Mvua yazua balaa Buguruni, watu 1,163 hawana mahali pa kuishi
>
Mkazi wa eneo la Buguruni kwa Mnyamani akihamisha vitu vyake jana baada
ya makazi yao kukumbwa na mafurika kutokana na mvua inayoendelea
kunyesha jijini Dar es Salaam. Picha na Said Khamis
Zaidi ya wakazi 1,163 wa eneo la Buguruni kwa Mnyamani hawana mahali pa kuishi baada ya nyumba zao 517 kukumbwa na mafuriko.
Akizungumza
jana na gazeti hili, Mwenyekiti wa Mtaa wa Buguruni kwa Mnyamani,
Abdallah Mng’ae alisema maji hayo yanaendelea kuongezeka na madhara
zaidi yanaweza kutokea kutokana na mvua kuendelea kunyesha.
Alisema siku ya kwanza, nyumba 30 zilikumbwa na mafuriko, lakini kadri mvua inavyozidi kuendelea ndivyo maafa nayo yanaongezeka.
“Wengi
wao waliokumbwa na mafuriko hayo kwa sasa wanalala katika vibaraza vya
watu wakiwa na watoto wadogo, wanapigwa na baridi usiku kucha,” alisema
Mng’ae na kuongeza:
“Hadi sasa hawajapata msaada wowote kutoka serikalini, tunaomba msaada hasa chakula, mavazi na dawa.”
Alisema
watu waliojitokeza kutoa msaada ni Mwenyekiti Taifa wa Chama cha
Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba aliyetoa Sh500,000.
Eneo la Vingunguti, mwandishi alishuhudia nyumba nyingi
zikiwa zimejaa maji, huku wamiliki wakilalamika kuwa vitu vingi
vimeharibika.
Mkazi wa eneo hilo, Amina Salehe alisema
tangu juzi hadi jana maji ya mvua yameendelea kuingia ndani ya nyumba
yake na kumsababishia kukosa sehemu ya kulala.
Wakati
huohuo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema mvua itaendelea
kunyesha kwa siku tatu mfululizo katika mikoa ya Pwani, Mtwara, Lindi,
Dar es Salaam na Tanga.
Akizungumza katika maadhimisho
ya Siku ya Hali Hewa jana, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agness Kijazi
aliwataka wananchi wanaoishi mabondeni kuhama ili kuepuka madhara
yanayoweza kuwakumba.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Samwel Mwampashe alisema polisi wanaendelea kufanya doria ili kubaini madhara zaidi.
Naye
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema
hawajapata taarifa ya kutokea kwa vifo mkoani humo zaidi ya zile za
baadhi ya watu kukosa makazi baada ya nyumba zao kujaa maji.