Wagombea urais wagongana msiba wa Komba


Rais wa Tanzania,Jakaya Kikwete akiwafariji wanafamilia ya Mbunge wa Mbinga Magharibi na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Marehemu John Komba, nyumbani kwa marehemu Mbezi Tanki Bovu, Dar es salaam jana. Wapili kushoto ni Mke wa Marehemu. Picha na Said Khamis
Dar es Salaam. Msiba wa Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba jana uligeuka uwanja wa siasa, baada ya makada wa CCM wanaotajwa kugombea urais pamoja na wapambe wao kupigana vikumbo na kurushiana vijembe, ikiwa na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Ilikuwa kama walijipanga kwani kila mgombea aliyekuwa anafika katika msiba huo alionekana kuwa na wapambe waliompokea, kumpeleka kutoa pole kwa wafiwa na kumuonyesha eneo la kukaa.
Ukiacha kauli mbalimbali walizotoa kumwelezea marehemu Komba (61), wapambe wa wagombea hao walionekana mara kwa mara kuwa karibu nao wakizungumza, hali iliyoonyesha kuwa kila kundi lilitaka mgombea wao kuonyesha uwepo wake.
Waliohudhuria
Wanaotajwa kuutaka urais ambao walihudhuria msiba wa mbunge huyo uliotokea juzi jioni ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, wote kutoka CCM, pamoja na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibroad Slaa.
Wapiga picha na Membe
Membe ndiyo alikuwa wa kwanza kufika nyumbani kwa marehemu eneo la Mbezi Tangi Bovu na baada ya muda aliwasili Rais Jakaya Kikwete na kukaa naye.
Mara baada ya Rais Kikwete kuondoka, Membe alilakiwa na kundi kubwa la makada wa CCM ambao mbali na kumsalimia walimvuta pembeni na kuomba kupiga naye picha huku wakisika wakisema kuwa “Tunataka kupiga picha na mheshimiwa rais”.
Watu hao ambao walikuwa wakiongozwa na Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage ambaye hata hivyo hakupiga picha na waziri huyo, walisema kuwa kama mambo yakienda vyema, Membe anaweza kuwa rais na hata alipokuwa akiondoka walimsindikiza hadi kwenye gari lake.
Vijana na Nchimbi, Ngeleja
Ukiacha Dk Nchimbi ambaye alikuwa akizongwa zaidi na vijana wa CCM, kivutio kingine kilikuwa kwa Ngeleja ambaye mara kwa mara alikuwa akizungukwa na vijana waliokuwa wakimuuliza maswali mbalimbali, hasa kuhusu sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Ngeleja pamoja na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka walipata mgawo wa fedha kutoka katika akaunti hiyo na tayari wamehojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM, huku Ngeleja akisubiri kesho kuhojiwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo tayari imeshamuhoji Profesa Tibaijuka.
“Kwa sasa siwezi kusema chochote. Chama kilitupa adhabu (ya kuanza kampeni za urais mapema), ninaiheshimu adhabu hiyo na ninasubiri tamko la chama na hapo ndiyo nitakuwa na mengi ya kusema,” aliwajibu Ngeleja.
Mwigulu na wanahabari
Kiongozi mwingine aliyekuwa kivutio ni Mwigulu Nchemba kwani kila baada ya muda aliitwa na makada wa chama hicho katika makundi na kuonekana wakizungumza mambo mbalimbali.
Nchemba ambaye hivi karibuni ziara zake za mikoani zilisitishwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwa maelezo kuwa hazikuwa na baraka za chama hicho na zililenga kujitangaza, ndiye kiongozi aliyeongoza kwa kuzungumza na vyombo vya habari katika msiba huo.
Katika muda wa saa tano aliokaa katika eneo hilo alizungumza na vyombo vya habari zaidi ya mara tano, ikiwa ni mara nyingi kuliko kiongozi yeyote aliyefika katika msiba huo.
Lowassa azima muziki
Kati ya viongozi waliokuwa kivutio zaidi ukiacha Dk Slaa, ni Lowassa ambaye alifika katika msiba huo saa 7:30 mchana ikiwa ni nusu saa baada ya walinzi wake kufika.
Mara baada ya kufika aliwapa pole wafiwa na kwenda kukaa eneo lililotengwa kwa ajili ya viongozi wa Serikali karibu na Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba na Ngeleja, na mara kadhaa alifuatwa na makada wa chama hicho na viongozi mbalimbali na kuzungumza naye.
Wakati akizungumza na vyombo vya habari, muziki uliokuwa ukipigwa iliamuliwa uzimwe na mmoja wa waongozaji wa msiba huo kwa maelezo kuwa waziri huyo wa zamani na mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama alikuwa akizungumza.
Dk Slaa na walinzi
Mara baada ya Lowassa kuondoka eneo hilo, muda mfupi baadaye aliwasili Dk Slaa akiwa na walinzi watano wenye miraba minne wakiwa wamevaa suti nyeusi na miwani nyeusi.
Kuwasili kwa kiongozi huyo wa Chadema kuliibua minong’ono ya hapa na pale kutokana na walinzi waliokuwa wamemzunguka ambao hawakumpa mtu yeyote nafasi ya kumsogelea.
Msafara wa magari manne ya Dk Slaa ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa wanaotajwa kuwania urais ndani ya Ukawa, yalikuwa yamepambwa na bendera za Chadema tofauti na viongozi wa CCM waliofika eneo hilo
Powered by Blogger.