Nyumba 30 zabomolewa na mvua Mara
Mafuriko
Serengeti. Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali,
imesababisha nyumba zaidi ya 30 kuanguka, ng’ombe saba kufa katika
vitongoji vya Maganana na Mgenda Msirori katika Kijiji cha Gusuhi, Kata
ya Nyambureti Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Ofisa
mtendaji wa kijiji hicho, Juma Kitorobo alisema jana kuwa mvua hiyo ya
dakika tano, ilinyesha kijijini hapo mwishoni mwa wiki iliyopita na
kusababisha madhara hayo makubwa.
Alisema mbali na mvua
hiyo kusababisha uharibifu mkubwa, pia ilimjeruhi mtu mmoja, ambaye kwa
sasa amelazwa Hospitali Teule ya Wilaya ya Serengeti.
“Madhara
ni mengi baada ya mvua kubwa kunyesha, lakini kubwa ni kuharibika kwa
nyumba nyingi na mazao kijiji hapa,” alisema Kitorobo.
Alisema
nyumba 29, zikiwemo za nyasi 12 na bati 10, zilianguka kabisa, huku
nyumba sita zikiezuliwa na ghala moja la vyakula kubomoka.
“Ng’ombe saba, mbuzi watatu walikufa kutokana na mvua hiyo, huku pia mazao yakiharibika,” alisema na kuongeza:
“Tukio hilo limeacha maswali kwa wananchi kwa kuwa mvua ilinyesha muda mfupi na upepo ulikuwa mkali kama kimbunga.”
Mwenyekiti
wa Kitongoji cha Maganana, Ndori Motiba alisema wanakijiji
wamekubaliana kumjengea nyumba mwanakijiji mwenzao, Mgaya Motika ambaye
mke wake amejeruhiwa vibaya wakati akijaribu kuwaokoa watoto wake kutoka
kwenye nyumba ambayo iliangushwa na mvua hiyo.
“Mwenzetu
hana makazi kutokana na mvua hii, lakini pia mke wake amejeruhiwa,
hivyo tumekubaliana kumsaidia kujenga nyumba nyingine,” alisema.-