Ajali ya Majinjah yaondoka na wanafunzi watano UDSM
Dar es Salaam na Iringa. Wanafunzi watano
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ni miongoni mwa watu waliofariki
katika ajali ya basi la Majinjah iliyotokea wilayani Mafinga, Jumatano
baada ya kugongana na lori na kuangukiwa na kontena lililokuwa limebebwa
na lori hilo.
Katika ajali hiyo iliyoua watu 50,
mwanafunzi mmoja wa chuo hicho alinusurika kifo na kujeruhiwa.
Mwanafunzi huyo wa mwaka wa kwanza, Tupate Mosigwa alifikishwa katika
Hospitali ya Wilaya ya Mafinga lakini baadaye alihamishiwa Hospitali ya
Rufaa Mbeya kwa matibabu zaidi.
Katika taarifa yake kwa
Umma, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala aliwataja
wanafunzi waliopoteza maisha kuwa ni Eric Killeo (mwaka wa tatu), Daud
Sosten (mwaka wa tatu) na Jeremia Watson (mwaka wa pili).
Wengine
ni Frank Mbaule (mwaka wa pili) na Didimo Chiwango (mwaka wa tatu).
Profesa Mukandala alisema miili ya marehemu hao ilitambuliwa na ndugu
zao na kuchukuliwa kwa ajili ya maziko.
“Uongozi wa
chuo unatoa pole kwa wanafamilia wote pamoja na jumuiya ya chuo kikuu.
Pia, tunamtakia mwanafunzi mwingine Rafael Norbert apate nafuu baada ya
kujeruhiwa katika ajali hiyo,” alisema mkuu huyo wa chuo.
Aliongeza
kuwa, uongozi wa chuo kwa kushirikiana na viongozi wa Mkoa wa Iringa,
wanaendelea kufuatilia kama kuna wanafunzi wengine waliokuwamo kwenye
basi hilo lililochukua maisha ya watu wengi.
Wakati huo
huo, watu kutoka nchi jirani ya Malawi wamefika nchini kwa ajili ya
kutambua miili ya ndugu zao kama ni miongoni mwa watu waliokufa katika
ajali hiyo.
Ujio wa watu hao ambao walifikia katika
ofisi za ubalozi mjini Dar es Salaam na baadaye kwenda katika ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, umekuja huku miili ya watu wawili kati ya watu
50 waliofariki dunia katika ajali hiyo ikiwa bado haijatambuliwa.
Mganga
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Robert Salim aliliambia gazeti hili kuwa hadi
sasa miili 48 imeshatambuliwa na ndugu zao na imesafirishwa kwa ajili ya
maziko, huku akisisitiza kuwa hospitalini zimebaki maiti mbili tu
ambazo hazijatambuliwa.
Akifafanua kuhusu majeruhi, Dk
Salim alisema hadi jana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa
walikuwa wamebaki watu tisa waliokuwa wanaendelea na matibabu, saba
wakiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa na wawili katika
Hospitali Wilaya ya Mufindi.
Imeandaliwa na Geofrey Nyang’oro, Zainab Maeda na Peter Elias.