JK awaambia polisi wakae mguu sawa
Rais Jakaya Kikwete akikagua gwaride maalumu wakati wa hafla ya kuwatunukia vyeo maofisa 289 wa Polisi katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam jana. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete
amelikata Jeshi la Polisi nchini kujiandaa kikamilifu ili kukabiliana na
vurugu zozote zitakazojitokeza wakati wa uandikishaji wapigakura,
upigaji Kura ya Maoni ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Akifunga mafunzo ya maofisa
warakibu wasaidizi katika Chuo cha Taaluma ya Polisi, Dar es Salaam
jana, Rais Kikwete alisema dalili zinaonyesha kwamba kuna watu wenye nia
ya kuhatarisha amani katika matukio hayo.
“Tunayoyasikia
na tunayoyaona yanaashiria kuwapo kwa dalili za wenzetu kukwamisha
shughuli hizi za kitaifa kwa kufanya vurugu, Jeshi la Polisi jiandaeni
na vitendo vyote vitakavyofanywa kwa lengo la kuhatarisha amani,”
alisema akijibu maombi ya kupatiwa vifaa yaliyowasilishwa kwake na Mkuu
wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu.
Alisema Serikali
itahakikisha kazi ya uandikishaji katika daftari la wapigakura, upigaji
wa kura ya maoni na uchaguzi mkuu vinafanyika kwa amani na utulivu kwa
gharama zozote.
Alisema ili kufanikisha kazi hiyo,
Serikali italiwezesha Jeshi la Polisi ili litekeleze kikamilifu majukumu
yake ya kulinda amani na utulivu.
“Tutawawezesha kwa
kuwapa vifaa ili kuhakikisha mnafanya kazi yenu ya kutunza amani kwa
umakini zaidi,” alisema Rais Kikwete anayemaliza muda wake wa mihula
miwili ya urais baada ya uchaguzi mwaka huu.
Iwapo
mambo yote yatakwenda kama yalivyopangwa, Kura ya Maoni ya Katiba
Inayopendekezwa itapigwa Aprili 30 wakati Uchaguzi Mkuu utafanyika
Oktoba.
Profesa Lipumba apinga
Akizungumzia
kauli hiyo ya Rais Kikwete, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
alisema, “Rais Kikwete yeye ndiye mtu wa kwanza kuivuruga amani kwa
kutangaza tarehe ya kufanyika kwa kura ya maoni wakati siyo jukumu lake
na jukumu hilo ni la NEC, Serikali yake kushindwa kuratibu vyema
mchakato wa uandikishaji.
“Kama uandikishaji hauendi
vizuri mpaka sasa, anavunja sheria za nchi halafu yeye mwenyewe tena
anakwenda kwa vyombo vya dola na kuvieleza vijiandae wakati yeye
huyohuyo ndiye ameanzisha uvunjifu wa amani tunashindwa tumweleweje,”
alisema.
Profesa Lipumba alisema kinachotakiwa
kufanyika kwa sasa ni NEC kutangaza tarehe kamili ya uchaguzi na
uandikishaji uende kwa utaratibu tofauti na ilivyo sasa kwa mkoa mmoja
wa Njombe kusuasua mambo ambayo yanaashiria uvunjifu wa amani.
Kuhusu rushwa
Akizungumzia
tuhuma za rushwa dhidi ya polisi, Rais Kikwete alisema tafiti
mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanyika nchini zinaonyesha kwamba taasisi
hiyo bado inaongoza kwa rushwa.
“Bado kuna wenzenu
wachache ambao wanachukua rushwa, wachukulieni hatua ili mwondokane na
aibu hii, msikubali watu wachache waharibu sifa nzuri ya Jeshi la
Polisi,” aliagiza.
Roho mbaya
Kikwete aliutaka uongozi wa
Jeshi la Polisi kujenga utamaduni wa kuwapandisha vyeo askari polisi ili
kuwaongezea ari ya kufanya kazi.
“Zamani viongozi wa
polisi walikuwa na roho mbaya hawakuwa wakiwapandisha vyeo askari,
nikawauliza kwa nini, lakini hawakuwa na majibu, inasikitisha vyeo vipo
lakini mtu anasota kwa miaka mingi na kacheo kale kale, acheni roho
mbaya pandisheni vyeo askari kila inapobidi,” alisema.
Alisema kuna umuhimu wa kuwa na jeshi lenye wasomi wengi ili waweze kukabiliana na mbinu mpya za uhalifu.
“Wahalifu wanaendelea kubuni mbinu za kila aina, tunatakiwa kuwa na wasomi ambao wataweza kukabiliana na mbinu hizo,” alisema.
Aliutaka
uongozi wa jeshi hilo kuongeza idadi ya polisi wanawake ili kuimarisha
dawati za jinsia kwenye vituo vya polisi, kitendo kitakachopunguza
vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Ujambazi
Kuhusu ujambazi, Rais Kikwete alisema katika kipindi chake, jeshi hilo limefanya kazi kubwa katika kukabiliana na ujambazi.
“Wakati
naingia madarakani nilikuta matukio ya majambazi kuingia na kuiba fedha
hadi benki, matukio hayo yalikuwa ya kawaida kuyasikia, nikasema
majambazi hayawezi kuachwa yatambe,” alisema.
Alisema
hivi sasa matukio hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa na akalipongeza
jeshi hilo kwa kazi nzuri ingawa bado kuna matukio machache.
Awali,
IGP Mangu alimwomba Rais Kikwete kuliwezesha jeshi hilo kivifaa ili
liweze kujiandaa mapema na upigaji wa kura ya maoni na uchaguzi mkuu.
“Tunaomba
tuwezeshwe vifaa mapema ili tuweze kuvifanyia mazoezi kabla ya upigaji
wa kura ya maoni na uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani baadaye
mwaka huu,” alisema.
Mkuu wa Chuo cha Maofisa wa Polisi
Dar es Salaam, Ali Lugendo alisema askari 290 wamehitimu mafunzo hayo
na hivi sasa watakuwa warakibu wasaidizi wa polisi.
Alisema
wahitimu hao watakwenda kuwa viongozi kwenye vituo mbalimbali vya
polisi vya wilaya na hivyo kuwa wasimamizi wa nidhamu kwa askari.