Chadema yatetea wanahabari

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeungana na wadau wa sekta ya habari nchini kupinga usiri na udharura unaotaka kufanywa na Serikali katika miswada miwili muhimu inayogusa masilahi ya mwananchi mmoja mmoja na makundi ya wadau mbalimbali katika jamii.
Kwa mujibu wa tarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya chama hicho, Tumaini Makene ameeleza kuwa kwa takriban wiki moja sasa zipo taarifa (za uhakika) kwamba Serikali inapanga kuwasilisha bungeni kwa hati ya dharura miswada miwili; Muswada wa Sheria ya Kupata Habari wa Mwaka 2015 na Muswada wa Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari wa Mwaka 2015.
“Usiri na udharura huu kwenye jambo linalogusa haki za Watanzania halikubaliki. Tunatumia fursa hii kuungana na wadau mbalimbali wa habari nchini kupinga mipango hiyo ya Serikali kutaka kulitumia Bunge kupitisha miswada hiyo kisha kutunga sheria bila kutoa fursa kwa wadau kutoa maoni yao ili kuboresha miswada hiyo,”alisema Makene katika tarifa hiyo.
Alisema haki ya wananchi kupata taarifa na uhuru wa vyombo vya habari mbali ya kugusa haki za mtu mmoja mmoja na makundi ya kijamii kitaaluma na kikazi, ni moja ya misingi muhimu kwa Taifa lolote ambalo linataka kuweka mifumo na taasisi imara kwa ajili ya maendeleo ya demokrasia na ustawi wa jamii.
Makene alisema Chadema, kikiwa taasisi ya kisiasa iliyotia saini Azimio la Dar es Salaam la Uhuru wa Uhariri na Uwajibikaji, kikiamini katika uwajibikaji lakini pia dhana kwamba wadau wa habari ni pamoja na vyama vya siasa na makundi mengine katika jamii, kinapinga vikali hatua hiyo ya Serikali kutumia hati ya dharura kuwasilisha jambo linalohitaji maoni ya wananchi kwanza.
Taarifa hiyo ya Chadema inaunga mkono tamko lililotolewa katikati ya wiki na wadau mbalimbali wa vyombo vya habari nchini wakipinga hatua ya Serikali kutaka kuwasilisha miswada hiyo miwili kwa hati ya dharura jambo ambalo halitatoa nafasi kwa wadau kutoa maoni yao.Katika taarifa ya Chadema jana, Makene ameleza kuwa, “Serikali hii ambayo imekuwa na tabia ya kuhalalisha ukandamizaji wa uhuru wa maoni na vyombo vya habari (mathalan kufungia magazeti ya Mwanahalisi, The East African) haiwezi kuaminika kupeleka muswada kwa ajili ya Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari, kwa usiri siri na udharura wa kutengenezwa.”
Alisema usiri huo na udharura unaotaka kutumika kupitisha sheria bila maoni ya wananchi ni mwendelezo wa kukosekana kwa nia njema ya Serikali dhidi ya wadau wa uhuru wa habari nchini ambao itakumbukwa wamekuwa wakipigania kuwapo kwa sheria hizo kwa takriban miaka 10 sasa.
Juzi, jopo la wadau wa habari kutoka asasi, taasisi na vyombo vya habari nchini, lilipanga kuwatumia wabunge kuwashawishi wakatae kupitisha muswada wa sheria ya habari uliopangwa kuwasilishwa bungeni kwa hati ya dharura.
ADVERTISEMENT
Hatua hiyo inatokana na mipango ya Bunge hilo kuweka ratiba ya uwasilishaji wa miswada miwili ya habari kwa njia ya hati ya dharura, huku utata ukiibuka kutokana na usiri uliopo ndani ya miswada hiyo.
Katika mkutano kati ya wadau hao na waandishi wa habari, walisema lengo la kutoa tamko hilo ni kulitaka Bunge kusitisha uwasilishaji wa miswada hiyo kwa utaratibu wa hati ya dharura ili kutoa fursa kwa wadau na wananchi kuiona miswada, kuisoma, kuichambua na kutoa maoni yao.
Walioshiriki kuandaa tamko hilo ni wadau kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT), Sahara Media Group, Policy Forum, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Kampuni ya The Guardian, Mwananchi Communications Ltd, Free Media Ltd, Hali Halisi Publishers, Taasisi ya Twaweza, Mfuko wa Vyombo vya Habari (TMF), Tanzania Citizens’ Information Bureau na Shirika la Sikika.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania Bara (Jukata), Deus Kibamba alisema wadau wa habari wanaamini kuwa Serikali na Bunge hawatakuwa tayari kupokea lawama za wananchi kwa upitishaji wa miswada hiyo bila kufuata utaratibu wa kawaida.
“Hatutegemei kuona Serikali ikipuuza tamko hili ila inawezekana tukachukua hatua nyingine, endapo itashindika kwa njia hii ya tamko,” alisema.
Mkurugenzi wa Shirika la Sikika, Irinei Kiria alisema: “Hatuamini kama Serikali iko tayari kuona ikichonganishwa na wananchi kwa sababu ya miswada hiyo, wabunge wetu pia hatuamini kama watakubali kuona miswada hiyo ikipitishwa kwa hati ya dharura bila kushirikisha wadau.
“Miswada hiyo haiwahusu wanahabari pekee, bali hata wadau wengine, hata CCM hatuamini kama inaweza kukubaliana na upitishwaji wa miswada hiyo kwa usiri usiojulikana kwa wahusika.”
Akijibu swali kuhusu athari za kutaka kukwamisha miswada hiyo, Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena alisema ni heri kuzuia kuliko kuruhusu miswada iliyojaa usiri.
Powered by Blogger.