Kanisa Katoliki latoa msimamo Katiba Mpya


Rais wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar,  Dk Ali Mohamed Shein, kwa pamoja wakikata utepe kuzindua rasmi Rasimu ya Katiba inayopendekezwa baada ya kukabidhiwa.
Dar es Salaam. Kanisa Katoliki nchini limeanza rasmi mkakati wa kutoa elimu kuhusu Katiba Inayopendekezwa kwa waumini wake, kutokana na kuondolewa kwa mambo mengi ya msingi yaliyotolewa maoni na wananchi.
Mkakati huo umeanzia katika Jimbo la Mwanza ambapo imedaiwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Juda Thaddeus Ruwai’chi ameunda kamati maalumu iliyopewa jukumu la kuchambua na kutoa ufafanuzi juu ya Katiba Inayopendekezwa katika makanisa yaliyopo katika jimbo hilo kupitia semina mbalimbali.
Kura ya Maoni ya kupitisha Katiba hiyo inatarajiwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu (siku 45 kuanzia leo), katika mkakati huo kanisa hilo limeainisha mambo 100 yaliyotolewa maoni na wananchi lakini yakaondolewa.
Uongozi wa kanisa hilo umekiri kuwapo kwa maelekezo hayo yakiwa na lengo la kutoa elimu kwa waumini wake kuhusu mambo yaliyomo na yasiyokuwamo kwenye Katiba Inayopendekezwa.
Kanisa hilo kupitia Tume ya Haki na Amani ya Tec limekuwa linatoa matamko mbalimbali kuhusu mchakato huo, likiwamo lile la Machi mwaka jana la kupendekeza Serikali tatu, lililosababisha Askofu Mkuu wa Jimbo Mkuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kuibuka siku mbili baadaye na kusema msimamo huo siyo wa Kanisa Katoliki nchini.
Katika tamko hilo tume hiyo chini ya Askofu Mkuu wa Tabora, Paulo Ruzoka, CPT ilikuwa imeeleza kuwa muundo wa Serikali mbili haukutatua matatizo ya msingi na badala yake ulilimbikiza kero zilizosababisha Zanzibar kujiundia katiba yake mwaka 2010 bila kushauriana na Tanzania Bara.
Akifafanua tamko hilo siku mbili baadaye, Kardinali Pengo, alisema “Maoni ya Tume hayawezi kuwa ni msimamo wa kanisa. Kanisa Katoliki lina utaratibu wa kutoa misimamo yake na huwa inatolewa na Mwenyekiti wa TEC.”
Kauli ya Rais Tec
Akizungumza na gazeti hili jana kuhusu mpango huo, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, alisema lengo la mkakati huo ni kuhakikisha waumini wa kanisa hilo wanaijua Katiba Inayopendekezwa ili waweze kukipigia kura kitu wanachokifahamu.
“Kama watapiga kura ya ‘Ndiyo’ au ‘Hapana’ hiyo ni juu yao wao. Sisi tunachokifanya ni kuwaeleza Katiba hii ina mambo gani,” alisema huku akisisitiza kuwa katiba yenyewe wananchi wengi hawaijui hadi sasa.
Kilichotokea Mwanza
Wajumbe watatu wa kamati hiyo wakizungumza katika mkutano uliofanyika katika Parokia ya Nyakato jana walisema kuwa wameombwa na Askofu Ruwai’chi kutoa elimu kuhusu mambo 40 yaliyopuuzwa na kuondolewa katika Katiba Inayopendekezwa.
Wakisoma mambo 40 waliyodai kuwa wameyachambua kutoka katika mambo muhimu 100 yaliyopuuzwa na kuondolewa katika Rasimu ya Katiba pamoja na kasoro zilizojitokeza katika Bunge la Katiba, wajumbe hao walisema baadhi ya watu wakielewa mambo hayo wataweza kuwaeleza waumini wenzao.
ADVERTISEMENT
“Kuna mambo 100 yaliyopendekezwa na wananchi lakini kanisa limeyachambua kwa kifupi na kupata mambo 40 ambayo yatasomwa ili watakaosikia waweze kuamua watapiga kura ipi siku ikifika,” alisema Deusdedit Kagashe kwa niaba ya wajumbe wawili wa kamati hiyo, Domician Saganya na Asnath Lyakulwa.
Walisema Kanisa Katoliki linapingana na mchakato wa kupata Katiba Mpya kwa sababu mchakato huo ulikosa maridhiano na ulilenga kundi la watu wachache.
Kati ya mambo 40 yaliyoanishwa ni pamoja na kuongezwa kwa ukubwa wa Baraza la Mawaziri wakati Iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipendekezwa baraza dogo la mawaziri pamoja na idadi ndogo ya wabunge.
“Upigaji wa kura ya siri na wazi lilikuwa tatizo, kujiuzulu kwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, wajumbe kuruhusiwa kupiga kura wakiwa nje ya Bunge,” inaeleza sehemu ya kasoro 40 za upatikanaji wa Katiba Inayopendekezwa.
Awali, Padri Baptist Mapunda alisema katika mahubiri yake kwamba kanisa haliko tayari kuona Katiba ikipitishwa na wachache na kuyataka majimbo mengine kuiga mfano wa jimbo la Mwanza.
Aliomba vichapishwe vitabu vidogo vyenye mambo hayo 40 ili visambazwe katika jumuiya ndogondogo ili waumini waweze kusoma na kuelewa.
Jijini Dar es Salaam, Tume ya Haki na Amani (CPT) kwa kushirikiana na Tec, imetoa waraka ikipendekeza kusitishwa kwa mchakato wa kura ya maoni ili kupisha maandalizi ya Uchaguzi Mkuu kwa sababu Katiba Inayopendekezwa imepatikana kwa njia zilizojaa utata mwingi wa kisheria, maadili na ukosefu wa maridhiano ya kitaifa.
Tume hiyo ilitoa mapendekezo hayo katika mkutano wake wa Kitaifa uliofanyika Februari 24 – 25 mwaka huu katika Kituo cha Mbagala jijini Dar es Salaam wakati ikijadili mchakato wa Katiba na Kura ya Maoni.
“Katika hali hii, mkutano unaazimia kwamba: Ama mchakato usitishwe mpaka baada ya Uchaguzi Mkuu ambapo hatua stahiki zitachukuliwa. Au, kama mchakato hautaahirishwa, kwa kuzingatia Tamko la Tume ya Haki na Amani la Novemba 2014, wananchi wahamasishwe kupiga kura ya “hapana” kwenye Kura ya Maoni,” ulisoma waraka huo uliochapishwa na gazeti la TEC la Kiongozi.
Kasoro
Baadhi ya kasoro zilizoelezwa katika waraka huo ni kukiukwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na ile ya Kura ya Maoni na jinsi tarehe ya kura hiyo ilivyotangazwa na usambazaji usioridhisha wa katiba Inayopendekezwa.
Tume hiyo imesema kuwa kasoro za mchakato huo zinadhihirisha ukiukwaji wa hali ya juu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliosababisha kupitishwa kwa Katiba Inayopendekezwa kwa njia na misingi iliyojaa utata mwingi wa kisheria, maadili na ukosefu wa maridhiano, muafaka na mshikamano dhati wa kitaifa.
Katika mkutano huo, Tume hiyo ilizingatia umuhimu wa kukamilika uandikishaji wapigakura katika Daftari la Kudumu la Wapigakura na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutumia uwezo na muda wa kutosha kutimiza wajibu wake ndani ya muda uliobaki.
Powered by Blogger.