Makonda aanza U-DC kwa staili ya Mwinyi



Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda (wa pili kulia), akimsilikiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, mhandisi Mussa Nati, alipotembelea kukagua kazi ya ujenzi wa maabara mpya ya shule ya sekondari Manzese jana. Picha na Emmanuel Herman
Dar es Salaam. Alifanya Rais Ali Hassan Mwinyi na baadaye Augustine Mrema na sasa mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda anataka kufuata nyayo baada ya kutenga kila Ijumaa kuwa siku maalumu ya kusikiliza kero za wananchi wake wa wilaya hiyo kuhusu suala nyeti la ardhi.
Mwinyi, ambaye alikuwa rais wa Serikali ya Awamu ya Pili, alitenga siku ya Ijumaa kuwa maalum kwa ajili ya kusikiliza matatizo ya wananchi, akitumia ofisi ndogo ya CCM iliyo Barabara ya Lumumba jijini Dar es Salaam.
Na Mrema, ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wakati wa Serikali ya Awamu ya Pili, alitenga siku ya Alhamisi kuwa maalum kwa ajili ya kusikiliza matatizo ya ndoa.
Sasa ni zamu ya Makonda, kiongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM ambaye uteuzi wake kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni umekuwa gumzo kutokana na kuhusishwa na vita dhidi ya kada wa chama hicho, Edward Lowassa, na Jaji Joseph Warioba, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Makonda alisema amebaini kuwa Kinondoni ina migogoro mingi ya ardhi na kwamba njia pekee ya kuitatua ni kwa kuwasilikiza wananchi na kutoa majibu ya papo kwa papo.
Akizungumza kwa kujiamini, Makonda alisema atakuwa akisikiliza wananchi kuanzia saa 3:00 asubuhi na ataanza rasmi utaratibu huo Ijumaa ijayo na kutaka kila mwananchi mwenye tatizo la ardh, kufika ofisini kwake akiwa na nyaraka zote muhimu.
“Ili kufanya zoezi hili liwe na ufanisi na mafanikio, ningeomba wananchi wafuate utaratibu kuanzia ngazi za watendaji wa chini kabla ya kufikisha katika ofisi yangu,” alisema Makonda.
Katika kufanikisha kazi hiyo, imeundwa kamati ndogo itakayomuhusisha katibu tawala, mwanasheria wa manispaa, ofisa mipango miji na ofisa ardhi, itayosimamiwa na mkuu wa wilaya.
Alisema iwapo wananchi watakaojitokeza watakuwa wengi, anaweza kuendelea na kazi hiyo kwa siku za Jumamosi na Jumapili kwa kuwa anaamini wakati huu ni wa kutatua matatizo ya wananchi.
Kuhusu uvamizi wa maeneo ya wazi, mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa atatumia kanuni aliyoiita STK, akimaanisha Sheria, Taratibu na Kanuni, kuhakikisha kuwa kila aliyejenga katika maeneo yasiyoruhusiwa anabomoa kabla hajamobolewa.
Wilaya ya Kinondoni imekuwa ikielezewa kuwa ina matatizo makubwa ya ardhi kutokana na utapeli wa viwanja, dhuluma, uwekezaji kuuziwa maeneo ya wananchi na ujenzi kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli maalumu.
“Kama kuna maeneo ya wazi ulijenga, anza kubomoa. Kauli zangu hazijawahi kubadilika. Sitatuma mgambo, nitakwenda na askari wangu kubomoa,” alisema Makonda.
Pia, Makonda alisema amejipanga kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa maji ya kutosha wilayani humo na kwamba tayari ameshaviagiza vyombo husika kuchunguza upotevu unaofikia asilimia 54 ya maji yote yanayosambazwa Kinondoni.
“Changamoto ya upatikanaji wa maji katika wilaya ya Kinondoni inazidi kukua kutokana na ukuaji wa kasi wa idadi ya watu na ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya watu kwa kujiunganishia maji isivyo halali na pia kuharibu miundombinu,” alisema Makonda.
Vile vile, alisema mkakati maalumu umeshandaliwa wa kuwatambua, kuwaumbua na kuwachukuliwa hatua za kisheria wote waliojiunganishia maji kinyume cha taratibu na sheria.
Kabla ya kiongozi huyo kukutana na waandishi wa habari, alifanya ziara ya kukagua ujenzi wa maabara katika shule za sekondari za Turiani na Manzese ambako alisema viongozi wa ujenzi wameokoa fedha nyingi za Serikali kwa kutumia mbinu mbadala.
Mkurugenzi wa Wilaya ya Kinondoni, Injinia Musa Natty, alisema wameokoa zaidi ya Sh300milioni kwenye ununuzi wa masinki ya maabara baada ya kuamua kuyatengeneza hapa nchini.
Powered by Blogger.