CCM na Chadema waikosoa taarifa ya Mdhibiti Mkuu wa Serikali
> Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Prof. Mussa Juma Assad.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chadema wamekosoa taarifa ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kupata hati zenye
mashaka na kueleza kuwa hesabu za vyama vyao zipo sahihi.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape
Nnauye na Mkurugenzi wa Fedha wa Chadema, Anthony Komu walidai taarifa
ya CAG ndiyo yenye upungufu.
Nape katika mahojiano
maalumu na waandishi wa habari yaliyorushwa moja kwa moja na kituo cha
Radio 5 Arusha alisema, kuna tatizo la kutokubaliana kutokana na ukaguzi
wa CAG.
Alisema mahesabu ya CCM yanayotokana na fedha
za ruzuku kutoka serikalini yapo sahihi lakini wana mgogoro na CAG
ambaye anataka mahesabu juu ya mali zote za CCM.“CCM ina miradi mingi
kwa mfano hapa Arusha tuna uwanja wa Sheikh Amri Abeid awali uwanja huu,
ulikuwa unasimamiwa na Mkoa wa Arusha pekee, sasa mkoa umegawanywa siyo
rahisi kuwa na mahesabu yote,” alisema.
Alisema kwa
maagizo ya CAG, kuandaa hesabu na taarifa za mali zote za CCM, inahitaji
kutumika kwa zaidi ya Sh1 bilioni jambo ambalo ni gumu.
“Sisi
tunadhani CAG anapaswa kukagua mahesabu ya fedha za ruzuku tunazopewa
na Serikali lakini siyo mahesabu ya mali zote za CCM,” alisema.
Kwa
mujibu wa taarifa ya CAG, ameainisha vigezo saba tofauti
vilivyosababisha hesabu za CCM kupata hati yenye mashaka na kueleza kuwa
CCM imekosa uhalali wa kisheria kumiliki baadhi ya mali ilizonazo.
Ukaguzi huo wa CAG umefanyika kwa mujibu wa Sheria namba
5 ya mwaka 1992 ya Vyama vya Siasa, iliyofanyiwa marekebisho na Sheria
namba 7 ya mwaka 2009, inayompa CAG mamlaka ya kukagua hesabu za vyama
vya siasa.
Ilibainisha vigezo vingine vya hati yenye
mashaka kuwa ni CCM kutowasilisha taarifa ya mapato yake ya fedha kutoka
kwa wafadhili mbalimbali zilizofikia Sh1,526,536,802, huku CAG pia
akishindwa kupata nyaraka za kuthibitisha matumizi na malipo
yaliyofanywa na chama hicho yanayofikia Sh6,045,438,052.
Kwa
upande wa Chadema, Komu alisema ripoti ya CAG ina upungufu kwani,
inataka chama hicho kuandaa taarifa za mahesabu na uthamini wa mali hadi
mikoani.
“Mapungufu (upungufu) ambayo alianisha ya
kutofanya uthamini wa mali zetu kutokuwa na mahesabu ya benki katika
ngazi mbalimbali na vitabu vya risiti kwa baadhi ya maeneo ni mambo
ambayo huwezi kuyakamilisha kutokana na mfumo wa vyama vyetu,” alisema.
Alikiri kuwa chama kuwa na akaunti nyingi kwa madai kuwa kila mkoa, wilaya na jimbo wana akauti yao.
Ripoti
ya CAG ilibaini kwamba Chadema ina zaidi ya akaunti 200 katika benki
mbalimbali nchini lakini fedha zilizotajwa kuwapo katika taarifa zake
kwa mwaka ulioishia Juni 2013 ni Sh224,824.750.56 kati ya hizo
Sh221,060,446.41 zikiwa ni salio katika akaunti zake sita na kuacha
salio la Sh3,764,304.15 kwa akaunti zaidi ya 194 zilizosalia.
Magari 10 yalinunuliwa kwa Sh559,031,330 bila kuidhinishwa Sh27,500,000 zilitumika kukodi jenereta bila kuwa na nyaraka.
Posted Sunday, March 22, 2015 | by- Musa Juma
Posted Sunday, March 22, 2015 | by- Musa Juma