Serikali kuugawa Mkoa wa Mbeya
Waziri Mkuu, Mizengo PInda akizungumza na wakazi wa Mji Mdogo wa Makongorosi, Chunya baada ya wakazi hao kufunga barabara wakimtaka azungumze nao akiwa katika ziara ya Mkoa wa Mbeya juzi. Picha na PMO
Mbeya. Serikali imeyapokea maombi ya kikao cha Kamati ya
Ushauri ya Mkoa wa Mbeya (RCC) yanayopendekeza mkoa huo ugawanywe na
kuwa miwili ya Mbeya na Songwe.
Akizungumza na maelfu
ya wakazi wa Wilaya ya Chunya kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika juzi
katika uwanja wa Saba saba, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema Serikali
imeridhia maombi hayo kutokana na ukubwa wa mkoa huo ambao una kilometa
za mraba 63,000.
“Tumekwishapokea maombi ya kuugawanya
Mkoa wa Mbeya kwa sababu una eneo la kilometa za mraba 63,617
zilizogawanyika katika wilaya 8 na halmashauri 10. Hili ni eneo kubwa
sana kiutawala, siyo rahisi kuusimamia na kusukuma mbele maendeleo,”
alisema Pinda.
Alisema kamati hiyo imeshauri mkoa huo
ugawanywe katika wilaya nne, huku akifafanua kuwa mkoa mpya wa Songwe
utakuwa na wilaya za Ileje, Momba, Mbozi na Chunya. “Wamekubaliana makao
makuu yatakuwa Mbozi lakini ninyi wa Chunya mmeenda mbali zaidi kwa
kuigawa Chunya kwenye wilaya mbili za Songwe na Chunya itaenda Mbeya,”
alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.
Alisema katika kikao hicho ilikubaliwa kwamba makao makuu ya Wilaya mpya ya Songwe yatakuwa Mkwajuni.
Mkoa
wa Mbeya una wilaya nane zilizogawanyika katika tarafa 27, kata 262,
vijiji 842 na mitaa 252. Idadi ya wakazi kwa mujibu wa Sensa ya Watu na
Makazi ya mwaka 2012 ni 2,707,410.
Akizungumzia kuhusu
mpango wa maji katika wilaya hiyo, Pinda alisema bado kuna changamoto
kubwa ya kuyafikisha vijijini. “Tuna mpango wa kuchimba visima vikubwa
vitatu na mwakani tuna mpango wa kuchimba visima vingine virefu 11,
tunachohitaji ni fedha na usimamizi,” alisema.
Alivitaja
vijiji vitakavyonufaika kuwa ni Makongorosi, Mkwajuni, Kapalala,
Isangawana, Galula, Lupa na Matwiga. Vingine ni Kambikatoto, Tanile,
Bitimanyanga na Mapogoro.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu
amezindua maabara tatu katika Shule ya Sekondari Saza zilijengwa kwa
ufadhili wa Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Shanta.
Akitoa
taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Chunya,
Sophia Kumbuli alisema ujenzi wa maabara hizo tatu umegharimu Sh268.5
milioni.
ikijumuisha pia ununuzi wa samani, uwekaji wa mfumo wa maji na gesi.
“Kati
ya hizo Sh 23.5 milioni ni za ununuzi wa vifaa vya maabara na kemikali
na Sh245 milioni ni ujenzi wa jengo, samani na uwekaji wa mfumo wa maji
na gesi,” alisema.
Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara
yake mkoani Mbeya kwa kutembelea wilaya ya Mbozi ambapo mbali ya
kuzungumza na wananchi, atazindua maabara Vwawa sekondari, atakagua
ghala la nafaka la NFRA na kupokea taarifa ya uzalishaji na usambazaji
wa miche ya kahawa kwenye kituo cha TACRI - Mbimba.