Siasa bila dini ni uendawazimu


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza katika kikao cha mashauriano cha viongozi wa dini kilichofanyika Febuari mwaka huu.
Historia ya siasa duniani haitengani kwa kiwango kikubwa na historia ya dini. Vitu hivi viwili kwa maisha ya mwanadamu vimekuwa sambamba na vyenye mafanikio kwa jamii yoyote ile duniani. Kwa upande mwingine dini na siasa vimeleta matatizo makubwa duniani.
Tusipojenga uhusiano mzuri kati ya siasa na dini katika dunia na nchi yetu, tutaendelea kushuhudia machafuko na uharibifu mkubwa wa mali pamoja na mauti dhidi ya binadamu kama yalivyowahi kutokea hapa nchini hasa katika kampeni za kisiasa. Mara nyingi maovu hayo yanasababishwa na uelewa mdogo juu ya uhusiano wa siasa na dini.
Hivi sasa Tanzania imezalisha ugonjwa mpya unaojulikana kwa jina la ‘udini.’ Unapoanza kuingiza udini katika ajira, elimu, afya na siasa ujue kwamba usalama wa nchi upo hatarini.
Kutenganisha kabisa siasa na dini ni kitu kisichowezekana katika dunia ya leo. Ndiyo maana ninaandika kwamba “siasa bila dini ni uendawazimu”.
Uendawazimu
Huwezi kusema wewe unashughulika na siasa halafu ukajidanganya kwamba huhusiki na masuala ya dini, wananchi wengi ni waumini wa madhehebu mbalimbali. Mathalan, Tanzania kuna Waislamu, Wakristo, Wabudha, Wahindu na hata wapagani.
Siasa ambayo haigusi maisha ya waumini inakuwa imejitenga na jamii husika. Kitu muhimu na kinachotakiwa ni kujenga uhusiano mzuri kati ya nyanja hizi mbili bila upotofu.
Katika siasa za Tanzania, nimegundua kwamba kelele za muda mrefu zinazotolewa na Serikali na wanasiasa kuwataka viongozi wa kiroho au wa dini wasichanganye dini na siasa hazina msingi wowote ule kwa vile mambo hayo mawili hayawezikutenganishwa kabisa.
Wanaoshikilia msimamo huo wanaonyesha woga wao juu na uelewa finyu katika masuala ya dini na siasa, hii ni bahati mbaya.
Yesu Kristo hakuhubiri habari za ufalme wa Mungu pekee na kuacha dhambi, bali aligusa masuala ya jamii kama amani, umaskini, kutenda haki, uhusiano mzuri, madhara ya rushwa na ufisadi, wizi wa mali ya umma, utuanzaji wa rasilimali na hata kuponya magonjwa. Na hii ndiyo injili sahihi, yaani injili ya jamii.
Yesu alikuwa akihubiri injili ya jamii, je, sisi sasa hatupaswi kuihubiri injili hiyo? Nini msingi wa hofu ya viongozi wa Serikali na wanasiasa kwa viongozi wa kiroho kuongelea masuala ya kisiasa katika nyumba za ibada?
Kanisa Katoliki lilitoa msimamo wake kuhusiana na kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa; Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania kupitia kwa Tume ya Haki na Amani kwa ushirikiana na CPT, wametoa waraka au tamko ikipendekeza kusitishwa kwa mchakato wa Kura ya Maoni ili kupisha maandalizi mazuri ya Uchaguzi Mkuu. Je, hapo kanisa limefanya siasa?
Ni wajibu wa kanisa kama chombo cha wokovu wa wanadamu wote, na kiongozi wa imani na jamii kufanya kazi yake hii ya kinabii. Sura ya nne ya ujumbe wa maaskofu Katoliki wa Kwaresima, unaongelea wajibu wa kijamii wa kanisa.
Sehemu moja ya ujumbe huo inasema: “Kila mara kanisa linapotimiza wajibu huu, linashutumiwa kuingilia siasa. Tafsiri hiyo ni potofu.”
Kamwe Kanisa Katoliki haliwezi kukaa pembeni, kwani litakuwa linafanya dhambi ya kutotimiza wajibu kwa jamii. Injili ya Yesu ambayo ni ya upendo, amani na umoja lazima ihubiriwe kwa kila mtu katika jamii husika. Kwa mfano, Yesu anafundisha tuache “siasa za jino kwa jino”.
Katika ujumbe huu wa Kwaresima, Mwalimu Julius Nyerere amenukuliwa kuwa aliwahi kuliasa kanisa akisema: “Iwapo kanisa halitashiriki kwa vitendo katika maasi dhidi ya mifumo dhalimu ya kiuchumi inayosababisha watu kutoswa katika fedheha ya umaskini na kudhalilishwa, kanisa halitakuwa na maana yoyote kwa watu na dini ya Kikristo itapoteza mvuto na kuwa kama ushirikina. Jambo hili likitokea, kanisa litakufa.”
Katika jamii ya Kiyahudi enzi za kale, manabii walikuwa wanaishi ikulu pamoja na Mfalme kwa lengo la kumsaidia katika kazi yake ya kuongoza jamii.
Ni nabii aliyekuwa anampaka mafuta Mfalme ili mkono wa Mungu, nguvu, na hekima iwe naye katika kazi yake ya kuhudumia jamii nzima bila ubaguzi.
Tanzania na manabii
Tanzania ya leo inahitaji manabii kama alivyojitokeza Mwalimu Nyerere. Pia ni wajibu mkuu wa viongozi wa dini kuwasaidia viongozi wa Serikali na wanasiasa ili waweze kuwa na “ roho ya Mungu’ katika uongozi wao. Ndiyo maana nasema siasa bila dini ni uenda wazimu.
Ikumbukwe kuwa enzi za kale wakati wa uteuzi wa kiongozi wa jamii, mtu aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo mara nyingi alikuwa ni yule aliyeonekana mtiifu wa kiwango cha juu kwa Mungu na watu waliamini ataweza kuongoza vyema kwa sababu “sauti ya Mungu ilikuwa ndani yake”.
Kuipotosha jamii kwamba viongozi wa dini hawana uhusiano na mambo ya kisiasa ni kutowatendea haki. Lazima tutambue kwamba viongozi wa dini ni viongozi wa jamii pia.
Napenda kujua je, mpaka wa dini na siasa uko wapi? Inakuwaje wananchi wanaohutubiwa katika mikutano ya kisiasa majukwaani, haohao siku ya ibada wanakuwa waumini wetu?
Kuwatenganisha viongozi wa dini na siasa ni kutaka kujenga chuki kati ya waumini na viongozi wao.
Napendekeza kwamba viongozi wa Serikali na wanasiasa wa vyama vyote, lazima waepuke kuwapotosha waumini na kuwajengea chuki na viongozi wa madhehebu yao. Mungu ibariki Tanzania na watu wake.
Powered by Blogger.