Mbatia aitupia lawama Serikali ajali ya Iringa
Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu kuendelea kwa ajali za barabarani. Picha na Venance Nestory
Dar es salaam. Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi taifa ,James
Mbatia amesema kwamba ajali iliyotokea eneo la Mafinga Changalawe
mkoani Iringa ilikuwa imepangwa na binadamu na wala sio mipango ya
Mungu.
Akizungumza jijini leo Mbatia amesema ajali hiyo
ilipangwa na watendaji wa serikali kwa sababu ajali hiyo ilisababishwa
na shimo kubwa ambalo limekaa kwa muda mrefu eneo hilo pasipo juhudi
zozote za Serikali kulikarabati.
Mbatia amesema hawezi
kukaa kimya ni lazima awasilishe suala hili bungeni ili wahusika
wachukuliwe hatua kwa kuacha shimo kubwa barabarani kwa muda mrefu bila
kuliziba.
Amesema shimo hilo ambalo ndio hasa lilikuwa
chanzo cha ajali hiyo ni la muda mrefu lakini viongozi wa serikali
wanaliangalia tu bila kuchukua hatua ya kuliziba.
‘’Jamani
watanzania waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo ni wengi na ni aibu
kwa taifa, ukizingatia chanzo cha ajali hiyo ni shimo la muda mrefu
ambalo linaangaliwa na viongozi wetu kila siku bila kuliziba’’alisema
Mbatia
Amesema ajali hudokeza kwa ujumla matokeo mabaya
ambayo labda yangeweza kuepukwa au kukingwa ikiwa matukio
yaliyosababisha ajali hiyo yangetambuliwa na kurekebishwa kabla ya
tukio.
Amesema madereva wanaoendesha magari ya abiria
wanatakiwa kupelekwa shule angalau kwa miezi sita ikiwa ni pamoja na
kupimwa afya mara kwa mara.
Aidha ameitaka serikali
kutoa tamko kuhusu ajali hiyo na sio kukaa kimya mpaka waanze kupigiwa
makelele na wananchi kupitia vyombo vya habari.
Watu
zaidi ya 40 waliokuwa kwenye basi la kampuni ya Majinjah Express
lililokuwa likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam, walifariki papo hapo
katika ajali hiyo iliyotokea jana wengine 23 wakijeruhiwa.