Pengo atofautiana na maaskofu
Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo akibariki matoleo yakiotolewa na Umoja wa Wanawake wa katoriki(WAWATA), wakati wa Ibada iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis
Dar es Salaam: Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es
Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema waumini hawana budi
kusoma vizuri na kuelewa Katiba Inayopendekezwa ili wakati ukifika,
wafanbye uamuzi kwa hiari na utashi wao wakati wa kupiga Kura ya Maoni.
Ametoa
kauli hiyo ikiwa ni siku mbili baada ya Jukwaa la Wakristo kutoa tamko
linalowataka waumini kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari
la Wapigakura, kushiriki kikamilifu kwenye shughuli zote za elimu ya
Katiba Inayopendekezwa na kupiga kura ya “hapana” kuikataa Katiba
Inayopendekezwa.
Lakini jana, Kardinali Pengo alisema
kuisoma na kuielewa katiba hiyo ndiyo wajibu wa msingi ambao Wakristo
wanao kwa sasa ili kupiga kura inayostahili wakati ukifika. Kuhusu
maaskofu kuagiza waumini waikatae Katiba Inayopendekezwa, Kardinali
Pengo alisema wao wakiwa viongozi wa watu, hawana mamlaka wala uwezo
huo, bali wenye uwezo ni wananchi wenyewe.
Hata hivyo,
Kardinali Pengo alitaka tamko hilo lisambazwe kwenye parokia na vigango
vyote vya Jimbo Kuu la Dar es Salaam ili waumini wasomewe, wauelewe
kwanza, ili hatimaye waweze kufanya uamuzi sahihi wakielewa ni nini
wanachokitakiwa kukifanya.
Changamoto za familia
Katika
hatua nyingine, Kardinali Pengo pia alizungumzia changamoto za
wanandoa, ikiwamo tabia ya kuchepukia nje ya ndoa ambayo alisema
inasababisha amani kutoweka ndani ya familia.
Akizungumza
katika ibada ya Kwaresima kwa Wanawake Wakatoliki Tanzania (Wawata)
jana, Kardinali Pengo alisema akina mama wengi kwa sasa, hususan katika
ndoa wamekuwa wakisaliti ndoa na baadaye kuwatupia lawama watoto wao juu
ya tabia walizoanzisha wenyewe.
Katika mahubiri yake
aliyoyatoa katika Kanisa la Mt. Joseph Dar es Salaam, mbali na
changamoto sugu za kifamilia, Kardinali Pengo alijikita katika kuangalia
aina sita za malezi kwa watoto na athari za utandawazi kwenye jamii.
“Wapo
wanawake ambao kwa sasa wanaendekeza michepuko kwenye familia na
wamekuwa hawana hofu ya Mungu wakati wote. Kuna wengine ambao wanavaa
mavazi ya mabinti wakisema wanakwenda na wakati,” alisema.
“Wanawakemea watoto wao wakati wao wanaendekeza tabia chafu, wakiulizwa wanasema eti wao wameshakuwa watu wazima.”
Katika
sehemu ya mafundisho yake, mbali na kupungua uaminifu, Kardinali Pengo
alizitaja changamoto nyingine alizosema kuwa zimeendelea kuumiza familia
ambazo ni tofauti za kiimani, kipato, elimu, kulea watoto nje ya ndoa,
kushindwa kudhibiti maadili ya watoto, ushirikina na ufisadi.
Alisema changamoto hizo zinatafuna familia nyingi kwa sasa.
”Familia
inayokuwa inaendeshwa kwa imani tofauti za kidini ni changamoto kubwa
sana, amani inapungua ndani ya familia kwa hivyo tunahitaji kuwa makini
na changamoto hizo,” alisema Kardinali Pengo.