Zitto ahusisha hukumu yake na escrow
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amewaaga wapigakura wake kuwa hatakuwa tena mbunge wao, akisema kuwa kesi ya dhidi ya Chadema ilitupwa na Mahakama Kuu kutokana na baadhi ya majaji kutajwa kwenye kashfa ya escrow.
Chadema ilimvua
Zitto uanachama saa chache baada ya Mahakama Kuu kutupa shauri lake
alilofungua akitaka chombo hicho cha sheria kimlazimishe katibu mkuu wa
chama hicho kumpa nyaraka za mwenendo wa vikao vya Kamati Kuu
vilivyomvua nyadhifa zote, huku akifanikiwa kupata amri ya muda ya
kuizuia Chadema kumjadili.
Akizungumza katika mkutano
wa hadhara uliofanyika Kata ya Mwandiga mkoani Kigoma jana, Zitto
alisema hatakuwa mbunge wa jimbo hilo baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba
mwaka huu, na akatumia fursa hiyo kueleza safari yake ya kisiasa ndani
ya Chadema na mtazamo wake baada ya kufukuzwa uanachama.
“Nimejifunza
mengi nikiwa mbunge. Katika utumishi wangu kwenu, bungeni nimejifunza
namna nchi yetu inavyoendeshwa. Katika kujifunza huko kuna mambo kadhaa
nimefanya ya kujivunia na mengine ni makosa,” alisema Zitto ambaye
alikuwa naibu katibu mkuu wa Chadema.
“Nimejifunza
kuwa mzalendo zaidi kwa nchi yangu na kuwatumikia watu wa nchi hii.
Ndiyo maana hamkunisikia tu nikitetea watu wa Kigoma pekee, bali watu
maeneo mengine ya nchi yetu na makundi mbalimbali ya kijamii.”
Alisema safari yake ya ubunge ilikuwa ngumu yenye mafunzo makubwa na imemfanya apevuke kifikra na kupata mafunzo.
Awali,
akizungumza na waandishi wa habari, Zitto alisema: “Bado nina nia ya
dhati ya kuendelea kuwatumika Watanzania kama mwakilishi wao kupitia
jimbo lolote nchini.
Nitaendelea kuwapo kwa uwezo wa
Mungu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba. Itakuwa kwa tiketi gani na jukwaa
gani watu watayajua hayo wiki hii.”
Akizungumzia
sakata la escrow lililowahusisha watendaji mbalimbali wa Serikali,
wakiwamo majaji na hukumu ya kesi yake, Zitto alirudia tena kauli yake
kuwa hukumu hiyo imetolewa bila yeye kujua. “Kwa kazi ninazozifanya kuna
miguu ya watu wengi ninayoikanyaga.
Moja ya
ninaowakanyaga ni mahakama. Kuna majaji ambao taarifa ya kamati ya PAC
imewataja kuhusika na escrow na wanatakiwa kuchunguzwa,” alisema.
Alisema inawezekana ndani ya mahakama wameona hukumu ya kesi hiyo ndiyo eneo zuri la kumkomoa.
“Inawezekana
pia watu ambao kupitia kazi za PAC, nimesababisha wachukuliwe hatua nao
pia wanaweza kuwa wameshiriki kwa njia moja au nyingine. Lakini pia
inawezekana ni taratibu za kawaida za mahakama. Mpaka hukumu inatolewa
kuna maswali mengi hayana majibu,” alisema.
Alisema
wanatilia shaka hukumu hiyo kutokana na mahusiano ya karibu yaliyokuwapo
kati ya mahakama na mawakili wa Chadema kwa maelezo kuwa yeye na wakili
wake hawakuwa nayo na kwamba hawakupata taarifa za kuitwa mahakamani.
“Kwetu
sisi hukumu hii ni mshangao. Tulivyoenda kutaka hukumu ya kesi siku
mbili mfululizo tulinyimwa, siku ya tatu tulivyoitaka tulielezwa kuwa
faili limechukuliwa na jaji kiongozi kwa ajili ya mapitio,” alisema.
Alisema
kilichotokea kimempa funzo na kwamba iwapo atapata fursa ya kufanya
mabadiliko nchini, idara ya mahakama ni sehemu ambayo ataifanyia
mabadiliko makubwa kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa wananchi.
Kuhusu
uhuasiano wake na Freeman Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, Zitto
alimponda kiongozi huyo kuwa ana tabia za ‘undumilakuwili’, na
kusisitiza mara kadhaa amekuwa akimtumia (mbunge wa Moshi Mjini,
Philemon) Ndesamburo kuwasuluhisha, lakini akiwa pembeni amekuwa akitoa
kauli za kumponda yeye (Zitto) kuwa amemsadia mambo mengi. “Nikikaa peke
yangu huwa najiuliza ni nini ambacho kimetokea, sipati jibu.
Ninachokiona ni ugomvi wa madaraka na juhudi za watu kutaka kuwaondoa
wengine katika ulingo. Katika mazingira kama hayo watu wanaweza
kutafsiri nina ugomvi naye,” alisema. Zitto pia aliponda kanuni za
Chadema zinazoeleza kuwa mwanachama akifungua kesi mahakamani kupinga
uamuzi wa chama anafukuzwa uanachama na kuwataka wana-Chadema kuipinga
kanuni hiyo.
Akizungumzia madai ya kutumiwa na CCM na
usalama wa Taifa, Zitto alianza kwa kueleza jinsi alivyoibua hoja nzito
bungeni na kuongoza kamati yake ya PAC kuibua mambo yaliyowang’oa
mawaziri mara tatu kwa nyakati tofauti, na kuhoji kuwa kama angekuwa
anatumiwa na CCM asingeweza kuibua hoja za kuiangusha Serikali ya chama
hicho tawala ndani ya miaka mitano bungeni.