Serikali kujenga nyumba 403 Mwakata
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na kuwafariji waathirika wa Mvua ya Mawe,iliyonyesha hivi karibuni katika Kijiji cha Mwakata,Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga. Picha na Mwandishi Wetu
Kahama. Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali itajenga nyumba
403 ambazo zimebomolewa na mvua kubwa iliyonyesha wiki iliyopita katika
kijiji cha Mwakata wilayani Kahama na kusababisha watu 649 kukosa
mahali pa kuishi.
Kauli hiyo aliitoa jana kwenye kijiji
cha Mwakata baada ya kutembelea eneo lililoathiriwa na mvua hiyo na
kujionea maisha duni wanayoishi watu hao.
Akizungumza
na wananchi waliohudhuria mkutano wake Rais Kikwete alisema Serikali iko
pamoja na wananchi hao na itahakikisha makazi yao yanarejea katika hali
yake ya kawaida kwa kuwajengea nyumba hizo.
Pia, Rais
Kikwete aliagiza Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) wajenge nyumba hizo bila
kupitia mkandarasi yeyote kama vile ulivyo ujenzi wa Serikali kwa kuwa
ujenzi wa jeshi unaisha kwa muda mfupi na hakuna uchakachuaji
Aliwataka
viongozi mkoani Shinyanga kuhakikisha ujenzi huo hautangazwi na kuagiza
JKT kwenda kwenye eneo hilo kufanya tathmini ya ujenzi huo ili uanze
mara moja.
Rais Kikwete aliwatoa wasiwasi wananchi wa Mwakata
waliokumbwa na tatizo hilo kwamba Serikali itahakikisha wote wamepata
chakula hadi mwisho watakapolima na kupata mavuno na tukio hilo
wasilihusishe na imani za kishirikina.
Alisema mvua
hizo ni za kawaida ambazo hutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi na si
ushirikina hivyo aliwataka wananchi hao waendelee kuwa na hisia hizo
lakini wasilichukulie kwa uzito swala la ushirikina wakatafuta mchawi wa
mvua hiyo
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ally
Rufunga alimwambia Rais Kikwete kwamba mvua hiyo licha ya kuua watu 47
pia imeharibu mazao hekari 2,332 pamoja na visima 53 vya maji ya kunywa.
Rufunga
alisema mpaka kufikia sasa wahisani mbalimbali wamechangia kwenye tukio
hilo Sh64 milioni pamoja na tani 63 za unga wa sembe pamoja na mahitaji
mbalimbali ya kibinadamu yakiwamo mabati zaidi ya 1,000
Kufuatia
hali hiyo Rais Kikwete alisema Serikali itatumia zaidi ya Sh 2 bilioni
kurejesha makazi hayo huku akitupilia mbali madai ya Mbunge wa jimbo la
Msalala, Ezekiel Maige ya kuitaka Serikali ifute ushuru wa vifaa vya
ujenzi ili wananchi wanunue kwa bei rahisi wajenge nyumba za kisasa.