Kauli za viongozi zatikisa nchi
Mwaka 2013: “Sugu naomba ukae kimya, halafu uelewe mimi siongei na mbwa, naongea na mwenye mbwa.” Juma Nkamia
Dar es Salaam. Kauli kama “kutumia Sh10
milioni kununulia mboga” na ile maarufu ya “vijisenti”, zimetikisa nchi
katika siku za karibuni na kuibua hisia tofauti, lakini waliotoa kauli
hizo ni sehemu tu ya orodha ndefu ya viongozi wa umma waliowahi kutoa
maneno yaliyoibua maoni tofauti.
Kauli ya Profesa Anna
Tibaijuka, aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
ndiyo iliyokuwa gumzo katika siku za karibuni baada ya mbunge huyo wa
Muleba Kusini kusema alitumia Sh10 milioni kununulia mboga wakati
alipokuwa akihojiwa na Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa
Umma kuhusu Sh1.6 bilioni alizopewa na ambazo zinahusishwa na kashfa ya
uchotwaji wa Sh306 bilioni kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Akilieleza
baraza hilo jinsi alivyotumia baadhi ya fedha zilizoingizwa kwenye
akaunti yake, Tibaijuka alisema: “Hivyo nilipolipwa (Shilingi) milioni
117, nilitoa milioni mbili nikachangia Kanisa la Makongo na nikatoa
400,000 nikapeleka kanisani na milioni 10 niliitoa kwa ajili ya matumizi
yangu ya kununulia mboga.”
Kauli hiyo iliamsha mjadala
mkubwa uliokumbusha kauli nyingine nyingi zilizotolewa na viongozi wa
umma kwa nia njema au kujitetea wakati walipokabiliwa na matatizo au
kutetea misimamo yao au ya Serikali.
Mkurugenzi wa
utetezi, maboresho na sheria wa Kituo cha Haki za Binadamu na Sheria,
Harlord Sungusia anaelezea kauli hizo kuwa zinatokana na Katiba
kuwalinda viongozi.
“Katiba iliyopo kwa sasa inatoa
jeuri kwa viongozi kutoa kauli zozote kutokana na ulinzi waliowekewa.
Katiba imewawekea kinga kwa hivyo kwanza, inawapa kiburi cha kuona wako
juu ya sheria,” alisema Sungusia.
Sungusia pia alisema kauli hizo zinaweza kuwa zinasababishwa na mtu kutoelewa nafasi yake kwenye jamii.
“Ujinga
ni ugonjwa unaotesa nchi nyingi za Kiafrika, yaani kiongozi anaingia
kwenye kashfa ya ufisadi, lakini akifika jimboni kwake anatawazwa (kuwa
chifu) na wanakijiji, athari zake ni mmomonyoko wa utawala wa sheria na
hata kuyumba kwa nchi kama ilivyokuwa Somalia,” alisema.
Katika
sakata la escrow, fedha zilizochotwa kwenye akaunti hiyo zilihusishwa
na miamala ya mamilioni ya fedha zilizoingia kwenye akaunti za mawaziri
na wabunge waliowahi kushika nafasi nyeti serikalini, maofisa waandamizi
serikalini, majaji na viongozi wa kidini ambao walipewa kati ya Sh40.4
milioni na Sh1.6 bilioni.
Mmoja kati ya watu waliopokea
Sh80.8 milioni ni msimamizi wa makazi ya Rais, Shabani Gurumo, ambaye
alielezea kiasi hicho cha fedha kuwa ni kidogo kwa kuwa anazo fedha
nyingi zaidi ya hizo, wakati Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani,
Andrew Chenge alielezea Sh1.6 bilioni zilizohusishwa na ununuzi wa
kifisani wa rada, kuwa ni “vijisenti”.
Alitoa kauli
hiyo alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu kuhusishwa kwake na
kashfa ya ununuzi wa rada kwa bei ya juu wakati kashfa hiyo ilipoibuliwa
na Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Jinai cha Serikali ya
Uingereza.
“Wanasiasa wengine huathiriwa na mila na
desturi za makabila yao na hivyo hushindwa kuchunga kauli zao,” alisema
mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar esSalaam (UDSM), Richard Mbunda.
Alisema
viongozi wanaotoka kwenye makabila yenye asili ya uchifu, wameingia
madarakani na dhana ya kifalme hivyo wanaamini majibu yoyote ni sahihi
bila kujali jamii iliyomzunguka,” anasema.
“Tibaijuka
angezungumza kauli ile katika jamii ya Kihaya inafahamika kabila lile
jinsi lilivyo, lakini tatizo ni pale anapojisahau na kuzungumza kwa
jamii nyingine.”
Mwananchi imekusanya baadhi ya kauli
zilizowahi kutolewa na viongozi mbalimbali Serikali kuanzia enzi za
Serikali ya Awamu ya Kwanza hadi ya Nne.
John Malecela
Wakati
tatizo la usafiri linaanza kuwa kubwa na wananchi wakilalamikia hali
hiyo, John Malecela, ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Mawasiliano na
Uchukuzi, aliulizwa na waandishi wa habari kuhusu matatizo makubwa ya
usafiri wa treni na akajibu, “nani anasema Tanzania kuna shida ya
usafiri… anayesema kuna shida ya usafiri “he can go te hell”, akiwa na
maana “anaweza kwenda kuzimu”. Kauli hiyo aliyoitoa mwaka 1989
ilimsumbua sana kisiasa hadi aliposhindwa ubunge.
Basil Mramba
Wakati
akitetea uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tatu kununua ndege ya rais kwa
bei kubwa, Basil Mramba, ambaye alikuwa Waziri wa Fedha, alisema ndege
hiyo itanunuliwa hata kama “wananchi watakula nyasi”.
Mramba alikwenda mbali kidogo, kwa kauli ya kejeli akasema “Rais hawezi kupanda punda”.
Mchungaji Peter Msigwa
Wakati
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa akichangia kwenye
mjadala wa Bajeti ya Serikali, alisikitishwa na kile alichokiita kitendo
cha wabunge kutotaka kutumia akili zao kutatua matatizo ya wananchi.
“Wananchi
wametuamini tuje tujadili vitu vya maana hapa, lakini tunakubaliana
akili ndogo itawale akili kubwa. James Madison mwaka 1822, alisema
‘knowledge forever will govern ignorance (ujuzi utatawala ujinga
milele,” alisema Mchungaji Msigwa.
“Tumekubali kwenye
Bunge hili knowledge ndogo (ujuzi mdogo) i-govern knowledge kubwa
(utawale ujuzi mkubwa, tumekubali ignorance i-govern knowledge (ujinga
utawale ujuzi),tunalipeleka wapi taifa?”
Andrew Chenge
Akihojiwa
na wanahabari Aprili mwaka 2008, Mwanasheria Mkuu wa zamani wa
Serikali, Andrew Chenge kuhusu tuhuma nzito za akaunti yake iliyokuwa
kisiwa cha Jersey na ambayo ilikuwa na Dola 1 milioni za Marekani,
alijibu kwamba fedha hizo kwa viwango vyake zilikuwa ni vijisenti
akisema suala la kumiliki kiasi gani cha fedha si hoja ya kuzungumza
kwani kila mtu ana kiwango vyake.
Wiki moja kabla ya kauli yake, gazeti moja la Uingereza,
The Guardian liliandika kuwa katika uchunguzi uliofanywa na SFO,
ilibaini kuwa Chenge, ambaye wakati wa ununuzi wa rada alikuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alikuwa na fedha hizo kwenye akaunti hiyo
iliyokuwa nje ya nchi. Rada hiyo ilinunuliwa kwa bei iliyokuzwa ya Sh70
bilioni kutoka Kampuni ya Bae Systems ya Uingereza.
Cleopa Msuya
Wakati
nchi ikiwa kwenye hali ngumu kiuchumi, Cleopa Msuya, akiwa Waziri wa
Fedha aliwasilisha bajeti ambayo ilionekana haimjali mwananchi na baada
ya malalamiko, alijibu kwa kusema “kila mtu atabeba msalaba wake”, kauli
iliyozua mjadala mkubwa.
Rais Jakaya Kikwete
Julai
18, mwaka 2010, Rais Jakaya Kikwete, ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM,
alitamba kuwa chama hicho kwa miaka mitano iliyopita kimeinua maisha ya
Watanzania akifafanua kuwa foleni kubwa za magari jijini Dar es Salaam
ni ishara ya wananchi kuwa na “maisha bora”.
Alitoa
kauli hiyo wakati akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na CCM Mkoa wa
Dar es Salaam kwa ajili ya kumpongeza kuchaguliwa kuwa mgombea pekee wa
urais kwa asilimia 99.16.
Mwaka huohuo, Rais Kikwete
akihutubia wananchi wa kijiji cha Kisesa wilayani Magu katika ufunguzi
wa mashindano ya ngoma kwa Kabila la Wasukuma, alisema matukio ya mimba
kwa wanafunzi wa kike nchini yanasababishwa na viherehere vya wanafunzi
wenyewe.
Pia, katika hotuba yake ya kuomba ridhaa kwa
wananchi mwaka 2010, kati ya mambo aliyozungumzia ni hali ya ugonjwa wa
Ukimwi, kwamba wapo wanaoupata kwa bahati mbaya, wanaoambukizwa kutokana
na mazingira, lakini wengine wanaupata “kwa viherehere vyao”.
Pius Msekwa
Wakati
akiongoza moja ya vikao vya mwisho kabla ya Bunge la Tisa kuanza
shughuli zake, Pius Msekwa akiwa spika wa Bunge alilazimika kujibu hoja
za wabunge za kumtaka aachie uenyekiti wa Bodi ya Vodacom ili kumfanya
aeweze kufanya shughuli za chombo hicho cha uwakilishi wa wananchi bila
ya kuwa na maslahi binafsi.
Katika kujibu hoja hizo,
Msekwa aliwaelezea walioanzisha hoja hiyo kuwa wana “wivu wa kike”,
kauli iliyowatia hasira wanaharakati wa haki za wanawake.
John Magufuli
Mwaka
2012 wakati akizungumza na wakazi wa Kigamboni kuhusu nauli mpya ya
Sh200 ya kivuko, alisema “asiyetaka kulipa nauli hiyo, apige mbizi
baharini na kama hawezi azunguke Kongowe kuingia katikati ya jiji au
arudi kijijini akalime”.
Dk Didas Masaburi
Mwaka
2011 tuhuma za uuzwaji kifisadi wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam
(Uda) kwa Kampuni ya Simon Group liliibuka bungeni. Meya wa Jiji la Dar
es Salaam, Dk Didas Masaburi alituhumiwa kuhusika. Katika majibu ya
tuhuma hizo, Dk Masaburi alisema kuwa wabunge waliokuwa wanazungumzia
suala hilo ni wa aina tatu; waliodandia hoja bila ya kujua; wanaotafuta
umaarufu na kundi la tatu ni la wabunge ambao wanaujua ukweli lakini
wanaupotosha ili kuficha madhambi yao.
“Hawa wanashindwa kufikiri kwa kutumia akili zao, badala yake wanafikiria kwa kutumia makalio,” alisema Dk Masaburi.
Mizengo Pinda
Akijibu
swali kuhusu vitendo vya askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania kupiga
raia, hasa kutokana na vurugu zilizotokea Mtwara, Waziri Mkuu Mizengo
Pinda alisema watu wanapokaidi amri halali wanajitakia matatizo kwa
vyombo vya dola, watapigwa tu.
“Sasa kama wewe
umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi, wewe ndiyo jeuri zaidi
watakupiga tu. Mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna
nyingine, maana tumechoka,” alisema Waziri Pinda wakati wa kipindi cha
maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu kinachofanyika kila Alhamisi
bungeni.
Juma Nkamia
Mwaka
2013, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alitoa madai kuwa kuna
ukabila mkubwa kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma mjini na kwamba ana ushahidi
wa mikanda ya video, lakini mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia
akasimama na kukanusha habari hizo. Wakati akikanusha, Mbunge wa Mbeya
Mjini, Joseph Mbilinyi alisema “na ya Rwakatare je?” akimaanisha ile
mikanda iliyotumika kumshtaki Mkurugenzi wa Usalama wa Chadema, Wilfred
Rwakatare kuwa anahusika na vitendo vya ugaidi.
Kusikia
hivyo, Mkamia alimtaka Mbilinyi atulie na akasema: “Sugu naomba ukae
kimya, halafu uelewe mimi siongei na mbwa, naongea na mwenye mbwa.”
Kauli hiyo ilisababisha mtafaruku bungeni hadi Nkamia alipoomba radhi.
Philipo Mulugo
Aliyekuwa
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo aliwahi
kukaririwa akisema kuwa Tanzania imetokana na muungano wa visiwa vya
Zimbabwe na Pemba vilivyoungana na Tanganyika.
Kauli
hiyo aliitoa mwaka 2012 wakati akiwasilisha mada katika mkutano wa
viongozi na wataalamu wa elimu katika Bara la Afrika uliofanyika nchini
Afrika Kusini.
Imeandikwa na Fidelis Butahe na Kelvin Matandiko