Simba yaendeleza ubabe kwa Yanga
Mashabiki wa Simba wakishangilia huku wakiwa wamebeba mfano wa jeneza baada ya timu yao kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga jana kwenye Uwanja wa Taifa. Picha na Said Khamis
Dar es Salaam. Mshambuliaji Emmanuel Okwi alitumia juhudi
binafsi kumtungua kipa, Ally Mustapha katika dakika ya 51 na kuipa Simba
ushindi mnono wa bao 1-0 dhidi ya wachezaji 10 wa Yanga jana kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Okwi alipokea pasi
ndefu kutoka kwa Juuko Murshid aliyempoka mpira Simon Msuva aliyeshidwa
kutuliza kona fupi aliyopigiwa na Haruna Niyonzima kabla ya kutoa pasi
kwa mfungaji ambaye alimwangalia kipa Mustapha aliyekuwa ametoka golini
na kupiga shuti la umbali wa mita 35, na kujaa wavuni.
Bao
hilo la Okwi lilitibua kabisa rekodi nzuri ya Mustapha aliyokuwa nayo,
hali iliyofanya baada ya filimbi ya mwisho Barthez kuangua kilio na
kudondoka chini hadi pale meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alipokwenda
kumwinua na kumsindikiza kwenda vyumba vya kubadilishia nguo.
Yanga
iliyoshindwa kabisa kwenda na kasi ya Simba iliyokuwa ikicheza kwa
kujiamini ilipata pigo jingine dakika ya 71, wakati kiungo wake
Niyonzima alipopewa kadi ya pili ya njano na kutolewa nje kwa kadi
nyekundu na mwamuzi Martin Saanya ambaye katika mchezo huo alitoa kadi
za njano tisa, Simba wakipata kadi tatu na sita kwa Yanga pamoja na
nyekundu.
Simba ilianza mchezo taratibu na kutawala
sehemu ya katikati ya uwanja kwa kugongeana pasi fupi fupi huku viungo
wake Jonas Mkude, Abdul Banda, Ramadhani Singano na Ibrahimu Ajibu
wakiwazidi ujanja wenzao wa Yanga.
Yanga ambayo imekuwa
ikitumia winga wake wenye kasi kufanya mashambulizi, Msuva na Mrisho
Ngassa ambao katika mchezo huo walishindwa kutamba kutokana na ubora wa
mabeki wa pembeni wa Simba, Kessy Ramadhani na Mohamed Hussein.
Hata
hivyo nafasi chache ilizopata Yanga kupitia washambuliaji wake Msuva,
Ngassa, Amiss Tambwe walionekana kukosa umakini na mashuti yao mengi
yaliishia mikononi mwa kipa Ivo.
Kocha wa Yanga, Han
Pluijm alilazimika kumtoa Danny Mrwanda baada ya kupewa kadi ya njano na
nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Javu ambaye alisaidia kuimarisha
safu ya ushambuliaji ya Yanga ambayo ilikosa bao dakika ya 36, baada ya
krosi ya Javu kumpita Tambwe na kumkuta Ngassa ambaye alipiga shuti
hafifu lililookolewa kwa miguu na Ivo kabla ya Msuva kupiga shuti
lililopaa juu.
Hadi mapumziko mwamuzi Martin Saanya
alitoa kadi saba za njano, tatu kwa Simba na nne kwa Yanga kutokana na
vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyoonyeshwa na wachezaji wa timu zote
mbili.
Mara baada ya mechi kumalizika kocha wa Yanga,
Pluijm alisema Simba ilikuwa na bahati, lakini pia ilicheza mpira wa
nguvu kulinganisha na timu yake, hivyo wanajipanga kwa mchezo ujao wa
ligi.
Taulo la Ivo
Mwamuzi
Saanya alilazimika kumzuia kipa wa Simba, Ivo asining’inize taulo lake
katika goli kutokana na imani za kishirikina zinazotawala katika mchezo
huo.
Kwa nini Yanga huwa inazidiwa na Simba?
Simba
hata kama itakuwa katika kiwango dhaifu huwa inafanya maandalizi
makubwa kujiandaa dhidi ya Yanga kuliko inavyojiandaa na mechi yoyote
ile labda jambo hilo nalo linachangia kuwapa wakati mgumu wapinzani wao
pindi wanapokutana.
Lakini jambo jingine linalochangia
Yanga kuwa na wakati mgumu katika mechi dhidi ya Simba ni kwamba
wanakuwa katika presha kubwa ya mchezo kuliko Simba ambao huwa
wanatulia, Yanga huwa na wasiwasi.
Msimu uliopita
kwenye Ligi Kuu Bara, Simba ikiwa dhaifu, lakini ilitoka sare ya mabao
3-3 na Yanga, mabao ya Yanga yakifungwa na Mrisho Ngassa na Hamis Kiiza
aliyefunga mawili wakati ya Simba yalifungwa na Betram Mwombeki, Joseph
Owino na Gilbert Kaze.
Mzunguko wa pili timu hizo
zilitoka tena sare ya bao 1-1, bao la Simba likifungwa na Harun Chanongo
wakati la Yanga lilifungwa na Simon Msuva.
Lakini
Simba iliyokuwa dhaifu iliibuka mbabe mbele ya Yanga iliyokuwa katika
ubora wake kwa kuinyuka mechi zote mbili za Nani Mtani Jembe kuanzia
mwaka juzi walipoifunga Yanga mabao 3-1 na mwaka jana waliichapa mabao
2-0.
Awali timu ya vijana wa Simba iliisambaratisha
Yanga kwa kuinyuka kwa mabao 4-2 ushindi ulioamsha shangwe kwa mashabiki
wa Simba.
Tanga. Mgambo Shooting ilitumia vizuri uwanja wake wa nyumbani kwa kuichapa Ndanda FC kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Mgambo
ilipata mabao yake kupitia Salim Aziz Gilla aliyefunga mabao mawili
dakika ya 14 na 70, Malimi Busungu (26), wakati Ndanda ilipata bao lake
kupitia Gideon Benson (44).
Wakati Mtibwa Sugar ililazimishwa sare 1-1 na Mbeya City kwenye Uwanja wa Manungu.
Vikosi
Simba:
Ivo Mapunda, Kessy Ramadhani, Mohamed Hussein, Hassan Isihaka, Juuko
Murshid, Abdi Banda/Simon Sserunkuma, Ramadhani Singano, Ibrahimu Ajibu/
Elius Maguri, Said Ndemla na Emmanuel Okwi.
Yanga:
Ally Mustapha, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kelvin Yondani,
Said Juma, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Mrisho Ngassa/
Kpah Sherman na Danny Mrwanda/ Hussein Javu.