Kikwete: Vyuo vikuu visitegemee wahadhiri ‘wazee’
Rais Jakaya Kikwete amevitaka vyuo vikuu nchini kuwaandaa vijana kuwa wahadhiri badala ya kutegemea wastaafu.
Kikwete
alisema hayo juzi usiku, katika harambee ya kuchangia fedha Chuo Kikuu
Kishiriki cha Tumaini (Tudarco) iliyofanyika katika ukumbi wa Diamond
Jubilee jijini Dar es Salaam ambapo Sh 1.6bilioni zilipatikana.
Alisema
kuwa vijana zaidi wanahitajika kutoa elimu katika vyuo vikuu nchini ili
kupunguza uhaba mkubwa wa wataalamu wa kada hiyo.
“Ajirini
wahadhiri wenye damu changa, tusiwategemee wastaafu peke yao kuwa
katika kada hii. Utegemezi wa wahadhiri wastaafu liwe jambo la mpito tu
katika vyuo vyenye sifa,” alisema Rais Kikwete.
Hata
hivyo, ushauri huo wa Rais Kikwete wa kutaka vyuo viajiri vijana zaidi
umepokewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wahadhiri. Mhadhiri wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Jamidu Katima, alisema suala hilo lina
sura mbili kwani wahadhiri wazee wamefanya mengi kama tafiti, machapisho
na wamekaa muda mrefu katika taaluma tofauti na wahadhiri vijana.
“Upande
wa pili ni kweli kuwa, ingawa wahadhiri wazee wamefanya mengi,
wahadhiri vijana nao wanahitajika ili kuziba mianya ya uhaba iliyopo,”
alisema Profesa Katima.
Alisema wakati mwingine vyuo huona gharama kubwa kusomesha vijana, badala yake huwatumia wahadhiri ambao tayari wamestaafu.
Kwa
upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Emmanuel
Malya alisema ingawa wahadhiri vijana ni wazuri, ni wachache hapa
nchini.
“Serikali iwekeze katika kuwasomesha maprofesa, ni
gharama lakini ni vizuri kwa sababu kuna uhaba mkubwa wa vijana katika
kada hii,” alisema Dk Malya.
Alisema ni vigumu kuwapata
wahadhiri vijana wenye shahada za uzamivu (PhD) na hata hao wenye
shahada moja ni wachache wenye alama nzuri zinazohitajika katika
kufundisha.
Mbali na ushauri huo, Rais Kikwete pia
amevitaka vyuo vikuu kuwa na vifaa vya kufundishia kozi mbalimbali huku
akisisitiza vyuo kuwa na vyanzo vingine vya mapato badala ya kutegemea
ada za wanavyuo.
“Chuo kinatakiwa kijiendeshe chenyewe
na ada za wanafunzi ziwe tu sehemu ya mapato ambayo yataimarisha zaidi
chuo. Ni lazima kuwe na vyanzo vingine vya mapato zaidi ya ada,”alisema.
Kwa
upande wa mchango wa serikali katika elimu ya juu Kikwete alisema
serikali inatoa mikopo kwa wanafunzi wote kutoka shule binafsi na za
serikali, huku wale wa masomo ya sayansi wakipata kipaumbele zaidi.
“Serikali
inagharamia taasisi zote za elimu ya juu kwa kutoa mikopo kwa
wanafunzi. Wanapata mikopo wale wanaochukua masomo ya sanaa na sanaa ya
jamii,” alisema na kuongeza:
“Hatuna budi kuzalisha
wanasayansi wa ndani, tukitegemea wanasayansi kutoka nje, tutaaibika kwa
sababu usipofuata masharti yao tu, wanaondoa misaada yao.”
Aidha,
Rais Kikwete alisifu Tudarco kuwa kimekuwa mfano mzuri katika masuala
ya nidhamu tangu kuanzishwa kwake na kimeshajijengea sifa kubwa nchini.