Kenya, Nigeria zagoma kuiazima Tanzania BVR
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), Jaji Damian Lubuva amesema ofisi yake ilijaribu kuazima vifaa vya
kielektroniki vya Biometric Voters Registration (BVR) katika nchi ya
Kenya na Nigeria kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura, lakini nchi hizo
zilikataa.
Uamuzi wa NEC wa kutaka kuazima vifaa hivyo
ni kutokana na mchakato wa uandikishaji kukwama kwenda kama ulivyopangwa
kutokana na BVR 250 zilizopo kutokuwa na uwezo wa kuandikisha wapiga
kura wote nchini.
Kitendo hicho kinaweza kusababisha
Kura ya Maoni iliyopangwa kufanyika Aprili 30 mwaka huu kushindikana
kwani mpaka sasa ni mkoa wa Njombe pekee uandikishaji unaendelea
kufanyika ambako utamalizika Aprili 12, 2015.
“Tulitaka
kuazima Kenya lakini wakasema wanavitumia hata kama wamemaliza uchaguzi
lakini mchakato wao wa uandikishaji unaendelea kutokana na kwamba watu
wao wanapofikisha umri wa kuandikishwa wanawaingiza katika daftari lao,”
alisema Jaji Lubuva na kuongeza:
“Tulikwenda Nigeria nako walitueleza wanazitumia. Kuazimana siyo jambo geni kwetu na huu ndiyo ukweli wake.”
Kuhusu
mchakato wa uandikishaji mkoani Njombe alikoweka kambi alisema:
“Uandikishaji huku unakwenda vizuri licha ya kauli mbalimbali na mimi
nimekuwa nikiwahamasisha kujitokeza na tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa.”
Katika
uchaguzi wa Ghana uliofanyika mwaka 2013 mfumo wa BVR ulitumika na
kuonyesha mafanikio makubwa. Hata hivyo, Malawi iliukataa mfumo huo
katika uchaguzi wa mwaka 2014 baada ya kuonyesha udhaifu mkubwa katika
uchaguzi wa mwaka 2005.
Katika mahojiano maalumu na
viongozi, wahariri na waandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi
Communications Ltd (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti
na The Citizen makao makuu ya kampuni hiyo Tabata Relini Dar es Salaam
jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema, NEC ilianza
mchakato huo bila vifaa ikitegemea kuazima.
“Tulipokwenda
Kenya na TCD (Kituo cha Demokrasia Tanzania) kuangalia walivyofanikisha
mchakato huo wakatueleza kuwa NEC walikuja hapa kuazima BVR za
kuandikisha... tulikuwa na mawaziri pale yaani ilikuwa aibu na
walitueleza kama hadi Novemba hamjanunua hamuwezi kuandikisha. Walisema
walikuwa na BVR 15,000 Kenya na waliandikisha wapiga kura milioni 14 kwa
zaidi ya siku 45 hadi 60, sisi tuna matatizo, matatizo.
“Wanatupa
wasiwasi mkubwa, ikiwa lengo ni kuandikisha wapiga kura wote
haiwezekani tukawa na kura ya maoni Aprili 30, lakini ukiwa unahitaji
lazima uandikishe kwanza halafu ufanyike uhakiki wake, lakini muda huo
hautoshi?
Kauli hiyo ya Profesa Lipumba kuhusu
kusimamishwa kwa kura ya maoni pia ilitolewa Februari 12 na viongozi wa
vyama 22 vya siasa walipokutana na NEC kujadili mchakato huo wa
uandikishaji kwa kutumia BVR.
Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema: “Mchakato huu ni muhimu na kama
hautafanyika vizuri tutaichafua nchi yetu. Wadau washirikishwe na
waridhike kwani kusipokuwa na uwazi kutaleta shida huko mbele.”
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe alisema: “Ilitakiwa kutuhusisha katika hili
mwanzo hadi mwisho. NEC wanatuonyesha hardware (vifaa vya kompyuta)
badala ya software (programu ya kompyuta) zinavyofanya kazi ambayo tuna
haja ya kuifahamu. Nani anatuuzia hizo hardware na nani anatuuzia
software hizo?”
Profesa Lipumba alisema: “Serikali
inatakiwa kujikita zaidi katika uandikishaji wapiga kura lakini Serikali
haina fedha, bajeti ya Sh144 bilioni haipo sasa itakuwaje tunaingia
katika kura ya maoni?
Mchakato wa Katiba
Kuhusu
mchakato wa Taifa kupata Katiba Mpya chini ya utawala wa Rais Jakaya
Kikwete, Profesa Lipumba alisema hakuna matumaini hayo na kinachofanyika
ni kutaka kuhalalisha utaratibu ambao haukuwa na uhalali kutoka kwa
wananchi.
Alisema Februari mwaka 2013 wakati Rais
Kikwete akizindua Vitambulisho vya Taifa, alisema vitambulisho hivyo
vingeweza kutumika pia katika kupiga kura lakini hakuna utaratibu wowote
uliotumika kuhakikisha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na NEC
wanashirikiana.
Profesa Lipumba alisema baadaye Jaji
Lubuva alinukuliwa akisema kazi ya uandikishaji itafanywa na tume yake
na si mtu yeyote kwani haiwahusu.
Alisema bajeti ya
mchakato huo ni Sh297 bilioni lakini alipotizama katika kasma ya tume
kulikuwa na Sh7.01 bilioni, fedha za maendeleo na fedha za tume
hazikuonekana.
“Ukienda kuchambua fedha ziko wapi
huzioni, mimi nikauliza mbona bajeti ni kubwa lakini haijulikani iko
wapi? Hata ukifanya ukaguzi unatakiwa kujua fedha hizo, katika maombi
yake Tume iliomba Sh144 bilioni kwa ajili ya Kura ya Maoni lakini nayo
haionekani katika vitabu vya Serikali sasa unajiuliza mchakato huo
utakwendaje na fedha zimekwenda wapi?” alihoji na kuongeza:
“Suala
la muda halitekelezeki, awali tume ilisema uandikishaji ungeanza
Septemba mwaka jana lakini ilishindwa, Desemba ikifanya majaribio ya
uandikishaji na katika Jimbo la Kawe wameandikisha wapiga kura kama
15,000 na ushee katika maeneo ya Bunju na Mbweni.
Walisema
wamevuka malengo lakini ukienda katika takwimu za Sensa za mwaka 2012
za Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) haziendani. Bunju wapo 51,000 lakini
hawa wameandikisha 15,000 wanasema wamevuka lengo sasa hapa kuna ukweli
wowote?”
“Makambako walisema wataandikisha wapiga kura
kama 31,000 lakini kwa Sensa ya mwaka 2012 ina wapiga kura zaidi ya
53,000 sasa utasemaje umevuka lengo na Jaji Lubuva alishatamka kwamba
daftari la mwaka 2010 limechakaa hivyo wakisema tutumie daftari hilo
haiwezekani.”