Zitto atinga bungeni, aomba ushauri kwa spika

 
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango Malecela akimlaki Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alipowasili ndani ya kumbi ya Bunge Miji Dodoma jana. Kushoto ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba
Dodoma. Siku tisa baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza kumvua uanachama, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe jana alitinga bungeni na kufanya kikao cha siri na Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa zaidi ya saa moja.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa watu walio karibu naye, mbunge huyo alipanga kuaga wabunge jana asubuhi baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, lakini baadaye alilieleza gazeti hili kuwa atazungumzia hatima ya ubunge wake leo.
Mbunge huyo ambaye pia jana alichangia mjadala wa Muswada wa Sheria ya Udhibiti wa Ajira za Wageni wa Mwaka 2014, alipowasili bungeni wabunge wengi walidhani angewaaga kutokana na taarifa zilizosambaa mjini hapa juzi kuwa angetumia siku ya jana kuaga lakini hakufanya hivyo.
Akizungumzia hali hiyo Zitto alisema: “Kuhusu mimi kuaga bungeni we subiri tu. Kama jambo hilo lipo litakuwepo tu. Ila kwa sasa, nimeitwa na Spika Makinda na ndiyo nakwenda kuzungumza naye.”
Aliongeza, “Si unaniona bwana, nimekuja bungeni na kama nisingekuwa mbunge nisingekuja. Nitazungumza tu, ila kwa sasa ngoja tuone mambo yatakavyokwenda.”
Hata hivyo, habari kutoka kwa watu walio karibu na Zitto zililieleza gazeti hili kuwa mbunge huyo atatoa kauli leo baada ya kushauriana na spika wa sasa, spika aliyepita, Waziri Mkuu wa sasa (Mizengo Pinda), waziri mkuu aliyepita, aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Chadema, Said Arfi na washauri wake wa karibu kuhusu suala hilo.
Zitto alipoulizwa kuhusu hilo, alisema, “Aliyekueleza yuko sahihi, nitaongea kesho (leo) jioni kabla ya Bunge kuahirishwa ili kuweka wazi msimamo wangu kuhusu kinachoendelea kwenye ubunge wangu.”
Chadema ilitangaza kumvua Zitto uanachama siku tisa zilizopita, saa chache baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kutupa shauri lake alilofungua akitaka chombo hicho cha sheria kimlazimishe katibu mkuu wa chama hicho kumpa nyaraka za vikao vya Kamati Kuu vilivyomvua nyadhifa zote.
Awali, Mahakama hiyo ilitoa amri ya muda ya kuizuia Chadema kumjadili na amedumu kwenye nafasi ya ubunge chini ya zuio hilo kwa takriban mwaka mmoja.
Iwapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itapokea taarifa ya kuvuliwa kwake uanachama na kumjulisha Spika, Zitto atakuwa amepoteza kiti hicho.
Mpaka sasa ubunge wa Zitto ni kama unaning’inia kutokana na kitendo cha kutupiana mpira kati ya Ofisi ya Bunge, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Chadema kuhusu hatima yake, huku mwenyewe akisisitiza kuwa bado ni mbunge.
Kutupiana mpira kulijitokeza juzi baada ya Makinda kusema Bunge linasubiri taarifa rasmi ya kufukuzwa uanachama kwa mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kutoka NEC, ambayo hata hivyo, nayo ilisema inasubiri taarifa kutoka Chadema ambacho kilisema kinashughulikia kwanza kesi zinazowakabili wanachama wake wanaotuhumiwa kumpiga aliyekuwa mlinzi wa Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa.
Wiki iliyopita mbunge huyo aliwaaga wapigakura wake wa Kigoma Kaskazini akisema hatagombea ubunge tena katika Jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu Oktoba.
Posted Thursday, March 19, 2015 | by- Fidelis Butahe
Powered by Blogger.