Tundu Lissu apambana dakika 125

 >
 Msemaji wa kambi Rasmi ya upinzani Bungeni na Waziri kivuli wa ofisi ya waziri mkuu (uratibu na Bunge), Tundu Lissu akiwasilisha maoni ya kambi ya upinzani kuhusu mswada wa sheria  ya wakala wa usimamizi wa maafa wa mwaka 2014 Bungeni mjini Dodoma jana.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu juzi alitumia dakika 125 kupinga muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha vipengele.
Lissu, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alikuwa na kazi ngumu ya kupambana na Naibu Waziri wa Sheria, Mwanasheria Mkuu na baadhi ya wabunge wa CCM waliokuwa wakijaribu kusaidia kupitishwa kwa muswada ambao hata hivyo ulikwama kutokana na idadi ndogo ya wabunge waliokuwa ukumbini.
amoja na uwingi huo wa wapinzani wake, Lissu hakuonekana kukata tamaa wala kuingia hasira zaidi ya kumwambia Mwanasheria Mkuu, George Masaju, “stoop!” kutokana na kuchukua jukumu la kulishauri Bunge, kitendo ambacho Lissu alisema kinamkera kwa kuwa AG ni mshauri wa Serikali na si Bunge.
Lissu, ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema na kaimu kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, alipinga vifungu vyote 44 vya muswada huo, akisema kuwa unamuondolea mamlaka Rais ya kutangaza hali ya hatari, sheria mpya kudurufishwa bila ya kuwa na upya wowote na kwamba inavunja Katiba ya nchi.
Mvutano huo ulianza saa 12:00 jioni, lakini ulishika kasi kuanzia saa 1:25 hadi 3:25 usiku baada ya Bunge zima kukaa kama kamati kwa ajili ya kupitisha kufungu kimoja kimoja cha muswada huo, huku Lissu akisimama mara 19 kupinga kupitishwa kwa vifungu hivyo, akieleza kasoro zake na kushauri jinsi vinavyotakiwa kuwekwa, huku vingine akitaka vifutwe kabisa.
Kutokana na kuibuka kwa ubishani mkali na mrefu kati ya mbunge huyo, Masaju, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), Jenister Mhagama, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angela Kairuki na Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia na kusababisha muda kuyoyoma jambo lililomfanya mwenyekiti wa Bunge, Musa Azzan Zungu kulazimika kulihoji Bunge ili kupitisha vifungu husika.
Hata baadhi ya wabunge waliosimama kupinga hoja za Lissu, akiwamo mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu, Henry Shekifu (Lushoto, CCM) na kutoa ufafanuzi wa kisheria, hawakuweza kuzipangua hoja za mbunge huyo wa Singida Mashariki.
Wakati Lissu akianza kutoa ufafanuzi wa vifungu hivyo, mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali naye alikuwa ama akiunga mkono hoja za Lissu au kuja na hoja zake za kupinga muswada huo.
Hata hivyo, mbunge huyo baadaye alikata tamaa na kusema kuwa hana sababu ya kupoteza nguvu zake kutoa maoni ya msingi, mwisho wa siku yanapuuzwa na Serikali ambayo ilikataa kila pendekezo la wabunge hao.
“Nashangaa Mkosamali unakata tamaa,” alisema Lissu baada ya mbunge huyo kusema hawezi kuendelea kutoa hoja zaidi za kupinga muswada huo.
Wakati Mhagama akieleza kuwa sheria hiyo itasaidia wanaokumbwa na maafa na kukosa msaada, kutofautisha maafa na hatari ambazo kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Kudhibiti Maafa ya Mwaka 1990, zinatakiwa kushughulikiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Lissu alisema muswada huo hauna jipya.
Ilivyokuwa
Lissu alianza kusema kuwa Serikali inalenga kutumia sheria hiyo kuunda wakala wa kusimamia maafa ambao muundo, majukumu na utendaji wake hautakuwa na tofauti na kamati za maafa zilizopo kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti Maafa.
“Tatizo ni fedha. Serikali haitengi fedha za maafa. Kwa hiyo hata kama tukiunda wakala halafu tusitenge fedha haitasaidia,” alisema Lissu.
ADVERTISEMENT
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mkosamali na kueleza kuwa wakala huo ukiundwa utapokonya mamlaka ya kikatiba ya rais; ya kutangaza hali ya hatari, kuzuia watu kusafiri, kusafirisha vifaa na bidhaa na mambo mengine ya tahadhari, kwamba hatakuwa tena na mamlaka ya kutangaza hali ya hatari.
Lissu aliwachanganya mawaziri na Masaju na kuonekana wakiulizana baada ya kueleza kuwa vifungu vilivyopo kwenye sheria ya sasa ya maafa vinafanana na vilivyomo katika muswada huo.
“Kinachoonekana hapa na ambacho Serikali inakiri wazi ni kutokuwa na fedha za utekelezaji. Kama hali ndiyo hiyo iweje tupitishe sheria inayofanana na iliyopo. Tunachotakiwa kujadili ni jinsi ya kupata fedha ya kushughulikia maafa,” alisema Lissu.
Alisema kuwa kuongeza mamlaka zisizo na tija kwa wananchi ambazo uwepo na uendeshwaji wake mara nyingi unategemea kodi zinazolipwa na wananchi, ni kuongeza mzigo na utitiri wa watumishi wasio na shughuli za kufanya.
“Yaani mnapendekeza makatibu wakuu kuwa sehemu ya wakala endapo utaundwa, hawa sasa wa kazi gani? Maana wana shughuli nyingi,” alisema.
Mbunge huyo alipendekeza kufutwa kwa sehemu ya Tano ya Muswada huo yenye Ibara za 26 na 27 inayosema kuwa Rais hatatekeleza jukumu la kutangaza hali ya hatari, ambalo ni la kwake kikatiba, mpaka waziri aridhike kwanza.
Kwa nyakati tofauti Mhagama na Masaju walipingana na pendekezo hilo wakisema kuwa Rais lazima awe na wasaidizi ambao humshauri mambo mbalimbali.
Majibu hayo yalimfanya Lissu kupandwa na jazba na kumnyooshea kidole Masaju, akimweleza kuwa yeye ni mshauri wa Serikali si mshauri wa wabunge kutokana na Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali kudai kuwa anawapa ushauri wapinzani, akiwemo Lissu.
“Mimi huwa nakereka sana Mwanasheria Mkuu anaposema anatushauri. Mshauri wa Bunge ni katibu hivyo ‘stop’ kusema unatushauri,” alifoka Lissu.
Hali hiyo, ilimfanya Azzan kuingilia kati na kumweleza Lissu kuwa Rais hawezi kujua kila jambo linalotokea nchini, hivyo ni lazima watendaji wake wampe taarifa.
“Waziri yeyote anapopeleka taarifa kwa Rais, anatakiwa kuwa amejiridhisha kwa usahihi, hilo ndilo linalomaanishwa. Sisi tunaamini katika marekebisho tuliyofanya, katika misingi ya mamlaka ya Rais,” alisema.
Naye Mhagama alisisitiza kuwa “yanayotolewa na Katiba kwamba ndiye mtangazaji wa hali ya hatari nchini na tunabaki na msimamo kwamba waziri atatakiwa kuwa amejiridhisha ndipo apeleke kwa rais taarifa ya kumwezesha kutangaza hali ya hatari.”
Hoja hiyo ilipingwa na aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari waliodai kuwa wapo mawaziri mizigo ambao CCM imekiri wazi kuwa utendaji wao wa kazi hauridhishi, na kwamba wanaweza kushindwa kumfikishia rais taarifa.
Hata hivyo, wabunge wa CCM ambao ndiyo wengi walipitisha vifungu vyote vilivyokuwa vikipingwa na Lissu kwa kupiga kura ya ndiyo baada ya mwenyekiti kuwahoji.
posted Sunday, March 22, 2015 | by- Fidelis Butahe
Powered by Blogger.