Mabomu yarindima jijini Mwanza
Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU), wakilinda Mtaa wa Makoroboi, jijini Mwanza jana, baada ya kudhibiti vurugu. Picha na Ngollo John
Mwanza. Hali ya amani
katikati ya Jiji la Mwanza jana ilichafuka kwa takriban saa mbili
kutokana polisi kupambana na wananchi, waliokuwa wakipinga hatua ya
madhehebu ya Kihindi ya Swaminarayan kufunga Mtaa wa Makoroboi.
Hatua
ya wananchi ilikuja baada ya uongozi wa Hekalu la Swaminarayan kujenga
nguzo makutano ya Mtaa wa Lumumba na Makoroboi, ili kuzuia watu
kukatisha eneo hilo kwenda Makoroboi.
Awali, eneo hilo
lilikuwa lilikuwa likitumiwa na wamachinga, lakini viongozi wa hekalu
hilo walimuomba Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo kuwaondoa kwa
sababu walikuwa wakiwabughudhi wakati wa ibada zao.
Wamachinga
169 waliondolewa na kupewa eneo la Tanganyika ambako wanaendesha
biashara zao, sehemu hiyo ilibaki wazi huku wananchi wanaotaka kwenda
Makoroboi ambako kuna shughuli nyingi za jamii wakiendelea kukatisha
hapo.
Jana saa 3:00 asubuhi, hali ilibadilika ghafla
baada ya wananchi kuvamia nguzo za zege zilizojengwa usiku na kuanza
kuzing’oa, hali iliyosababisha kuitwa polisi ambao bila kuuliza
kilichokuwa kikiendelea walianza kutupa mabomu ya machozi.
Vurugu
hizo zilidumu hadi saa 5:30 asubuhi na kusababisha shughuli za
uzalishaji katikati ya mji kusitishwa, huku maeneo ya Msikiti wa Ijumaa,
Kituo cha Daladala, Mtaa wa Lumumba na Barabara ya Nyerere yakitawaliwa
na moshi wa mabomu ya machozi.
Mfanyabiasha wa eneo
hilo, Raphael Kinje alisema wamechoshwa na mabomu ya mara kwa mara
ambayo yanasababishwa na watu wachache wenye fedha.
Kinje
alisema eneo hilo ni njia ya umma ambayo inatumiwa na wananchi wengi,
hivyo kitendo cha kuweka geti kingezuia matumizi ya njia hiyo ya muda
mrefu.
Mfanyabiashara wa duka la Gupta Autos Ltd,
Jiddavy Hazaa alisema Serikali inatakiwa kuchukua hatua za kisheria ili
kuzuia vurugu hizo zinazotokea mara kwa mara, kwani zinaathiri akili na
afya za wakazi wake.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola alisema wanawashikilia vijana 12 waliokuwa wanafanya fujo.
“Tulichofanya tumedhibiti wafanya fujo na sasa tunachunguza iwapo ujenzi huo ulikuwa na kibali,” alisema Mlowola.