Zitto ataja sababu za kujiunga ACT, asema hakuna kurudi nyuma
Zito Kabwe akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar kueleza sababu za yeye kuamua kujiunga na chama cha ACT. Picha na Edwin Mujwauzi
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe ametaja sababu tano za kujiunga na chama cha ACT-Tanzania huku
akijigamba kuwa yeye ni mchapakazi na kwamba sasa mambo yote ni mbele
kwa mbele.
Akimnukuu Rais wa zamani wa Ghana, Hayati
Kwame Nkrumah aliyewahi kusema, ‘forward forever, backward never’, jana
Zitto alisema, sasa ni wakati wa kuangalia mbele, hakuna kurudi nyuma
tena huku akijisifu kwa umahiri wake katika kazi.
“Mimi
ni mchapakazi…siangalii nyuma tena, naangalia mbele . Mapambano
yanaanza matokea mtayaona baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu,”alisema
Zitto kujiamini.
Zitto ambaye aling’atuka kutoka kwenye
nafasi ya Ubunge Ijumaa iliyopita kupitia Chadema na kujiunga na chama
ACT siku moja baadae, alisema watu wengi wamekuwa nini kingefuata baada
ya ya kuachia nafasi .
“Sasa napenda kuwaarifu kuwa
Machi 20, mwaka huu siku ya Jumamosi nilijiunga na chama cha ACT na
kukabidhiwa kadi ya uanachama na mwenyekiti ACT, Tawi la Tegeta.
Hii
ilikuwa moja katika siku muhimu kabisa katika maisha yangu ya
kisiasa,”alisema Zitto na kuongeza kuwa amelipa ada ya uanchama hadi
mwaka 2025.
Zitto ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alifunguka na kueleza
sababu za kuhamia katika chama hicho ambacho kimenzishwa juzi na siyo
chama kingine cha siasa, kama ambavyo watu wengi wanajiuliza.
“Nimejiunga
na ACT kwa sababu ninaona kwamba huku ndiko kunakaoendana na kile
ambacho mimi nimekipigania kwa miaka yote tangu nianze siasa, ambacho
nikuweka maslahi ya taifa mbele dhidi ya kitu kingine chochote,”alisema
Zitto huku akishangiliwa na baadhi ya wanachama wa chama hicho
waliohudhuri mkutano huko.
Alisema sababu nyingine ni
kwamba ACT ni chama pekee nchini kinachokubaliana na Itikadi ya Ujamaa
na kinaamini katika Falsafa ya Unyerere.
Aliongeza
kuwa, amejiunga na chama hicho kwa sababu ni chama kinachoamini katika
msingi wa uadilifu na kimeweka miiko ya maadili ya uongozi katika
kuhakikisha kwamba viongozi wote wa ACT wanakubaliana nayo na
wanaisaini.
“Naamini kuwa na miiko na maadili kwa
viongozi ni mwanzo wa kuhakikisha kwamba jamii yetu inaishi katika
uadilifu na kwamba viongozi wanakuwa na audilifu katika jamii,”alisema.
Aliongeza;
“Mtakumbuka kwamba katika miaka yangu yote ya ubunge nimepigania
uwajibikaji na uwazi. Hii ni misingi ambayo ninaamini kwamba ni moyo wa
utashi na umma,”
Alisema amafurahi kwamba kati ya
misingi kumi ya chama chake kipya, uwajibikaji na uwazi ni sehemu
muhimu. Uwazi ni sehemu ya jina la chama hicho .
Naye,
Msanii wa muziki wa Hip Hop, Seleman Msindi ambaye alikuwa mwanachama wa
Chadema, aliunga mkono hoja ya msemaji huyo na kusema kuwa Chadema
haikufanya jambo la busara kumfukuza Zitto.
Wanachama
wengine wapya ni pamoja na aliyewahi kuwa mgombea wa kura za maoni 2010,
Askofu Gerald Mpango, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Haki
za Binadamu Kanda ya Magharibi, Jaji Mstaafu Musa Kwikima, aliyekuwa
Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Tabora, Kansa Mbarouk.
Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kaliua, Jorum Mbogo, aliyewahi kuwa
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora na Mjumbe wa Kamati Kuu, Meck
Mzirai, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jimbo la Kahama kwa kiti cha Chadema,
Charles Lubala, Diwani wa Halmashauri ya Mabogini, Moshi vijijini kwa
kiti cha Chadema, Albert Msando.
Aliyewahi kuwa
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Iringa, Dokta Ben Kapwani, aliyewahi kuwa
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Katavi, John Mallac, aliyekuwa Kaimu
Mwenyekiti wa TLP Mkoa wa Mbeya na Mwenyekiti Wilaya ya Mbarali
Mwasimtwa Mwagongo na Katibu wa TLP Wilaya ya Mbarali Seleman Nyumile.