Waliokufa ajali ya basi Mafinga sasa wafikia 50
Mmoja wa Majeruhi katika ajari ya basi la Majinja ilitokea juzi na kusababisha vifo vya watu 42 akiwa amelazwa katika Hosptali ya Wilaya ya Mufindi jana. Picha na Geofrey Nyangóro
Dar\Mikoani. Idadi ya watu waliofariki dunia katika ajali ya Basi la Majinjah imeongezeka na kufikia 50.
Mkuu
wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema maiti zilizotambuliwa na zile
zilizobakia, walipohesabu waligundua idadi yao kufikia 50.
“Tumebaini
kuwa maiti katika ajali ile zimefikia 50 baada ya kuhesabu vizuri zile
zilizotambuliwa na ambazo bado hazijatambuliwa hadi sasa,” alisema
Masenza.
Awali, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Robert
Salim alisema majeruhi waliopokewa hospitali hapo walikuwa tisa na mmoja
ndiye amefariki dunia.
Alisema majeruhi huyo ni Osward Mwinuka (58), aliyefariki dunia usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa.
Dk
Salim alisema hali za majeruhi wanne waliolazwa Hospitali ya Rufaa ya
Iringa zinaendelea vizuri wakati wengine wanne hali zao siyo nzuri na
wanatarajia kuwapa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Alisema maiti waliofikishwa hospitalini ni 27 na nane walitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao wengi wao kutoka Mbeya.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi aliwataja waliotambuliwa kuwa
ni Mbezi Deogratius, mkazi wa Soweto Mbeya, Editha Ngunangwa, mkazi wa
Soweto, Mohamed Juma, mkazi wa Mbeya, Ndenya Sixbert, mkazi wa Mbeya,
James Kinyamaguho, mkazi wa Morogoro, Said Halfan na Abuu Mangula.
Waliojeruhiwa ni Mustafa Ally, Dominic Shauri, Tito
Kyando, Martin Haule, Ipyana Mbamba, Fadhil Kalenga, Mussa Mwasege,
Nehemia Mbuji, Josam Abel, Tumpate Mwakapala, Nico Hamis na Esther
William.
Wengine ni Peter Mwakanale, Kelvin Mwakaladi,
Raphael Nerbot, Maga Sebastian, Catherine Mwijungu, Lucy Mtanga, Debora
Vicent, Ester na mwanaume ambaye jina lake halikuweza kujulikana
kutokana na kuwa katika hali mbaya.
Vilio mkoani Mbeya
Wakati huohuo, mitaa mbalimbali ya Jiji la Mbeya jana ilijaa misiba iliyotokana na ajali hiyo.
Waandishi
wa habari ambao wamepoteza ndugu zao ni pamoja na mwanahabari wa
Kampuni ya Mwananchi Communications mkoani hapa, Brandy Nelson aliyefiwa
na kaka yake, Osward Mwinuka na mfanyakazi wa Kampuni ya New Habari,
Mercy Mwalusamba wa mkoani Iringa aliyempoteza mdogo wake aliyetajwa kwa
jina la Omega Mwakasege, wakati Tumaini Msowoya wa gazeti la Uhuru wa
Iringa akimpoteza kaka wa mumewe.
Taasisi zingine
zilizoathiriwa na ajali hiyo ni pamoja na vyuo hususani Chuo cha
Maendeleo ya Jamii Uyole (wanne) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinadaiwa
kupoteza wanafunzi watano.
Baadhi ya misiba hiyo
ilihusisha wanandugu zaidi ya mmoja, wakiwamo wafanyabiashara, Alfred
Sanga wa Soweto, ambaye amefariki dunia na mdogo wake, Luteni Sanga.
Imeandikwa na Berdina Majinge, Hakimu Mwafongo (Iringa), Godfrey Kahango (Mbeya) na Hussein Issa (Dar).