Sumaye: Nec imarisheni usawa wakati wa uchaguzi
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye
Tabora. Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, ameitaka Tume
ya Taifa ya Uchaguzi(Nec) kuhakikisha vyama vyote vinapata haki pamoja
na kulindwa na sheria katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka
huu.
Sumaye alisema hayo jana katika harambee ya ujenzi
wa Kanisa la Moravian, Wilaya ya Tabora Mjini.Alisema vyombo vya dola
havina budi kuhakikisha kampeni zinakuwa na utulivu.
Sumaye aliyekuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo, alizungumzia zaidi suala la udanganyifu katika matokeo na wizi wa kura.
Katika hilo, alisisitiza usimamizi madhubuti na ulinzi katika vituo vya upigaji kura.
“Hili
ni eneo nyeti na kama hakuna uwazi wa kutosha, fujo na umwagaji damu
huweza kutokea. Hapa ndipo panapotokea udanganyifu katika kuhesabu au
hata kuibiwa kura moja kwa moja. Tume iweke usimamizi madhubuti,”
alisema.
Sumaye aliwataka kutumia fursa katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka huu kwa kuepuka kununuliwa na wanasiasa ili wapambane na dhuluma
zilizojaa nchini.
“Watanzania naomba tuamke na tukatae
kununuliwa kama bidhaa za sokoni au za mnadani. Najua fedha ni
kishawishi kikubwa katika hali hii ya umaskini.
“Kama
tunataka kupambana na dhuluma zilizojaa nchini mwetu, pazuri pa kuanzia
ni kupambana na rushwa nyakati za chaguzi zetu,” alisema Sumaye.
Askofu Isaac Nicodemu aliwataka Watanzania kuwa shupavu katika uchaguzi ujao na kumchagua kiongozi mwenye maadili.
Aliwasisitiza waumini kuendeleza mshikamano katika ujenzi wa kanisa hilo na kuhimiza upendo kwa kila mmoja.