Bila ya umoja wa kitaifa tunaelekea kubaya


Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na viongozi wa kidini alipowasili katika kongamano la viongozi wa dini jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Kwa hali ilivyo Tanzania inahitaji chombo cha kujenga umoja. Lakini kisiwe chini ya vyama vya siasa, dini, ukanda wala ukabila.
Hakuna taifa linaloweza kusimama bila ya kuwa na umoja. Tanzania imesimama imara hadi leo hii kwa sababu ya umoja wa kitaifa uliojengwa na waasisi.
Tunasifiwa kwa utulivu na amani. Sifa hizi ni za kweli na kilichotufikisha hapa tulipo ni umoja. Hili halikunyesha kama mvua, bali ni jambo lililofanyiwa kazi usiku na mchana.
Waasisi wa Taifa letu walijitahidi kuujenga umoja huu. Kuna mambo mengi yaliyowasaidia kuujenga kama vile kuwa na chama kimoja cha siasa. Chama kilitunga sera na kutoa mwelekeo. Hivyo chama kilikuwa ni chombo kimojawapo cha kuujenga umoja wa Taifa.
Ingawa kulikuwa na watu wachache walioupinga mfumo wa chama kimoja, hawakuwa tishio la kuuvunja umoja wetu. Walikuwa wapinzani wenye kulenga kujenga umoja wa kitaifa.
Waasisi wa Taifa letu hawakuzitanguliza dini zao, jambo la kuabudu lilibakia kuwa la mtu binafsi. Watanzania walikuwa na dini, lakini Tanzania haikuwa na dini; haikutawaliwa kidini.
Jambo hili lilionekana wazi katika Katiba ya nchi yetu. Mwalimu Nyerere alikuwa mcha Mungu na Mkatoliki hodari, lakini hakuthubutu kujenga nyumba ya ibada ndani ya Ikulu.
Ukabila ulipigwa vita na utawala wa machifu ulifutiliwa mbali. Lugha ya Kiswahili ilipewa kipaumbele na kuwa chombo cha kuwaunganisha Watanzania wote.
Nchi zinazotumia lugha za kigeni kama lugha zao za kitaifa hadi leo zinapata shida ya kujenga umoja wa kitaifa.
Kwa mfano, nchini Uganda, taarifa ya habari ili iwafikie wanachi wote inatangazwa kwa lugha zaidi ya sita!
Jeshi la Kujenga Taifa
Jeshi la Kujenga Taifa lilianzishwa kwa lengo la kuwakutanisha vijana waliomaliza kidato cha sita na vyuo.
Kipindi chote cha mafunzo ya vijana hawa, uzalendo na umoja wa kitaifa ni mambo yaliyosisitizwa.
Mfumo huu ulipunguza kasi ya ukabila, ukanda, majivuno na kiburi. Jeshi liliwatendea vijana wote sawa, bila ya kujali mtoto wa tajiri, kiongozi na mtoto wa maskini, wasichana wala wavulana.
Mfumo wa elimu wa kuwasambaza vijana kwenye shule mbali mbali za mikoa ya Tanzania, ulisaidia kuwakutanisha vijana na kujenga umoja wa kitaifa.
Vijana kutoka Kagera, walipelekwa kusoma Mtwara, Moshi au Dar es Salaam. Wa Kigoma, walipelekwa Arusha, Kagera, Musoma au Dodoma.
Mwenge wa Uhuru ulibuniwa kwa malengo ya kujenga umoja wa kitaifa. Mbio za kuuzungusha Tanzania nzima zilichochea cheche za umoja wa kitaifa.
Mfumo wa vyama vingi
Mwaka 1995, Tanzania ilijiingiza katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Tunayoyashuhudia sasa, hakuna chama kinachoonyesha sera ya kujenga umoja wa kitaifa.
Wapinzani wa leo ni tofauti kabisa na wapinzani wa zamani wakati wa utawala wa chama kimoja. Wapinzani wa leo pamoja na chama tawala, wanaangalia zaidi umoja wa vyama vyao kuliko umoja wa kitaifa. Wanatanguliza mbele ari ya kuingia Ikulu, ruzuku, mbwembwe za madaraka na ushindani wa chuki na utengano.
Wakati wanasiasa wa zamani walikuwa na sera ya uhuru na umoja, wanasiasa wetu wa leo wana sera ya ukoloni mambo leo (Utandawazi, ubinafsishaji, soko huria) na utengano.
Baadhi ya vigogo wa CCM wanasema ni lazima kitangulizwe chama. Wakati tunalilia umoja wa kitaifa, wao wanalilia umoja wa chama chao. Hivyo kwao jambo la muhimu ni kutanguliza chama.
Mfumo wa elimu umevurugika, shule nyingi za binafsi na sekondari za kata zimeanzishwa na kuchochea watoto wengi wasiweze kuivuka mikoa yao. Watoto wa matajiri hawasomi tena na watoto wa maskini
Kiwango cha elimu kimeanza kutofautiana na kuleta hatari ya kuanza kuunda matabaka katika taifa. Tabaka ni adui mkubwa wa umoja na amani. Baadhi ya watoto wameanza kuvuka mipaka ya nchi na kusomea Uganda, Kenya na nchi nyingine jirani kama Zambia na Malawi.
Mfumo uliokuwa umejengwa na waasisi wa kuunda umoja wa kitaifa umeaanza kupotea. Ni wajibu wa kila Mtanzania kujiuliza: Ni nani adui wa umoja wetu?
Adui wa umoja wetu
Kama nilivyosema hapo juu, ni vigumu taifa lolote kusimama bila ya umoja. Kama tunataka Taifa liendelee kusimama, lazima tukazane kujenga umoja.
Tukigundua adui wa umoja wetu ni lazima tumpige vita kwa nguvu zetu zote. Kati ya mambo ambayo yanaonyesha dalili za kutishia uhai wa umoja wetu ni dini! Na hasa hizi dini mbili kubwa za Uislamu na Ukristu.
Kila tunapoingia kwenye mchakato wa Uchaguzi Mkuu, Waislamu wanamtaka rais Mwislamu na Wakristu wanamtaka rais Mkristo. Maoni haya yanafunika hekima na busara yote.
Siyo uwezo wa mtu na wala siyo mapenzi ya mtu katika taifa lake. Jambo muhimu ni dini! Haya siyo maoni ya kujenga umoja na wala haya siyo mawazo ya waasisi wa Taifa letu.
Watanzania wengi wamejiingiza kwenye dini hizi mbili. Ni vigumu kuwaambia wazikimbie maana zinahatarisha umoja wa Taifa letu.
Ushauri wa pekee ni kuzilazimisha dini hizi zikakubali utamaduni wetu.
Waasisi wa Taifa letu walitujengea utamaduni wa umoja, utulivu na amani, hivyo ni lazima dini zetu ziheshimu utamaduni huu. Mtanzania Mwislamu ni Mtanzania, na ni lazima apate haki zote za Mtanzania.
Aheshimiwe na Watanzania wote kufuatana na karama zake alizonazo na mchango wake kwa Taifa.
Mtanzania Mkristo ni Mtanzania na ni lazima apate haki zote za Mtanzania, aheshimiwe na Watanzania wote kufuatana na karama zake na mchango wake kwa Taifa letu.
Mtanzania anayefuata dini za jadi ni Mtanzania, lazima apate haki zote za Mtanzania, aheshimiwe na Watanzania wote kufuatana na karama zake na mchango wake katika taifa letu.
Chombo cha umoja wa kitaifa
Wale wanaoiona hatari iliyo mbele yetu ya kuuvunja umoja wetu na hasa hatari ya dini za kigeni, ni lazima wafikirie kwa haraka jinsi ya kuunda chombo cha kujenga umoja wa kitaifa.
Nilivyodokeza hapo juu, vyama vya kisiasa tulivyonavyo kwa sasa haviwezi kujenga umoja wa kitaifa. Dini za kigeni ni adui mkubwa wa umoja wetu.
Mifumo mingine imeharibiwa makusudi! Lazima sasa kuundwe chombo cha kujenga umoja wa kitaifa.
Chombo ambacho hakitatawaliwa na vyama vya kisiasa, chombo ambacho hakitatawaliwa na dini, chombo ambacho hakitatawaliwa na matajiri, wawekezaji kutoka nje, ushawishi na nguvu kutoka nje ya nchi, ukabila wala ukanda.
Kuna tetesi kwamba sasa hivi Wakristo wanaomba na kusali kwa nguvu zote ili Tanzania, isitawaliwe na rais Mwislamu tena. Pia, Waislamu wanasali kwa juhudi ili Tanzania, isitawaliwe tena na rais Mkristo!
Kwa vile tumezoea kutawaliwa na unafiki, mambo haya hayasemwi na kuonyeshwa wazi; ni ajenda za siri ambazo kila kikundi kinazitunza kwa uaminifu mkubwa. Mwelekeo huu siyo wa umoja na wala si wa kujenga amani.
Powered by Blogger.