Uenyekiti wa Mrema wapingwa mahakamani
Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha TLP , Augustine Mrema
Dar es Salaam. Mwasisi wa chama cha TLP, Stanley Ndamugoba
amemburuza mahakamani Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Augustine
Mrema akidai si kiongozi halali.
Kesi hiyo ya madai
namba 33/2015 ilifunguliwa na Ndamugoba Ijumaa iliyopita katika Mahakama
Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam ikiambatanishwa na hati ya
usikilizwaji wa haraka.
Katika kesi hiyo ambayo Baraza
la Wadhamini limeunganishwa kama mdaiwa wa pili, Ndamugoba ameiomba
mahakama itamke uongozi wa Mrema ulifikia kikomo mwaka mmoja uliopita.
Mdai anaiomba mahakama kuu itamke kuwa kwa vile muda wake wa uongozi
ulimalizika mwaka mmoja uliopita, Mrema hana mamlaka ya kuitisha mkutano
mkuu wa uchaguzi.
Ndamugoba mwenyewe alilithibitishia
gazeti hili jana kufungua kesi hiyo akisema leo atakwenda Mahakama Kuu
ili kuchukua samansi za kumuita Mrema shaurini pamoja na Baraza la
Wadhamini.
“Ni kweli nimefungua kesi na nafikiri kesho (leo) samansi zitatoka,” alisema.
Hata
hivyo Mrema alipoulizwa na gazeti hili jana kuhusu kuwapo kwa kesi
hiyo, alisema yeye hakujiongezea muda kwa nguvu bali katiba ya TLP ndiyo
ilimwongezea muda huo.
“Mimi sikujiongezea muda kwa
nguvu wala sikuongezewa na mtu yeyote. Sisi tunafuata katiba ya TLP.
Tatizo hapa ninaloliona ni vita ya ubunge Jimbo la Vunjo,” alisema
Mrema.
Mrema alifafanua kuwa kamati kuu iliyopita,
ilifanya uamuzi na kumpitisha yeye kuwa mgombea ubunge Jimbo la Vunjo na
mgombea pekee wa nafasi ya uenyekiti wa TLP Taifa.
Bila
kutaja kifungu cha katiba, Mrema alisema halmashauri kuu ya TLP imetoa
madaraka kwa kamati kuu kufanya kazi kwa niaba yake na mkutano mkuu wa
TLP.
“Katiba iko wazi kwamba endapo kuna mazingira
yatajitokeza, kamati kuu imepewa mamlaka ya kufanya kazi za halmashauri
kuu na mkutano mkuu na uamuzi huu ulifikiwa 2007,” alisema. “Tulitumia
kipengele hicho kusogeza mbele mkutano mkuu wa uchaguzi kwa mwaka mmoja
na tumeshatangaza mkutano mkuu wa uchaguzi utafanyika Aprili 23, mwaka
huu,” alisisitiza.
Mrema alisema maelezo hayo ndiyo
ambayo waliyatoa pia kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis
Mutungi baada ya baadhi ya wanachama kulalamika na huo ndiyo msimamo wa
kikatiba.