Kanisa la Pentekoste lanusurika kuteketezwa
Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Tanzania Usharika wa Tandika, Dar es Salaam, Raymond Noya akionyesha kiti kilichoungua baada ya kuchomwa moto na watu wasiojulikana katika jaribio la kuchoma ofisi ya kanisa hilo mwishoni mwa wiki iliyopita. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam. Kanisa la Pentekoste Tanzania Usharika wa
Tandika, Manispaa ya Temeke limenusurika kuteketezwa kwa moto. Tukio
hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita na mtuhumiwa alikamatwa na
kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi Chang’ombe.
Kaimu
Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Kamishna Msaidizi (ACP),
Zacharia Sebastian alisema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani leo
baada ya taratibu kukamilika.
Akizungumza na gazeti
hili katika ofisi yake, ambako ndiko moto huo ulianzia, Askofu wa Kanisa
Jimbo la Temeke, Raymond Noya alisema tukio hilo ni la kushangaza,
kwani halikulenga kuiba mali zilizokuwamo kwenye ofisi hiyo.
“Hili
siyo suala la uhuni…naona inaweza kuwa ni vita dhidi ya imani. Lengo
lilikuwa ni kuchoma kanisa na siyo kuiba vilivyomo. Kama unavyoona
hakuna kilichoguswa wala jaribio la kuvunja ama mlango au dirisha. Hili
ni jaribio la pili kutokea,” alisema Askofu Noya.
Kuhusu
jaribio la kwanza alisema lilitokea Novemba mwaka jana, lakini hakukuwa
na madhara makubwa na kesi ilifikishwa kituo cha polisi ingawa hadi leo
haijafikishwa mahakamani kwa maelezo kuwa upelelezi bado unaendelea.
Noya
alisema kwa miaka miwili iliyopita kumekuwa na matukio tofauti
yanayokwaza huduma ya kanisa, kwani wakati mwingine wamekuwa wakirushiwa
mawe wakati wa ibada.
“Kanisa lina mlinzi, lakini kuna
wakati huwa anazidiwa. Tangu kanisa hili lilipoanzishwa mwaka 1997 ni
miaka miwili tu iliyopita ndipo mambo yameanza kubadilika. Tumekuwa na
ushirikiano mzuri na watu wanaotuzunguka kwa muda wote tuliokuwapo
hapa,” alieleza.
Alphonce John, mkazi wa eneo lilipo
kanisa alishangazwa na tukio hilo na kusema hakutegemea vitendo vya
uharifu wa aina hiyo vinaweza kufanyika wakati huu.
“Wanapokuwa
na sherehe watu wa mtaani huwa tunaalikwa na tunaenda kujumuika nao kwa
chakula. Hakuna ugomvi wowote kati yetu. Hii inashangaza,” alisema
John.