Utaratibu Chadema sasa walalamikiwa
Bunda. Utaratibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), wa kutaka mwanachama anayehitaji kugombea nafasi mbalimbali
katika Uchaguzi Mkuu ujao kujigharimia mikutano yote ya kujinadi,
umewaweka njia panda baadhi ya waliotangaza nia wilayani hapa.
Hali hiyo ilidaiwa kujitokeza juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Stendi ya Zamani mjini Bunda.
Ilielezwa kuwa, mkutano huo uligharimiwa na Pius Masururi aliyetangaza nia kugombea ubunge mjini Bunda.
Baadhi
ya waliotangaza nia ambao walikuwapo eneo la mkutano walisema utaratibu
huo hauna budi kuachwa kwa kuwa unawanyima haki maskini na kuwabeba
matajiri, jambo ambalo ni hatari kwa chama hicho.
Hadi
sasa wanachama tisa wa Chadema wameshatangaza nia ya kuwania ubunge
mjini Bunda, jimbo ambalo linaloshikiliwa na Waziri wa Kilimo, Chakula
na Ushirika, Stephen Wasira ambaye pia ametangaza nia ya kulitetea.
Mwenyekiti
wa Chadema Jimbo la Bunda, Samuel Imanani alisema utaratibu huo
uliotolewa na chama Makao Makuu, hauna budi kufuatwa na kila mwanachama
mwenye uchungu.
Alisema utaratibu huo ni kipimo cha mwanachama kama anaweza kukihudumia chama.
Katika
mkutano huo uliohutubiwa pia na viongozi mbalimbali wa Chadema,
Masururi alitumia takriban dakika 20 kusisitiza nia yake ya kugombea
nafasi hiyo huku akijinadi kujipanga kumng’oa Wasira.
Masururi
alisema kinachomsukuma kugombea nafasi hiyo ni matokeo ya uwakilishi
mbaya uliopo ambao umekwamisha kwa kiwango kikubwa ukuaji wa maendeleo
ya jimbo hilo, lililojaa rasilimali nyingi huku wakazi wake wakiwa
maskini.
Pia, aliwahamasisha wananchi kujitokeza kwa
wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura ili wapate
haki ya kuwachagua viongozi wao.
Mwingine aliyehutubia
mkutano huo ambaye pia ametangaza nia ni Joyce Sokombi, aliyewataka
wakazi wa Bunda kubadilika kifikra kwa kuchagua viongozi watakaowaletea
maendeleo.