Mwanaume Auawa Kikatili kisa Ushirikina
Mtu mmoja aliyefahamika kwa majina ya Donald Peter Mwakajonga (62)
mkazi wa Kijiji cha Mkunga wilayani Rungwe, Mbeya ameuawa kwa kupigwa na
kitu kizito kichwani kwa kile kinachodaiwa kuwa ni imani za
kishirikina.
Habari kutoka kijijini hapo zinasema mwili wa Mwakajonga ulikutwa na majirani ukiwa nje ya nyumba yake.
“Mwili wake ulikutwa ukiwa nje ya nyumba yake hapa Kata ya Mkunga,
Tarafa ya Ukukwe, wilayani Rungwe Jumapili iliyopita, saa moja na
dakika hamsini asubuhi. Kwa kweli sisi tulishangazwa lakini inasemekana
aliuawa kutokana na imani za kishirikina,” alisema shuhuda mmoja
mwenyeji wa kijiji hicho aliyeomba jina lake kuhifadhiwa kwa kile
alichodai ni kutokana na usalama wake.
Aliongeza kudai kuwa, kuna baadhi ya watu walikuwa wakimsema mzee
Mwakajonga kwamba ni mchawi alikuwa akiwaroga wanakijiji na anaamini
kwamba watu hao ndiyo waliomuua.Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, SACP
Ahmed Msangi alipozungumza na mwandishi, alithibitisha kutokea kwa
kifo hicho.
“Ni kweli tukio hilo limetokea na inadaiwa kuwa chanzo cha kifo cha
mtu huyo ni kipigo kilichotokana na imani za kishirikina,” alisema
Kamanda Msangi.
Alipoulizwa kama kuna mshukiwa yeyote ambaye amekamatwa
hadi sasa alijibu: “Mpaka sasa tunamshikilia mtuhumiwa mmoja aitwaye
Daniel Venance mwenye umri wa miaka 35, mkazi wa kijiji hicho alichofia
marehemu na kutokana na tukio hilo sisi jeshi la polisi tunaendelea na
uchunguzi wetu.”
Kamanda Msangi aliwataka wananchi kuachana na tabia ya kujichukulia
sheria mkononi na badala yake akasema kama kuna mtu wanamhisi kutenda
maovu waliarifu jeshi la polisi ili aweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua
za kisheria baada ya kufanyika uchunguzi.