Nyalandu: Urais CCM, Ukawa ni kivumbi
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu (kushoto) akizungumza na
wahariri wa magazeti ya Mwananchi Communicatons Limited (MCL),
alipoitembelea kampuni hiyo iliyopo Tabata, Dar es Salaam jana, kulia ni
Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai.
Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu amesema uchaguzi wa Rais ajaye utakuwa na ushindani mkubwa
ndani na nje ya CCM, huku akibainisha kuwa haogopi mtu kati ya wote
wanaotajwa kwenye kinyang’anyiro hicho, bali anawaheshimu.
Lakini
mbunge huyo wa Singida Kaskazini amesema mgombea pekee atakayemwogopa
ni yule atakayekuwa anataka kulipiza kisasi dhidi ya wagombea wengine.
Waziri
huyo alitoa kauli hiyo jana wakati alipofanya ziara kwenye makao makuu
ya Ofisi za Mwananchi Communications inayozalisha magazeti ya The
Citizen, Mwananchi na Mwanaspoti zilizoko Tabata Relini kando ya
Barabara ya Mandela.
“Sipendi kulizungumzia sana jambo
hilo,” alisema Waziri Nyalandu ambaye huzungumza kwa sauti ya chini na
taratibu... “Kwenye chama chetu (CCM) muda wake bado. Lakini naweza
kusema kuwa mwaka huu ni wa ushindani mkubwa ndani ya CCM na
‘opposition’,” aliwaambia wahariri wa Mwananchi Communications.
“Mwisho
tutakuwa na kambi ya CCM. Kwaya ya CCM itapambana na kwaya nyingine
ambayo ina sauti zote nne kama CCM,” alisema akimaanisha kuwa upinzani
nao utakuwa umekamilika na kusisitiza muda ukifika atachukua fomu.
Kauli
ya Nyalandu imekuja wakati nchi ikijiandaa kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu
utakaoiweka madarakani Serikali ya Awamu ya Tano, hali ambayo inaipa
shida CCM kumpata mrithi wa Rais Jakaya Kikwete ambaye pia atalazimika
kuachia uenyekiti wa chama hicho.
Tayari wanachama
wanne wa CCM wameshatangaza nia, akiwamo Nyalandu. Wengine ni Hamisi
Kigwangala, ambaye ni Mbunge wa Nzega, January Makamba (Naibu Waziri wa
Sayansi na Teknolojia) na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Hata
hivyo, kinyang’anyiro kikubwa kinatarajiwa kuwa miongoni mwa makada wa
muda mrefu wakiongozwa na Edward Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu na
Bernard Membe (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa),
ambao hawajatangaza nia, lakini wanatumikia adhabu ya kufungiwa kwa
zaidi ya miezi 12 kwa makosa ya kukiuka taratibu za chama hicho kwa
kuanza kampeni mapema.
Wengine wanaotajwa kwenye mbio
hizo ni Mwigulu Nchemba, ambaye ni Naibu Waziri wa Fedha (Sera), Waziri
wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira, Mbunge wa Songea Mjini,
Emmanuel Nchimbi, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Mbunge wa
Sengerema, William Ngeleja.
Wakati CCM ikiwa na kazi ya
kumpata mgombea wake wa urais, hali ni ngumu zaidi safari hii nje ya
chama hicho kutokana na vyama vinne vya upinzani kukubaliana kusimamisha
mgombea mmoja kwenye kila nafasi.
Chadema,
NCCR-Mageuzi, CUF na NLD vimeunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na
vimesaini makubaliano ya kusimamisha mgombea mmoja.
Nyalandu,
ambaye alitangaza nia yake wakati akiwa jimboni kwake, alisema mjadala
wa kuelekea Uchaguzi Mkuu unatakiwa ujikite kwenye masuala ya kuiondoa
nchi kutoka hapa ilipo na kwenda juu zaidi.
“Baada ya
miaka 50, ungetegemea mjadala uwe katika kufufua uchumi, kuongeza ajira,
usalama wa wananchi, enlightment ya watu au elimu, afya na rasilimali.
Huo ndiyo uwe mjadala kwa watakaowania nafasi ya urais,” alisema.
“Wagombea
wote wa CCM na Ukawa tujadili namna gani tutaifanya Tanzania kuwa bora.
Ni namna gani tutajibu maswali ya Watanzania kwa wakati uliopo.”
Akijibu
swali kuwa kati ya wanaotajwa kuwania urais, ni yupi tishio kwake na
anayemwogopa, Nyalandu alisema: “Hakuna cha kuogopa, wote nawaheshimu.
“Kwa
sisi Walutheri, tunaambiwa ‘kisasi ni juu yangu, asema Bwana,” alisema
akinukuu maandiko ya kitabu kitakatifu cha Kikristo cha Biblia.
“Ninayemwogopa
zaidi ni atakayekuwa na revenge (kisasi). Ukiwa mtu wa kisasi ni
hatari, lakini ‘daima mwombee adui yako uzima’ ili aone utakapofanikiwa
na ajifunze.”
Hata hivyo, alisema ni vigumu kwa anayeshinda uchaguzi kutekeleza nia yake ya kulipa kisasi.
“Naamini
yeyote atakayeongoza ataongoza kwa Katiba ya Tanzania. Uongozi (rais)
ujao uwe wa maono juu ya nchi yetu, uzingatie uzalendo na heshima kwa
wote.”
Kuhusu mjadala wa umri kwa nafasi ya urais, Nyalandu alisema hakuna mtu mwenye wakati wake.
“Nasikia
maneno kuhusu ujana na uzee. Huu ni wakati wa wote. Uongozi wa nchi
unategemea busara siyo umri, mdogo au mkubwa,” alisema Nyalandu, ambaye
ana umri wa miaka 45.
Akizungumzia kauli ya Katibu Mkuu
wa CCM, Abdulrahman Kinana aliyempamba Lowassa na kumwita yeye kuwa
mzururaji, Nyalandu alisema hawezi kuzungumzia hilo kwa kuwa hajamsikia
akisema hayo, lakini akasema wanafanya kazi vizuri na alishawahi
kumwagia sifa wakati alipotembelea jimboni kwake... “Kinana alikuja na
Singida Kaskazini na kati ya watu aliowasifia sana alikuwa huyu Lazaro
Nyalandu,” alisema waziri huyo na kuongeza: “Kinana alikuta kila kijiji
kina maji kwa nguvu za wananchi, wafadhili au Serikali ilichangia.
Nilipoanza ubunge miaka 15 iliyopita mtu akijenga kwa bati alikuwa
anarogwa au anapata hofu ya kurogwa, lakini sasa nyumba za nyasi ni za
kuhesabu. Mwandishi ambaye angechukua stori ya Singida Kaskazini, kwa
kauli ya Kinana, angeandika: ‘Nyalandu mfanyakazi wa kutisha’.”
Utendaji wizarani
Waziri Nyalandu alitumia muda mwingi kuelezea utendaji
wa wizara yake, akisema ni ngumu kwa kuwa inagusa kila nyanja ya maisha
ya Watanzania na inayomfanya awaonee huruma watoto wake kutokana na
kutopata muda mwingi wa kuwa nao.
Alisema ni muhimu
uhifadhi wa maliasili usaidie maisha ya kawaida ya kila siku kwa
wananchi, lakini pia rafiki wa uhifadhi huo awe mwananchi mwenyewe.
Kuhusu
mapambano dhidi ya ujangili alisema Serikali kupitia wizara yake
inapambana na tatizo hilo ndani na nje ya nchi kwani lengo la dunia ni
kukomesha mtandao wa ujangili.
“Hatua kubwa nilichukua
kuagiza sensa ya tembo ili tuwe na uwazi. Sensa zilizofanyika Serengeti,
Mara na Kenya zinaonyesha ongezeko kubwa la tembo. Kuna mahali
tumefanikiwa, lakini kuna mahali wamepungua. Niliamua tupate ukweli
kwanza. Mwezi ujao tutatangaza matokeo ya sensa hiyo,” alisema Nyalandu.
Akizungumzia
hatua ya Kenya kuteketeza akiba ya meno yake ya tembo na Tanzania
kutofanya hivyo, alisema Serikali iliamua meno hayo kutofanyiwa
biashara, lakini akasema suala la historia pia ni muhimu kwa kuwa kuna
meno ambayo ni ya tembo wa zamani na ni makubwa hayawezi kupatikana
dunia ya sasa.
Alisema pia kuna meno ambayo hupatikana
baada ya tembo wazee kufa na kwamba meno hayo zaidi 100,000, yote
huwekewa alama ya utambuzi na kupimwa vinasaba (DNA) ili unapotokea
uhalifu yaweze kutambulika kwa urahisi.
“Sisi hatutachoma moto meno yetu ya tembo, bali tutakuwa wawazi kitaifa na kimataifa,” alisema.
Alisema
kuwa katika vita dhidi ya ujangili duniani ni habari njema kusikia
kwamba China imeacha kuingiza meno ya tembo kwa mwaka mmoja na kuongeza
kuwa ombi la Tanzania ni kuitaka nchi hiyo iache kabisa.
Pia
alielezea jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanyika kukabiliana na
ujangili, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa kama ndege pamoja na
makubaliano na nchi jirani za Kenya, Zambia na Msumbiji ili kuwa na
harakati za pamoja katika kuwanasa majangili na kukomesha usafirishaji
kwa njia ya reli, bahari na ndege.
Alisema ulinzi wa
asili pia ni muhimu katika hifadhi na mbuga za wanyama na kwamba ili
kuimarisha ulinzi, mwaka uliopita wizara yake iliajiri askari wa
wanyamapori 500 na wengine idadi kama hiyo walikuwa wa muda.
“Tatizo
la ujangili ni kubwa, askari wanapoteza maisha kwa kushambuliwa na
majangili. Lakini sasa tumeleta askari wa Marekani wanatoa mafunzo kwa
askari wetu ili nao waweze kuwa walimu wa wenzao. Hayo ni mafunzo
endelevu, majeshi yetu yanashirikiana na Marekani katika mafunzo ya
kupambana na ujangili,” alisema.
Kukaa ofisini
Akizungumzia
tuhuma kwamba hakai ofisini na kazi zake za uwaziri anazifanyia
hotelini, Nyalandu alisema anatumia muda wake ofisini kama mawaziri
wengine na kwamba hata angekaa ofisini, watu wangesema anashinda ofisini
bila ya kuhudumia wananchi.
“Jambo hilo siyo kweli. Hizo ni siasa chafu. Hii inalenga kumchafua mtu na kuharibu sifa yake.”
Alibainisha
kuwa kutokana na utendaji wake na walio chini yake, kwa mara ya kwanza
wizara hiyo mwaka huu imeongoza kwa kuliingizia taifa fedha za kigeni.
“Pia
inaongoza kwa kutoa ajira 500,000 za moja kwa moja na nyingine milioni
mbili kupitia sekta zake. Dola 1.7 bilioni ziliingia katika uchumi.
Unaweza usimpende mtu, lakini kwa anayofanya mafanikio yapo wazi,”
alisema Nyalandu.
Alipoulizwa kuhusu kutowekwa
hadharani kwa taarifa ya tume ya kimahakama iliyochunguza Operesheni
Tokomeza, licha ya kukiri Nyalandu alisema kuwa wakati ukifika itawekwa
hadharani.
“Hata mimi ilinihoji kwa saa tatu. Bado tunasubiri itolewe rasmi. Ni tume ya kimahakama, wote waliohusika walihojiwa,” alisema.
Kuhusu
utalii waziri huyo alisema ni jukumu la kila Mtanzania kuutangaza.
Alisema katika kuhakikisha Tanzania inajulikana zaidi kimataifa katika
utalii, tangazo la viwango vya kimataifa lililotengenezwa Hollywood
linakaribia kukamilika.
“Tangazo hilo limetengenezwa
kwa gharama za wafadhili wenyewe na hakuna hata fedha ya Tanzania
iliyotumika. Hivi sasa linafanyiwa editing (linahaririwa). Litakuwa la
aina yake,” alisema.
Akizungumzia tozo la kodi kwa
hoteli za kitalii jambo ambalo lilizua mjadala katika kikao cha Bunge
Desemba mwaka uliopita, Nyalandu alikanusha tuhuma kwamba Februari mwaka
huu alikutana na wamiliki wa hoteli hizo na kueleza kuwa alimwagiza
Katibu Mkuu wa wizara yake kufanya hivyo.
Alisema
awali, hoteli zilikuwa zikikatwa asilimia 10 kwa kila kitanda, lakini
baadaye ikaondolewa na badala yake tozo ikawa ya makisio ambayo
ilisababisha baadhi ya wamiliki wa hoteli kulalamika hivyo kumuagiza
katibu wake kwenda kujadiliana nao ili kufikia muafaka.
“Ilikuwa
lazima wakubaliane kuhusu njia ya ukokotoaji kodi husika na siyo
makisio bila ya kuwa na msingi wa makisio. Tangazo la Serikali la mwaka
2009 lilihusu hoteli 27 tu, lakini tangu wakati huo kuna hoteli 30
zimejengwa na nyingine 15 zinaendelea kujengwa,” alisema.