Mama Maria asema Makongoro ana haki kugombea urais
Mke wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Msasani jana, baada ya kuzushiwa kifo na watu wasiojulikana. Picha na Said Khamis
Dar es Salaam. Mke wa Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere amesema kuwa mtoto wake,
Makongoro Nyerere ana haki ya kugombea nafasi ya urais katika Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba.
Ijumaa wiki iliyopita, Makongoro
alilieleza gazeti hili kuwa uamuzi wake kuhusu kuwania kiti hicho
utajulikana mara kipenga kitakapopulizwa na CCM.
Kauli
ya Makongoro ilitokana na uvumi uliokuwa umeenea katika mitandao ya
kijamii kuwa mtoto huyo wa tano wa mwalimu Nyerere alikuwa anaandaliwa
na watu waliofanya kazi karibu na mwalimu awanie nafasi hiyo.
Akizungumza na waandishi ya habari nyumbani kwake Msasani jana, Mama Maria alisema mwanaye ana haki ya kugombea.
Mama
Maria aliyekuwa ameawaalika waandishi wa habari kuzungumzia uvumi
uliosambaa kuwa amefariki dunia, alitoa kauli hilo baada ya kuulizwa
kama uvumi huo unahusiana na habari kuwa mwanaye anataka kugombea urais.
Alisema,
“Hapana. Hayo mambo hayahusiani na mwanangu kutaka kuwania urais… yeye
ni raia wa Tanzania na hiyo ni haki yake ya msingi,”
Pia,
alidokeza kuwa wakati akizungumza na mwanaye mwingine juzi baada ya
uvumi wa kifo chake, naye alimwambia kuwa anataka kuwania nafasi hiyo.
Akitoa
ufafanuzi kuhusiana na uvumi huo alisema kuwa, taarifa za uvumi wa kifo
chake zilikuwa za furaha kwake na wala siyo za huzuni kama watu wengi
walivyodhania.
“Tumekuwa tukifanya maombi ya kusali na
kufunga kwa siku 40 kabla ya kipindi hiki cha Kwaresima kwa ajili ya
kuliombea taifa na dunia kwa ujumla. Na sasa tunafunga tena, hivyo
kwangu jambo hilo ni majibu ya maombi tunayofanya. Nimefurahia kwa
sababu naona maombi yanafanya kazi. Haya ni majibu, tunasema tumepita
mashetani,”alisema Mama Maria huku akitania kuwa karne hii ni ya kisasa
kweli, hata marehemu anaongea.
Aliongeza; “Baada ya
kupokea taarifa hizo, kwa kuwa nilikuwa nimelala nilichofanya niliamka
nikasali…nadhani Watanzania wanahitaji sana kusali, sala na kazi. Kama
Taifa pia tunahitaji kuwa na siku moja maalumu ya maombi.”
Licha
ya kusema kuwa taarifa hizo zilikuwa za furaha kwake, Mama Maria
alisema taarifa hizo zilizua hofu kubwa kwa familia yake na Taifa zima
kwa ujumla.
Alisema juzi mchana alianza kupokea simu kwa wingi tofauti na ilivyo kwa siku za kawaida.
Hata hivyo, alitoa angalizo kuwa huenda uvumi huo ukawa unahusiana na harakati za Uchaguzi Mkuu ujao.