Wiki ya ‘kutafuta maji’ yaanza
Wanawake wakifanya jitihada ya kutafuta maji kwa ajili ya matumizi katika familia zao. Picha na Maktaba.
Dar/Mikoani. Taifa leo linaanza maadhimisho ya Wiki ya Maji,
lakini vilio vimetawala kila kona ya nchi kutokana na uhaba mkubwa wa
huduma hiyo muhimu kwa afya na kufanya maashimisho hayo yaoneane kuwa ni
ya kutafuta maji.
Wiki ya Maji huadhimishwa kila mwaka
kuanzia Machi 16 hadi 22 kwa kujadili kero ya huduma hiyo ya msingi na
kuzindua miradi mingi, na mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika kitaifa
wilayani Musoma, ambako mradi wa maji ya Ziwa Victoria bado haujawa na
ufanisi mkubwa.
Uhaba wa maji umekuwa kero sugu na ya
muda mrefu kwa wananchi katika mikoa mingi, hasa ya Dar es Salaam,
Dodoma, Singida, Mara na Tanga na Kilimanjaro, mikoa ambayo idadi yake
ya watu ni zaidi ya robo ya idadi ya watu nchini kwa mujibu wa sense ya
mwaka 2012, na juhudi za kukabiliana na tatizo hilo hazijazaa matunda.
Ongezeko
la tatizo la maji linachangiwa na ukuaji wa shughuli za uzalishaji mali
katika sekta mbalimbali, hususan ni kilimo cha umwagiliaji, uzalishaji
umeme, viwandani, utalii, uchimbaji madini, ufugaji, uvuvi na hali
kadhali ongezeko la idadi ya watu.
Wakati kukiwa na
ongezeko kubwa la mahitaji ya maji, shughuli za binadamu zinachangia
kuharibiwa kwa vyanzo vya maji, ubovu wa miundombinu ya kusambaza maji,
bajeti ndogo isiyokidhi mahitaji ya wizara husika na mipango mibovu ya
kushughulikia tatizo hilo.
Dira ya taifa ya Maendeleo
2015, Mpango wa Maendeleo ya Milenia 2015 na Mkakati wa Kukuza Uchumi na
Kupunguza Umaskini Tanzania (Mkukuta), sambamba na Programu ya
Maendeleo ya Sekta iliyoanza mwaka 2007/08 ni mikakati inayolenga
kufikisha maji kwa asilimia 100 kwa wakazi waishio mijini na asilimia 90
vijijini.
Wakati takwimu za Serikali zikionyesha kuwa
asilimia 58.6 ya watu waishio vijijini wanapata maji salama na asilimia
86 ya watu waishio mijini wanapata maji safi, idadi ya watu waishio
vijijini ni asilimia 80, kitu kinachoonyesha kuwa tatizo hilo bado ni
kubwa.
“Mimi nafanya biashara saa zote, hata maji ya
Mchina (ya bomba yaliyotandazwa na Wachina) yakitoka, bado nitapata
tenda ya kuwapelekea wale wasioweza kubeba ndoo kichwani,” alisema
Hamisi China, mkazi wa Tabata anayejinufaisha na tatizo hilo kwa kuuza
maji.
Wafanyabiashara hao wana uwezo wa kupata kiasi cha angalau kati ya Sh5,000 hadi 10,000 kwa siku.
Maeneo
ya Mbezi Kimara kuna uhaba wa maji wa kudumu na wakazi wa maeneo hayo
hulazimika kununua maji yanayosambazwa kwa kutumia malori licha ya bomba
la maji kutoka Ruvu kupita maeneo yao.
Wakazi hao
hununua boza la lita 10,000 za maji kwa Sh75, 000, wakati kwenye maeneo
mengine maji hupatikana kwa Sh250 hadi Sh500 kwa dumu moja la lita 20,
kama maeneo ya Tabata.
Baadhi ya watu waliozungumza na
gazeti hili wamesema Wiki ya Maji haina maana yoyote kwao, na wengine
wamesema ingeitwa Wiki ya Uhaba wa Maji au kupendekeza fedha
zinazotumika kwenye maadhimisho hayo zitumike kuchimba visima.
Biashara ya maji
Licha
ya uhaba wa maji kuwatesa wananchi walio wengi, hasa akina mama, kwa
upande mwingine umewafanya vijana wachache kupata ajira kwa kuuza maji.
Biashara
hiyo imewanufaisha pia wafanyabiashara wenye magari ya kusambaza maji,
waliojenga visima na wakati mwingine hata Kampuni ya Majisafi na
Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) kutumia tatizo hilo kuuza maji kwa
kutumia magari badala ya kutandaza mabomba ili huduma hiyo iwafikie
wananchi kirahisi kwa unafuu.
Ahadi za maji
Mbali
na ilani ya CCM ya 2010 -2015 iliyoahidi kuwapatia maji watu wa mijini
kwa asilimia 90 na vijijini kwa asilimia 65 ambayo haijatekelezwa, hata
ahadi za viongozi mbalimbali kuhusu tatizo hilo hazijatimia.
Januari
2013 Rais Jakaya Kikwete alipokagua hali ya maji jijini Dar es Salaam,
aliahidi kuwa angeitisha kikao cha wadau Ikulu kujadili suala hilo,
lakini hadi sasa hajatekeleza ahadi hiyo.
Agosti 2014,
Waziri wa Maji, Profesas Jumanne Maghembe alimweleza Rais Kikwete kuwa
kuna miradi 1,055 inayojengwa nchini, kati ya hiyo miradi 250
imekamilika na inatoa huduma kwa watu 2,000 nchini.
Alisema
miradi mingine 538 inaendelea kujengwa katika vijiji 540 na ingekuwa
imekamilika ndani ya miezi sita na kuwahudumia wananchi 4,000 na miradi
mingine 525 ilikuwa inafanyiwa maandalizi ya ujenzi na ingeanza kujengwa
kuanzia Oktoba mwaka jana hadi Mwachi 2015 lakini haijakamilika.
Kauli ya Serikali
Alipoulizwa
kuhusu suala hilo, Naibu Waziri wa Wizara ya Maji, Amos Makalla alisema
chimbuko lake ni uzalishaji mdogo wa maji ukilinganisha na mahitaji ya
wakazi wa Dar es Salaam, ambao idadi yao kwa mujibu wa sense ya mwaka
2012 ni milioni 4.4.
“Nafahamu tuna changamoto ya
upatikanaji wa maji katika jiji letu lakini ukweli ni kwamba uzalishaji
ni mdogo. Hivi sasa tunazalisha lita milioni 300 za maji kwa siku kwa
ajili ya wakazi wa Dar es Salaam wakati mahitaji ni lita milioni 450 kwa
siku, na kufanya upungufu wa lita milioni 150,” alisema Makalla ambaye
wiki iliyopita aliahidi kuifumua Dawasco ili kupunguza ukubwa wa tatizo.
Makala alisema Serikali inatarajia tatizo kupungua baada ya kukamilika kwa miradi mitatu ya Ruvu Juu, Ruvu Chini na Ruvu Mpiji.
“Tunatarajia
miradi hiyo itakamilika ndani ya mwaka huu... tena mmoja ulikuwa
ukamilike mapema lakini kutokana na sababu mbalimbali haukuwezekana.
Hivyo itakapokamilika yote tutazalisha lita milioni 700 za maji kwa
siku, kiasi ambacho ni zaidi ya kile kinachohitajika,” alisema.
Akiwa
wilayani Igunga mkoani Tabora mwaka 2010, Rais Kikwete aliahidi kuwa
wananchi wa Tabora wangeanza kutumia maji kutoka Ziwa Victoria na hadi
sasa ahadi hiyo haijatimia.
Machi 5, mwaka huu Waziri
Maghembe aliwaeleza wanahabari kuwa mradi huo umeanza na utakamilika
ndani ya miezi 30 kwa gharama ya Dola 268.35 milioni za Marekani.
Uhaba wa maji na afya
Mei
2014, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilifanya utafiti kwa kushirikiana
na taasisi 14 duniani na kubaini kuwa vifo 842,000 vilivyotokana na
kuhara na kipindupindu mwaka 2014,vilisababishwa na uhaba wa maji. Hii
ni sawa na asilimia 1.5 ya vifo vitokanavyo na magonjwa.
Katika
ripoti maalumu iliyofanywa wilayani Handeni na gazeti hili mwaka 2010,
ilionekana kuwa uhaba wa maji umekuwa chanzo cha matokeo mabaya kwa
shule za wilayani humo.