Jaji Lubuva: Hakuna Kura ya Maoni bila uandikishaji BVR kukamilika
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (Nec), Jaji mstaafu Damian
Lubuva amesisitiza kuwa Kura ya Maoni kwa Katiba Inayopendekezwa
haitafanyika mpaka uandikishaji watu katika Daftari la Kudumu la
Wapigakura kupitia mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR)
ukamilike.
Jaji Lubuva alisema hayo juzi katika
mahojiano maalumu na gazeti hili ofisini kwake, kwamba kwa sasa, Daftari
la Kudumu ndiyo kazi namba moja ndipo yafuate matukio ya Kura ya Maoni
ya Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi Mkuu.
Katika
msisitizo wake, Jaji Luvuba amewataka Watanzania kuondoa hofu kwamba
Kura ya Maoni huenda isifanyike Aprili 30, mwaka huu kama ilivyotangazwa
na Rais Jakaya Kikwete badala yake waweke imani kuwa tume hiyo
itajitahidi kukamilisha uandikishaji ndani ya muda uliopangwa.
“Tarehe
ile haijabadilishwa, iko palepale na siku zote nimekuwa nikisema kuwa
tutakamilisha ndani ya muda uliopangwa. Pia ikifika tarehe ya mwisho
bado hatujakamilisha shughuli hii tutawaambia,” alisema Jaji Lubuva.
“Sisi
tume hatutafanya Kura ya Maoni kama daftari halijakamilika. Ndiyo
kwanza tumeanza Njombe na baadaye tutaenda mikoa mingine tutakayotangaza
hapo baadaye; tukishindwa nitasema ile kazi yetu namba moja ya
uandikishaji sijakamilisha,” aliongeza.
Alisema
wanaongeza kasi ya uandikishaji mkoani Njombe, ambapo kuanzia leo
kutakuwa na mashine zote 250 za BVR zilizonunuliwa awali kwa ajili ya
majaribio katika baadhi ya majimbo matatu katika mikoa ya Dar es Salaam,
Katavi na Morogoro.
Kwa nyakati tofauti wadau
mbalimbali wa uchaguzi wameonyesha wasiwasi kuwa huenda tume hiyo
isikamilishe uandikishaji wapigakura ndani ya muda uliopangwa kutokana
na kasi ndogo ya uandikishaji na uchache wa mashine za BVR.
Jaji
Lubuva alisema kuwa Serikali imefanya malipo ya ununuzi wa mashine
7,750 hivi majuzi na kwamba kulingana na mchakato huo kuchelewa na
uingizaji nao umechelewa.
Kutokana na kuchelewa huko,
mashine hizo zitaingia ndani ya wiki mbili zijazo. Awali, Nec ilitarajia
mashine hizo zingeingia kati ya juma la kwanza au pili la Machi.
Kasi
ya ununuzi wa mashine hizo imekuwa ikusuasua kutokana na ukata wa fedha
ambapo awali mahitaji yalikuwa mashine 15,000 lakini zilishushwa hadi
10,500 na baadaye 8,500.
Kati ya hizo 8,500, mashine
500 kwa mujibu wa Lubuva zitaenda kwa Shirika la Vitambulisho vya Taifa
(Nida) kwa ajili ya uandikishaji Vitambulisho vya Taifa.