Watoto wengine 11 wakutwa wamefichwa
Baadhi ya watoto 18 katika tukio la kwanza walikuwa wakihifadhiwa kwenye nyumba iliyopo Kata ya Pasua kwa lengo la kuwafundisha dini ya Kiislamu, mkoani Kilimanjaro. Picha ya Maktaba
Moshi. Mambo mazito zaidi yamezidi kubainika mkoani
Kilimanjaro baada ya polisi kugundua nyumba nyingine yenye watoto kumi
na mmoja waliokusanywa kutoka mikoa mbalimbali kwa ajili ya kufundishwa
dini.
Hii ni mara ya pili katika muda usiozidi wiki
moja baada ya polisi kubaini nyumba iliyohifadhi watoto 18 kwa lengo
kama hilo Jumamosi iliyopita.
Kamanda wa polisi mkoani
hapa, Geofrey Kamwela alisema tukio hilo linafanya wapelelezi kuumiza
vichwa kwa kuwa mikoa waliyotoka ndio ile ile waliyotoka watoto 18
waliokutwa kwenye nyumba moja mjini Moshi.
Nyumba hiyo
imebainika wakati kukiwa na madai kwamba baadhi ya misikiti katika
maeneo ya Pasua, Njoro na Kibosho yanaendesha mafunzo ya judo na karate.
Kamanda
Kamwela alieleza kuwa kama ilivyokuwa awali, watoto waliobainika juzi
wanatoka katika mikoa ya Tanga, Dodoma, Singida, Tabora na Kilimanjaro.
Kwa
mujibu wa kamanda huyo, watoto hao waligunduka katika nyumba iliyoko
eneo la Lyamungo wilayani Hai. Alisema umri wao ni kati ya miaka 14 na
17 na walikuwa wanafundishwa dini na ushonaji.
Alisema
kituo hicho ambacho hakijasajiliwa, kinaitwa Umm Sukhail na kinamilikiwa
na mwalimu mstaafu, Abubakar Juma (64) mkazi wa Tanga ambaye kwa sasa
anaishi maeneo ya Kibosho Mweka.
Kamwela alisema watoto
hao wamechukuliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi ili kujua sababu za wao
kuishi katika eneo hilo pia kubaini ukweli wa mafunzo yanayotolewa
kwenye kituo hicho.
“Kutokana na kugundulika kwa
mafunzo haya yasiyo rasmi yanayotolewa na walimu ambao pia si rasmi,
lazima tuchunguze kama baada ya kuhitimu wanapewa vyeti na wanafanya
kazi wapi,” alisema.
Kamwela pia alisema polisi
wanafanya uchunguzi ili kubaini kama watoto hao walipata elimu ya msingi
kama sheria inavyoelekeza na kama walifaulu ama la na kwanini
hawakuendelea na masomo. Kamanda alisema upo uwezekano wa watoto 18
waliokutwa Pasua kuhamishiwa kituo cha Narumu na kwamba jeshi hilo
linaendelea na uchunguzi kubaini kama wenye vituo hivyo wanafanya kazi
pamoja.
Kuhusu watoto 18 wa Pasua, Kamanda Kamwela
alisema wametambuliwa na wazazi wao na kuchukuliwa, lakini bado
uchunguzi unaendelea kujua uhusiano wao na mmiliki wa nyumba hiyo.
“Tunachunguza kujua kama wazazi walikuwa wakifahamu
maisha wanayoishi na sababu za kuwatoa kwenye shule za Serikali na
kuwapeleka kwenye shule za dini wakati elimu ya msingi ni ya lazima,”
alisema.
Pamoja na wazazi wo kudai waliridhia watoto
wao kwenda kupatiwa masomo hayo, kamanda alisema uchunguzi umebaini
watoto hao walikuwa wanaishi kwenye mazingira magumu kutokana na ufinyu
wa eneo na hivyo hulazimika kulala chini.
“Upelelezi
kuhusu tukio hili bado unaendelea kwa sababu kuna maswali mengi
yanayohitaji majibu kwa kuwa watoto hawa bado ni wadogo na walitakiwa
wawe wanasoma shule ya msingi,” alisema.
“Lakini wakawa
wanaishi kwenye nyumba hii lazima tujue uhalali wa wao kuacha shule na
kwenda kujifunza dini kwenye nyumba ambayo haijasajiliwa na nyumba
ambayo huduma za kijamii sio rafiki.”
Kamanda alisema:
“Elimu inayotolewa kwa siri ambayo hata Serikali haijui na majirani
hawajui inatia shaka na ndio maana polisi wanafanya uchunguzi kujua ni
siri gani imejificha.”
Kuhusu Jeshi la Polisi kuwa na
taarifa ya kuwapo mafunzo ya judo na karate kwenye baadhi ya nyumba za
ibada, alisema watachunguza madai hayo.
Inadaiwa mafunzo hayo hutolewa usiku katika baadhi maeneo ya Pasua, Njoro, Kibosho, na wilaya za Mwanga na Same.
Aprili
mwaka jana, raia 20 wa Yemen walikutwa vichakani alfajiri wilayani Same
na walipohojiwa na kiongozi mmoja wa kisiasa, walidai wamekuja
kufundisha dini.
Habari zinadai miezi kadhaa iliyopita,
polisi mjini Moshi walivamia msikiti mmoja uliopo Kibosho na kukuta
vijana wadogo kutoka Singida, Babati na Kondoa wakifundishwa mbinu hizo
za kupigana.
Katibu wa Baraza la Waislamu (Bakwata) wa
Kilimanjaro, Rashid Mallya aliliambia gazeti hili juzi kuwa wamestushwa
na wimbi hilo la watoto kuletwa mkoani hapa kwa mafunzo ambayo
aliyaelezea kuwa hayafahamika.
“Tumeshtushwa na
hatuliungi mkono hili kwa sababu maeneo ya kufundishia dini yetu
yanajulikana na si nyumbani kwa mtu. Vyombo vyetu vichunguze jambo hili
kwa uzito,”alisema.