KUELEKEA MAJIMBONI 2015 : CCM ijihadhari majimbo ya Mbarali, Mbozi Magharibi na Mbozi Mashariki
Julius Mtatiro
(Julius
Mtatiro ni kiongozi mzoefu katika siasa. Ana shahada ya Uzamili ya
Utawala na Uongozi (M.A), na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (L LB):
Jimbo la Mbarali
Jimbo la
Mbarali kama yalivyo mengine lilianza siasa za vyama vingi mwaka 1995
kwa ushawishi wa kipekee kutoka kwa vyama mbalimbali, huku NCCR Mageuzi
ikionyesha kila aina ya makeke.
CCM haikuwa na hofu na
ilimtumia kiongozi mzoefu wa kijeshi, Kanali Mstaafu Edmund Mjengwa
ambaye hakufanya ajizi, aliwashinda wapinzani na kutunza heshima ya CCM
hapa Mbarali. Kanali Mjengwa aliongoza kipindi kimoja, 1995 -2000.
Mwaka
2000 katika Uchaguzi Mkuu, CCM ilibadilisha ladha na kumleta mwanamama.
Huyu ni mtaalamu wa masuala ya uhasibu, Estherina Kilasi.
Estherina
alivaa viatu vya kanali mstaafu kwenye kampeni na ni kama alijengewa
ujasiri wa kijeshi, hakuwaogopa wanaume na akasaidiwa na mtandao wa CCM
ambao kipindi cha nyuma ulikuwa na maana ya ushindi.
Alitangazwa mshindi na akafanikiwa kuongoza Jimbo la Mbarali kwa kipindi cha kwanza mwaka 2000 – 2005.
Mwaka
2005 unakumbukwa kwa kimbunga cha Kikwete pamoja na matokeo yenye utata
kwa maana ya upigaji kura uliokuwa umepitiliza, (siku za mbele katika
uchambuzi wa masuala ya siasa tutakuja kuongelea masuala ya kushuka na
kupanda kwa upigaji kura ambako kunatia shaka).
Wapigakura
walijitokeza kwelikweli na kazi kubwa ikafanywa na wagombea huku CCM
wakimpa nafasi mwanamama Estherina ambaye alikuwa ameongoza kipindi
kimoja.
Vyama vya CUF na TLP vilikuwa na nguvu jimboni humu na kufanikiwa kuweka wagombea, ule utitiri wa vyama wa mwaka 1995 ulipotea.
Filimbi
ya upigaji kura ilipopulizwa na matokeo kutangazwa, mwanamama Estherina
aliwabwaga wagombea wa TLP na CUF. Estherina alipata kura 52,713
akifuatiwa na Pwilla Getrudi Jacob wa TLP kura 10,168 na Kharid Shaweji
wa CUF kura 6,912.
Kwa jumla vyama vya upinzani
vilijitahidi lakini viliangushwa na dhana ya ushindi wa kimbunga wa CCM
katika kila kona ya nchi. Bi Estherina akawa na ridhaa mkononi na akawa
mtumishi wa wananchi hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010 ulifika huku vyama vikiwa vimejiimarisha na CCM ikiendelea kutumia juhudi za mtandao wake.
Wananchi
wa Mbarali hawakuwa na kumbukumbu nzuri sana na mbunge aliyemaliza muda
wake, kwa sababu hakufanya vizuri katika kipindi cha miaka 10 na
Chadema iliitumia nafasi hiyo kujipanga.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliporuhusu vyama kujitosa kwenye uchaguzi vilipatikana vyama vitano.
Kampeni
zilionyesha dalili ya ushindani wa wazi kati ya Chadema na CCM ambapo
vyama hivi viwili vilileta wagombea wapya, huku TLP ikimleta mgombea
yuleyule aliyesimama mwaka 2005.
Mgombea mpya wa CCM
Modestus Kilufi alipata kura 34,869 na alifukuzwa bila mafanikio na
Jidawaya Kazamoyo wa Chadema kura 16,090.
Wagombea wengine watatu akiwemo wa TLP waliambulia asilimia moja ya kura zote.
Kama
yalivyokuwa maeneo mengi ya nchi, siasa za Mbarali zilitawaliwa na
Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na jambo hilo lilikuwa na
maana kubwa wakati nchi inaelekea katika uchaguzi wa mwaka huu.
Hata
hivyo, safari ya kiushindani jimboni Mbarali haiwezi kupita bila
kupimwa kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, japokuwa watu wengi huhoji
kigezo hiki kutokuwa na maana pale ambapo tathmini za ubunge
zinafanyika.
Kigezo hiki kina maana kubwa mahali ambapo vyama vinachomoza na vinaweza kufanya lolote.
Uchaguzi
huu unasaidia kujenga mtandao wa ushindi wa chama kwenye uchaguzi
mkubwa na wakati mwingine unaweza usisaidie ikiwa chama chenye mtandao
huo kitaweka mgombea asiye na sifa.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwezi Desemba mwaka jana uliipatia Chadema vijiji 18 kati ya 102 na vitongoji 121 kati 713.
Matokeo
haya siyo kipimo kizuri kwa Chadema kuelekea uchaguzi wa mwaka huu na
kuipatia Ukawa ushindi, lakini ikumbukwe kuwa Chadema iliweza kupata
asilimia 30 ya kura za ubunge mwaka 2010 kwenye jimbo hili bila kuwa na
hata asilimia 2 ya vijiji na vitongoji.
Hali hiyo ina
maana kuwa mipango ya Chadema kulitwaa Jimbo la Mbarali ikiwa itaweka
mgombea anayekubalika itakuwa kwenye njia sahihi na haitakwazwa na
matokeo haya ya serikali za mitaa. Lakini ikiweka mgombea dhaifu, CCM
watafanya sherehe.
Jimbo la Mbozi Magharibi
Mwaka
1995 Mbozi Magharibi ilianza safari ya siasa za vyama vingi kwa cheche
za hali ya juu. NCCR Mageuzi ilitisha na kujipanga kimtandao lakini
haikufua dafu kwa CCM.
CCM ikiwakilishwa na Eliachim
Simpasa ilifanya vyema na mwakilishi huyo akawa mbunge wa kwanza wa
jimbo hili chini ya mfumo mpya wa ushindani wa vyama.
Mwaka
2000 wakati NCCR Mageuzi inasambaratika vyama vingine vikianza
kuchomoza zaidi, CCM haikusita kumrejesha Simpasa ambaye kitaaluma ni
mwalimu mwenye shahada ya elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Enzi za Simpassa zilikoma baada ya kipindi hiki cha pili cha uongozi na mwaka 2005 kulikuwa na habari mpya zaidi.
Habari
inayosemwa kuwa mpya mwaka 2005 ni kuletwa kwa Dk Luka Siyame kuchukua
nafasi ya Simpasa ndani ya CCM. Siyame alishindana na Daniel Mwangamba
na Victor Sichone kutoka vyama vya CUF na TLP ambapo vyama hivi viwili
vilipata jumla ya kura 5,016 vikiiacha CCM na Siyame wakifurahi kwa
ushindi wa kura 44,781.
Dk Siyame ambaye ni msomi
mwenye shahada mbili za uzamili zote zikihusuutabibu alifanikiwa
kuongoza Jimbo la Mbozi Magharibi hadi mwaka 2010.
Ukuaji wa Chadema jimboni Mbozi Magharibi ulikuwa na hatari kwa ustawi wa CCM.
Silinde
David kijana machachari aliyekuwa katibu wa kitivo cha biashara Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (sasa Shule ya biashara) alifanya jitihada za
kufanya harakati za kiasiasa katika jimbo hili huku akiwa mwanafunzi
chuoni.
Nakumbuka wakati huo nikiwa waziri wa mikopo na
baadaye waziri mkuu wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo, Silinde
alinijia mara kwa mara akinijulisha kuwa atakuwa mbunge.
Sikuamini
haraka maneno hayo na nilijiuliza atakuwaje mbunge wakati uchaguzi
umekaribia na bado sisi tuko chuo! Silinde alionyesha kuwa makini na
kauli zake na mara nyingi alikuwa jimboni.
Juhudi za kijana huyu wa miaka 26 wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, zilizaa matunda.
Alimbwaga daktari mkongwe (Dk Siyame). Silinde alipata kura 20,835 dhidi ya kura 20,203) za Siyame wa CCM.
Mgombea wa CUF Asukile Kubango alipata asilimia 0.52 na hakuleta madhara yoyote kwa Silinde.
Matokeo
ya uchaguzi wa serikali za mitaa yanaonyesha kuimarika kwa Chadema.
Mwaka 2009 haikuwa na kitu cha kujivunia katika wilaya nzima ya Mbozi,
lakini kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Chadema kilipata vijiji 15
kati ya 125 vya wilaya nzima na pia ikipata vitongoji 149 kati ya 664
vya wilaya nzima.
Matokeo haya yana maana kuwa pamoja
na CCM kulipoteza Jimbo la Mbozi Magharibi mwaka 2010 pia imepoteza
asilimia 12 ya vijiji na asilimia 22 ya vitongoji mwaka 2014.
Hali
hii siyo ya kujivunia kwa CCM kwa hiyo bado Silinde ana nafasi kubwa ya
kupewa ridhaa kwa kipindi cha pili, na natambua kuwa CCM itakuwa inajua
kuwa kulirejesha jimbo hili hivi sasa ni sawa na “ngamia kupita kwenye
tundu la sindano”.
Jimbo la Mbozi Mashariki
Jimbo
hili lilianza harakati za vyama vingi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
1995, huku NCCR Mageuzi ikionekana kujijenga kiasi cha kutosha japokuwa
iko wazi kuwa vyama vyote vya upinzani vilikuwa vinasajiliwa wakati huo.
Kama
ilivyokuwa kwa majimbo mengi nchi nzima, CCM ilijiwekea kibindoni
ushindi mzuri, mbunge akiwa ni Edson Halinga na kuwa mbunge wa kwanza wa
wana Mbozi Mashariki katika mfumo wa vyama vingi.
Mwaka
2000, CCM ilimpa nafasi nyingine Halinga ambaye kitaaluma ni mwalimu
mwenye stashahada ya elimu, stashahada ya uchumi na sayansi ya siasa na
shahada ya elimu.
Aliingia kwenye kinyang’anyiro cha
pili na kuwaangusha wapinzani, jambo lililosababisha aongoze jimbo la
Mbozi Mashariki kwa kipindi cha pili. Lakini alipomaliza kipindi hiki
hakuwa na nafasi tena.
Mtanange wa kusaka ubunge nchi nzima kwa mwaka 2005 ulianza wakati CCM ilikuwa inajipanga upya.
Vyama
vya NCCR, CUF na TLP navyo vilionekana kujipanga huku ikionyesha kuwa
vina wagombea na mitandao dhaifu na kwa hiyo CCM ilikuwa na kazi rahisi
na ilimleta Godfrey Zambi ambaye alikuja na ule ushindi wa kimbunga wa
asilimia 89.0 kwa kupata kura 92,073.
Wagombea wengine
wa vyama vitatu waliambulia asilimia 11 ya kura zote. Zambi akaliongoza
Jimbo la Mbozi Mashariki kwa miaka mitano ya kwanza.
Mwaka
2010 haukuwa mzuri kwa CCM jimboni hapa. Umaarufu wa chama hicho
kikongwe ulishuka, huku mgombea wake akipoteza uungwaji mkono wa vijana.
CCM
ilimsimamisha tena Zambi ili atumie uzoefu wake na kufuta makosa yake
kukinusuru chama chake na huu ni wakati ambapo Chadema ilikuwa juu
ikiongozwa na kada kijana, Mtela Mwampamba ambaye wakati huo alikuwa
anatokea masomoni.
Mwampamba alikuwa na kila sababu za
kuongoza Jimbo la Mbozi Mashariki kwa kushinda uchaguzi wa mwaka 2010,
lakini wananchi wengi nilioongea nao (hasa vijana) wanasema kuwa kuna
wakati iliwalazimu hata kumchangia pesa za mafuta ya pikipiki na gari ya
kukodi.
Kwa kweli hakuwa na uwezo wa kiuchumi kukabili
ukubwa wa maeneo ya vijijini na inaonekana Chadema haikudhani jimbo
hili lilikuwa rahisi, kwa hivyo hakuwa amepata msaada wa kutosha katika
kampeni.
Udhaifu huo ulimwangusha. Zambi wa CCM
aliponea chupuchupu. Matokeo yalipotangazwa CCM ilisherehekea ushindi wa
kura 49,095 dhidi ya kura 31,997 za Mwampamba. CUF ilipata asilimia
1.01 ya kura zote na haikuwa tishio.
Kama Chadema
wangelijua umuhimu wa jimbo hili na kujipanga kulisukuma kimkakati huku
wakimpa Mwampamba nguvu, leo tungekuwa tunaongea mambo mengine.
Mara
nyingi vyama vya upinzani huwa na maeneo muhimu sana ya ushindi lakini
hupiga hesabu kimakosa na kujikuta maeneo hayo yanaangukia kwa chama
tawala hata kama yalikuwa “yameiva” kisiasa na yana wagombea wazuri.
Mwampamba baadaye alishajisalimisha CCM na kuwa kada wa chama hicho kinachoongoza dola.
Nadhani
alikosa umakini na uvumilivu ambao ungempa ushindi mkubwa katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kwani ni kijana mzuri na ana uwezo wa
kiuongozi.
Kuondoka kwake Chadema na kuhamia CCM kwa
sababu ya kutofautiana mitazamo na viongozi wake na kutazama kama
udhaifu kwa kijana huyu ambaye alipaswa kutambua kuwa maisha ya kisiasa
yana kupanda na kuteremka, hivyo alipaswa kuwa mtulivu. Sioni kama
atafanikiwa kisiasa ndani ya CCM.
Nimeongea na wana CCM
watatu jimboni Mbozi Mashariki na wanadai kuwa Godfrey Zambi ana nafasi
ndogo ya kurudishwa katika uchaguzi wa mwaka huu na chama chake (katika
kura ya maoni).
Arudi au asirudi, mtandao wa Chadema umeendelea kukua vizuri jimboni humu na panahitajika kumpata mgombea thabiti.
Maeneo
ya kata za mijini katika jimbo la Mbozi Mashariki wanamtambua vizuri
Mhandisi Msyette kwamba anaweza kulichukua jimbo hilo kwa tiketi ya
Chadema na Ukawa, lakini wanasema maeneo ya vijijini hajajiuza kwa
kiwango kikubwa.
Ni kazi kwa Chadema kujipanga katika
jimbo hili ambalo linahitaji kuongeza asilimia 20 tu ya ushindi na
kuongeza mbunge mwingine atakayeongeza changamoto za uwajibikaji na
demokrasia katika nchi yetu.
Jumamosi ya wiki hii
tutakamilisha uchambuzi wa Mkoa wa Mbeya kwa kuangazia majimbo ya Kyela,
Rungwe Magharibi na Rungwe Mashariki na kisha kesho yake Jumapili
tutahamia Mkoa wa Katavi na kudadavua majimbo yake yote.