo na dini. Alisema kwa msingi huo
jambo hilo linafanywa kisiasa kwa malengo ya kutaka kulifurahisha kundi
fulani katika jamii.
“Waziri Mkuu Mizengo Pinda
anachofanya ni kutaka kuwafurahisha watu fulani tu, jambo hilo
haliwezekani ufanye kitu kisichokubaliwa na Katiba,” alisema Luchenje.