Mbaroni kwa kukutwa na mifupa ya albino
Polisi mkoani Kagera wamedai kuwakamata watuhumiwa wawili
wakiwa na mifupa inayodhamiwa kuwa ya binadamu mwenye ulemavu wa ngozi
(albino), aliyefariki mwaka 2006 wa Kijiji cha Rushwa wilayani Muleba.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe, alisema watuhumiwa wote ni
wakazi wa Kijiji cha Kyota wilayani Muleba na kwamba walipata mifupa
hiyo kwa msaada wa mganga wa jadi.
Alisema watuhumiwa
walikamatwa na mfupa mmoja na baada ya kupekuliwa zaidi katika nyumba
yao walikutwa na mifupa mingine miwili na walipohojiwa wanadaiwa kukiri
kuwa ilikuwa ya albino.
“Walifukua kaburi mwaka 2008 kwa maelekezo ya mganga wa jadi,” alisema Mwaibambe.
Alieleza
kuwa watuhumiwa walifukua kaburi la Zeuria Justus aliyefariki mwaka huo
katika Kijiji cha Rushwa, Kata ya Mushabago, kazi iliyofanyika 2008 kwa
maelekezo ya mganga wa jadi.
Kwa mujibu wa Mwaibambe,
Zeuria alikufa muda mfupi baada ya kujifungua na polisi walilazimika
kufukua kaburi hilo baada ya kupata kibali cha mahakama na kukuta baadhi
ya viungo vimeondolewa.
Hata hivyo, Mwaibambe alisema
mganga wa jadi ametoroka na anasakwa na polisi, huku watuhumiwa
wakitarajiwa kufikishwa mahakamani. Majibu zaidi ya uchunguzi wa viungo
hivyo yanasubiriwa kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
Sangoma walaani wenzao
Waganga
wa jadi mkoani Tabora, wamelaani wenzao wanaojishughulisha na kupiga
ramli chonganishi kuwadanganya wateja wao kuwa viungo vya binadamu
vinaleta utajiri.
Mwenyekiti wa Chama cha Waganga wa
Jadi (Chawatiata) Mkoa wa Tabora, Yasin Mwarabu akitoa tamko la waganga
hao alilaani baadhi ya wenzao wanaojihusisha na imani potofu kuwa,
viungo vya binadamu vinaleta utajiri na kushiriki kupiga ramli
chonganishi zinazosababisha mauaji.
Mwarabu alisema
kama chama wanaungana na Serikali kwa jitihada zake za kuwabaini waganga
matapeli na watashirikiana kukemea kwa nguvu zote.
“Kazi
ya uganga ni kutibu siyo kuua, hivyo kama wapo wanaoua hao siyo wenzetu
na kamwe hatuwahitaji kwa vile wanatuharibia,” alisema.
Hivi
karibuni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda alikutana na
waganga wa jadi na kuwataka kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili na
sheria za nchi.
Watoa onyo
Msako
wa kukamata wapiga ramli chonganishi ukiwa unaendelea nchini, waganga
wa jadi wametoa onyo kwa polisi kuhusu vifaa vinavyokamatwa wakati wa
msako huo. Askari walipewa tahadhari ya kukumbana na hatari yoyote
baadaye iwapo wataendelea kukamata vifaa hivyo vikiwamo vibuyu, vitambaa
vyeupe na vyeusi, ngawo, mikuki na shanga huku wakitakiwa kuvirejesha
mara moja.
Akizungumza na waganga wa jadi wa Wilaya ya
Bariadi, Mkoa wa Simiyu juzi, Katibu Mwenezi wa Chawatiata Mkoa wa
Mwanza, Stephen Sebastian alisema kukamata vifaa hivyo ni kitendo cha
hatari.
Sebastian alikuwa akizungumza mbele ya Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo na kusema kitendo kinachofanywa
na polisi kukamata vifaa hivyo kinaweza kusababisha hali ya migogoro
mikubwa kati ya polisi na jamii.
“Nitoe tahadhari mbele
yako mkuu wa polisi, msako huu unaoendelea umelenga kusambaratisha jadi
wakati ndizo zilizotumika kuleta uhuru, vifaa hivi vinavyokamatwa
virejeshwe mara moja, wazee hawa wakikasirika hakuna atakayebaki ndani
ya polisi, msitake kugombana na mila gombana na wanaopiga ramli
chonganishi, lakini chondechonde rejesheni vibuyu vyetu haraka,”
alisema.
Sebastian alidai wazee hao wanaweza kukasirika
wakati wowote kuanzia sasa iwapo vibuyu vyao vitaendelea kukamatwa,
huku vingine vikiwa havirejeshwi kwa wamiliki walioachiwa.
Naye
Mkumbo alikanusha kwamba waganga wa jadi wanaonewa au kusingiziwa kuwa
wanapiga ramli chonganishi, kwani kwa uchunguzi wao wamebainika ndiyo
chanzo kikuu cha mauaji ya albino na vikongwe.
Mkumbo
aliwataka waganga hao kuacha vitendo hivyo, huku akiwaelekeza ndani ya
mwezi mmoja kila mganga awe amepata leseni au kujiandikisha kwa viongozi
wake wa kijiji au mtaa ili kuweza kukwepa msako mkali utakaoanza.
Katika
hatua nyingine, waganga hao walifanya uchaguzi katika mkutano huo na
kumchagua Mayunga Kidoyai kuwa Mwenyekiti wao, Shinyanga Isamila (Makamu
Mwenyekiti), Njile Kasula (Katibu) na John Kunini (Katibu Msaidizi).
Imeandikwa na Phinias Bashaya (Bukoba), Robert Kakwesi (Tabora) na Faustine Fabian (Bariadi)