Dk Kahangwa: Nitawania urais NCCR- Mageuzi
Majuma mawili tangu Umoja wa Vijana wa Chama cha
NCCR-Mageuzi umtake, Dk George Kahangwa (46) kugombea urais, mhadhiri
huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema ameridhia wito huo.
Machi
8, mwaka huu Kitengo cha Vijana cha NCCR - Mageuzi kilimpendekeza Dk
Kahangwa kugombea nafasi hiyo kwa kuwa kimeridhishwa na utendaji wake wa
kazi, ujana na ucha Mungu wake.
Akizungumzia
mapendekezo hayo mwishoni mwa wiki, Dk Kahangwa alisema: “Mwanzoni
yalikuwa mapendekezo tu ya vijana na mpaka sasa nilikuwa sijatoa kauli
rasmi, lakini baada ya kupata ushauri na kutafakari, nimeona sina
kikwazo katika jambo hilo.”
Msomi huyo wa masuala ya
elimu, alisema inawezekana akasita kwa kuwa jukumu hilo ni kubwa lakini
uungwaji mkono na hamasa anayopata na kauli wanazomwambia zinaonyesha
inawezekana na wanamwamini.
Vipaumbele vyake
Alitaja
vipaumbele vyake kuwa ni kuzalisha rasilimali watu bora, elimu isiyo na
ubaguzi, uchumi wa ushirika mamboleo utakaosisitiza kujitegemea na afya
bora wakati wote.
Pia, ujenzi wa miundombinu ya kuleta
maendeleo kwa kasi, demokrasia huru na ya kweli, umoja wa kitaifa na
michezo ambayo siyo tu itailetea sifa Tanzania, bali kutoa ajira kwa
vijana.
Alipoulizwa anaionaje changamoto ya uteuzi wa
wagombea ndani ya Ukawa, Dk Kahangwa alisema umoja huo utadumu iwapo
wataweka mbele masilahi ya Taifa na wananchi badala ya ubinafsi.
“Tunatambua
kugombea ni kushindana lakini tutangulize masilahi ya Taifa, masilahi
ya wananchi kabla ya masilahi ya chama kimoja ndani ya Ukawa,” alisema.
Sitishwi na umaarufu
Dk
Kahangwa alipuuza madai kwamba umaarufu wake ni mdogo na hivyo atakuwa
na wakati mgumu kupambana na wagombea wengine wa Ukawa na CCM ambao ama
wametajwa au kujitangaza wenyewe kuwania urais.
“Umaarufu
una sura nyingi; wapo wanaojulikana kwa mambo ya hasara ambayo hayana
msaada kwa Taifa. Unaweza usiwe na jina maarufu lakini una sifa za
uongozi na uadilifu, kwa hiyo sina hofu kupambanishwa na mgombea
mwingine yeyote ndani na nje ya Ukawa,” alisema.
Alitolea
mfano wa Rais, Benjamin Mkapa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed
Shein kuwa ni miongoni mwa watu ambao hawakuwa maarufu, lakini
walishinda uchaguzi.
Msimamo wa NCCR- Mageuzi
Katibu
Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema amefarijika kusikia Dk
Kahangwa amekubali kuwania nafasi hiyo akimtaja kuwa ni miongoni mwa
makada ambao ni nguzo ya chama hicho.
“Dk Kahangwa
hatujamwokota barabarani, ni mtu tunayemfahamu, kumheshimu na kuthamini
mchango wake ndani ya chama na yeye anakijua chama hiki vizuri,” alisema
Nyambabe.
Alipoulizwa anamlinganishaje Dk Kahangwa na
wagombea wengine kutoka vyama vinavyounda Ukawa na CCM, alisema: “Mimi
namtia moyo kwa sababu hata nikimlinganisha na wagombea wengine naona
anafaa zaidi. Kama hoja ya urais ni ujana, huyu ni kijana mwenzao na
kama hoja ni kwenda na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia, huyu ni
msomi aliyebobea.”
Alitoa wito kwa makada wengine wa
NCCR-Mageuzi kujitokeza kuchukua fomu ili kuleta ushindani wenye tija
ndani ya chama hicho. Dk Kahangwa ana Shahada ya Udaktari wa Falsafa
(PhD) katika masuala ya elimu.